The Chant of Savant

Sunday 25 September 2016

Umma ujulishwe sifa za wateuliwa


            Kwa wanaokumbuka enzi za utawala wa kwanza chini ya marehemu Mwl Julius Nyerere, watakumbuka uwazi uliokuwapo karibu katika masuala mengi. Mfano, tulizoea kusikia rais akifanya uteuzi jambo ambalo hadi sasa linaendelea kutokana na kazi na mamalaka aliyopewa. Hata hivyo, tangu kuondoka kwa Mwalimu, kuna mambo mengi ya kiwajibikaji na muhimu yaliuawa kutokana na kuwa na viongozi wasio makini au wanaofuata mkumbo tu kama si kuficha maovu fulani katika utumishi wa umma. Ilifikia mahali hadi idadi na majina watu wanaokuwa kwenye msafara wa rais vilikuwa vikifichwa kutokana na kupenyezwa watu ambao hawakustahiki. Hawa walifaidi matanuzi na per diem bila sababu kiasi cha kulitia taifa hasara bila sababu ya msingi zaidi ya ufisadi wa kimfumo. Huu wakati umepita; lazima tufanye mabadiliko na kuondokana na uovu na uhovyo huu ambao sasa unaanza kugeuka wa kimfumo. Maana vyeo na fedha wanazofaidi ni mali ya umma na si mali ya kundi fulani wala si hisani wala utashi kufichua historia na sifa za wahusika. Hii husaidia umma si kupata kuwajua wahusika bali kujiridhisha kuwa haki inatendeka.  
            Hata hivyo, leo tutaongelea kero tunayopata pale tunapotaarifiwa kuwa rais au waziri amemteua fulani kufanya kazi fulani. Hivyo, kutokana na mapungufu haya, tunatoa maangalizo yafuatayo:
            Mosi, wakati mwingine huwa najiuliza mantiki ya kuutangizia umma kuwa rais au waziri kafanya uteuzi fulani wakati taarifa zenyewe, licha ya kuwa kiduchu, ni fichi na zenye mashimo kibao.     Pili, ukiachia kutaja jina la mteuliwa, cheo na tarehe, umma haupewi fursa ya kumjua mhusika. Kwa wanaokumbuka wakati wa awamu ya kwanza, uteuzi uliokuwa ukifanywa na ofisi ya rais au mamlaka nyingine zilihakikisha zinatuma nakala ya taarifa husika kwa vyombo vya habari ikiwa inaeleweka na kujitosheleza. Kwa mfano, kila mteuliwa alielezwa sifa zake kiasi cha umma kumjua vilivyo. Hata hivyo, baada ya kuingia utawala wa ruksa, mambo mengi ya msingi yalianza kubadilika na mengine hata kupotea mojawapo yakiwa kueleza historia za wateule.
            Tatu, siku hizi watu wanateuliwa; umma unaishia kujua majina yao na tarehe za kuanza uteuzi basi. Inakuwa kama ni siri ya watu au mamlaka fulani. Je nini kinafichwa na kwanini wakati huu ambapo umma unapaswa kujua watendaji wake vilivyo kama sehemu ya uwajibikaji na upashanaji habari? Nadhani uwajibikaji na uwazi ni sehemu muhimu ya utawala bora na ambavyo vinaweza kutumika kama njia ya kuminya mianya ya uhalifu utokanao na kughushi.
            Nne, kwanini mamlaka hazitaki kueleza historia ya wahusika hasa wakati huu tunapopambana na kadhia ya kughushi vyeti vya kitaaluma kiasi cha kupoteza fedha nyingi kuwalipa watu wasio na sifa kama ilivyobainika hivi karibuni kuwa kuna vihiyo na vilaza kibao kwenye nafasi nyeti katika utumishi wa umma?
             Tano, ukiachia mbali elimu, pia kumejitokeza kadhia ambapo matapeli na wahalifu wa kigeni wanakuja nchini mwetu na kuajiriwa wakati ni kosa kinyume cha sheria? Je ofisi ya rais hata kitengo cha mawasiliano kimeshindwa kuona hata jambo dogo kama hili? Najua utawala uliopita ulikuwa wa kishikaji kiasi cha watu–kwa makusudi mazima–kuficha taarifa muhimu za wateuliwa kutokana na uoza uliokuwako nyuma ya uteuzi wao.
            Sita, kama tulivyosema hapo juu kuwa baada ya kuondoka Mwalimu Nyerere, ima kutokana na uoza au kufuata mkumbo, mambo mengi yalivurugwa na kusahaulika mojawapo likiwa hili tunalojadili leo. Je serikali ya rais John Magufuli inajua kuwa imeingia mkumbo wa kufanya uteuzi huku kitengo chake cha mawasiliano kikitoa taarifa hapa kuhusiana na wateuliwa ambao wanapaswa kujulikana kwa wananchi? Wengi wa wateuliwa hatuambiwi historia zao ziwe za kimaisha au kitaaluma.
            Saba, tunadhani wahusika warekebishe kasoro hii ili kuwawezesha wananchi kuwajua viongozi au maafisa wao.  Kwani imefikia mahali hata hao wakuu wa kitengo cha mawasiliano ikulu hatujui sifa zao wala historia yao pamoja na unyeti wa taasisi husika. Iweje tujue sifa na historia ya rais lakini tusijue historia ya wateule wake? Kunaweza kujengeka imani kuwa kuna kinachofichwa hata kama hakipo.
            Nane, kutangaza sifa za wahusika na historia zao kwa ukamilifu itasaidia si kuwajua tu bali kufichua aina yoyote ya kughushi au sifa mbaya ambazo mamlaka zinazowateua hazijui; lakini baadhi ya wananchi wanazijua.
            Tisa, watakuwa kwenye jicho la umma au limelight jambo ambalo litasaidia kuwakatisha tamaa wenye madoa ambao kwa kuhofia hili wanaweza kukataa uteuzi.
            Kumi, kutangaza sifa za kitaaluma na kimaisha za wahusika ni njia mojawapo ya kuwaonyesha umma ubora au ubovu wa uteuzi husika na ni uwazi unaotakiwa kwenye nafasi za umma.
            Mwisho, tunadhani umma una haki na stahiki ya kujua wateuliwa na maafisa wengine wanaoajiriwa kwenye ofisi zake. Huu ni wakati wa kutoaminiana wala kufichana hasa ikizingatiwa kuwa kuna wahalifu wanatumia udhaifu huu kujipatia ajira na kipato huku wakiwanyima wananchi wetu wenye stahiki ya kupata vitu hivyo.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: