Saturday, 3 September 2016

Fyatueni ajira si vitegemezi


          Baada ya Mlevi mmoja mkubwa tu kuja na mpya akiwataka walevi wafyatue vitegemezi kama hawana akili nzuri, Mlevi nakuja na angalizo. Nafanya hivyo baada ya kusikia walevi wenzangu wakikamia kuoa wake zaidi ili kufyatua vitegemezi kwa vile ilmu sasa ni ya ubwete.
            Katika kuangalia kadhia nzima hasa kwenye kaya apeche alolo iishiyo kwa kutegemea washitiri, kubomu na kukopakopa, nimegundua yafuatayo:
            Mosi, walevi waliopo wanatosha sana kaya hii kiasi cha kugeuka mzigo kutokana na ukosefu wa huduma muhimu kama majumba, maji, skuli bora,, lishe bora, mishahara fiti kwa maticha, nyumba za maticha, maabara na makandokando mengine. Madawati yenyewe yanawatoa walevi kijasho kiasi cha kuchangishana na kubanana hapa na pale. Bado madarasa ambapo vitegemezi vingi kayani hasa kule mashambani vinasomea ima kwenye madarasa mabovu au chini ya miti. Maticha bado wanabanana kwenye mbavu za mbwa hadi wengine kuishi kwenye vyoo. Hapa kweli kuna mantiki ya kufyatua vitegemezi vingine ili vije kuteseka kama hivi tulivyo navyo kwa sasa vikimaliza skuli bila hata kujua kusoma na kuandika? Tunamkomoa nani hapa?
            Pili, uchumi wa kaya hii bado ni wa kujikongoja hasa kutokana na uzalishaji duni, uzalishaji wa mazao ya kikoloni almaaruf kama cash crops yanayotegemea soko moja la wakoloni ukiachia mbali kuuzwa bila kusindikwa na kuwa na Added Valued na siyo VAT.
            Tatu, uchumi wetu licha ya kuwa wa mauzauza na kilevi, umegugunwa na ufisadi kiasi cha kuparaganyika. Hapa sijagusia njuluku zinazotoroshwa kila uchao na wachukuaji waitwao wawekezaji na hasa machainizi na magabacholi.
            Nne, kaya yetu inaongoza kwa kugawa uraia wake kama njugu ukiachia mbali mipaka yetu kuzalisha walaji wengi waingiao na kutoka kama watakavyo. Nadhani machinga toka Ugabacholini na Uchainizi waliojazana kayani wanatosha kula hicho kinachotutia kiburi hadi tukadhani kuwa tunahitaji vitegemezi zaidi.
            Tano, kama nilivyogusia hapo juu, kaya yetu haina huduma za kutosha kwa wajawazito kama vile lishe, tiba bora, hospitali na zahanati vya kutosha. Kama mke wa Mlevi mkuu angekuwa amewahi kujirudufia kwenye hospitali zetu zinazosifika kwa kuwatesa wajawazito, nina hakika asingetoa ushauri huu wa ajabu ajabu so to speak. Nikikumbuka wajawazito waliowahi kujifungulia kwenye mageti ya mahospitali napata kichefuchefu kusema ule ukweli.
            Sita, ukiangalia kanuni za ukuaji, Vitegemezi ya Bangi, Ulabu na Ahadi (VIBUA) vitachukua miaka zaidi ya kumi kukuka. Hivyo, wakati vikifikia wakati wa kwenda shule, mhusika atakuwa ameishakitoa na kumwachia atayerithi ulaji wake bonge la bomu. Na pia ifahamike kuwa maisha siyo skuli tu bali mambo mengine mengi tu. Hapa hatujaongelea mzigo wa kulisha, kuvisha, kulea na kutunza hivyo vitegemezi.
            Saba, kwa sasa ahitaji kufyatua vitegemezi bali inahitaji kufyatua ajira ili kuwawezesha walevi wetu wawe na kile walichoahidiwa na msanii mmoja mkubwa aitwaye Njaa Kaya ya Maisha Bora kwa Wote (MBOWO). Boresheni skuli zilizopo kwanza badala ya kuongeza vitegemezi wakati maisha yanazidi kubana kiasi cha jana kuonekana kuwa bora kuliko leo. Mnataka kuongeza idadi ya ombaomba na machinga nini?
            Nane, kwa wale waliosoma uchumi, watakubaliana nami hata kama naongea kwa ulevi. Kinachowasumbua wanaowahimiza walevi kufyatua vitegemezi ni ile hali ya kuridhika na mafanikio ya muda. Utafyatuaje vitegemezi wakati kipato cha walevi kinazidi kushuka kila uchao? Utafyatuaje vitegemezi bila kuzingatia kuwa kaya sasa inaumia tokana na kujifyatulia vitegemezi bila mpango?
            Tisa, nawataka walevi wachukulie ushauri huu kama wa kisiasa au utani tu lakini si wa kisayansi hasa ikizingatiwa kuwa aliyeutoa si mtaalamu wa uchumi.
            Kumi, ili kupata vitegemezi vingi, inabidi walevi waoe wake zaidi ya mmoja jambo ambalo litasababisha ugomvi katika ndoa. Nadhani, kama tunataka vitegemezi vya kutosha, basi tuhakikishe vile vinavyotupwa kutokana na mimba za utotoni na zisizotakiwa havitupwi kinyama na kuuawa bila kosa lolote.
            Kumi na moja, badala ya kufyatua vitegemezi kama hatuna akili nzuri, nashauri, tupange uzazi na kupunguza kufyatua vitegemezi hasa ikizingatiwa; siku hizi kaya yetu imeingia usuhuba na vijikaya vyenye mizigo mikubwa ya ongezeko la walevi vinavyotaka turuhusu kila mlevi toka kila kaya kwenye eneo hili aende kuishi atakavyo bila kujali uraia wake. Jambo hili nalo ni bomu kwa kaya yetu hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo yenye ardhi kubwa na raslimali nyingi ambazo wahusika wanataka kuzifaidi kwa kisingizio cha ushirikiano wa kikanda.
            Japo nasema kwa nguvu ya kanywaji na yale madude mengine ambayo huwa natwika, nashauri tusifyatue vitegemezi. Pia, nashauri tusiwe tunafanya mzaha na utani kwenye serious issues kama population au idadi ya walevi. Hapa lazima tuache kuwa na vipaumbele vya kisiasa vitonavyo na hisia badala ya tafiti na takwimu. Kufyatua vitegemezi kumenikumbusha mnene mwingine uchwara aliyetoa mpya hivi karibuni akijipiga kifua eti kujenga hedikwota ya baadhi ya shirika la kidini wakati eneo lake linasifika kwa uhaba wa nyumba za watumikaji wa lisirikali pamoja na vyumba vya madarasa. Hii ni akili au matope? Japo nafanya mambo kilevi, nisingependa na wanene wafanye mambo kilevi hasa pale wanapolewa ulaji.
            Kwa leo nadhani hii dozi yatosha kulaleki!
            Mlevi mwana wa Mpigakaya…PhD (Utopian Economics).
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: