Sunday, 4 September 2016

Kilichomkweza Makonda ndicho kitakachomshusha

Image result for photos of magufuli and makonda
            Kuna kisa maarufu cha jamaa aitwaye Kiburi. Huyu bwana alikuwa na kiburi kama jina lake kiasi cha kudhani yeye ni yote katika yote bila kujua avumaye baharini papa! Tokana na kiburiburi chake, bwana Kiburi hakupenda kukanya ardhini. Kila alipokwenda alipanda farasi wake mweupe. Siku moja si bwana Kiburi akajisahau na kumfanyia kiburi farasi wake. Farasi kwa hasira aliamua kupiga mateke na kuacha kumbeba kiasi cha Kiburi kurejea nyumbani akilia kwa maumivu na uchovu vyote vikiwa matokeo ya kiburi.
            Kwa wanaojua mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alivyoibuka tokana na siasa za majitaka za zama zile, hawana wasi wasi; siku atapotea hivyo hivyo kisiasa. Tuliwaona wengi. Wako wapi akina Augustine Mrema?
            Hivi karibuni akiaga miili ya polisi waliouawa na majambazi, Makonda alikaririwa akisema “nakuagiza Kamanda wangu Sirro mkiwapata watu wenye nia kama hizo msiwaache hata watu wa haki za binadamu waseme.” Kisheria, haiwezekani kujua nia ya mtu hadi upate ushahidi wa kutosha na si wa kusikia bali kutokana na jaribio au attempt lakini si hisia zako au za wengine na wala si kutokana na maagizo ya hasira na sanaa za kisiasa bali taratibu za kiupelelezi kisheria. Pamoja na kuwa agizo lilitolewa na layman, asiyejua sheria. Kufanya hivyo, kunaweza kusababisha uonevu hata uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu. Vyombo vya dola havipaswi kufanya kazi kwa maagizo ya wanasiasa au watu wasiojua hata mipaka ya madaraka yao bali sheria na utaalamu vilivyo nao. Makonda alikwenda mbali na kuita haki za binadamu uchizi na wendawazimu bila kuthibitisha madai yake. Hakuna anayefurahia mauaji ya polisi au mtanzania yoyote. Makonda alipoteza fursa ya kuonyesha uongozi na ukomavu.
            Wengi walishangaa kusikia kauli za ajabu kiasi cha kuhoji welewa na usomi wa mhusika. Mbona walikuwapo wengi tena walio karibu zaidi na marehemu? Tumemsikia mkuu wa jeshi la polisi akisema kwa uchungu bila kutoa amri za ajabu. Tumemsikia waziri wa mambo ya ndani; lakini hakutoa maagizo ya kiimla. Kimsingi, Makonda anapaswa kuvuliwa nafasi ya ukuu wa mkoa na kushitakiwa kwa kutishia haki za binadamu. Ajabu ni akina Makonda hawa hawa wanaoimba kulinda amani wakati wakitoa amri za kuivunja. Bila kutenda haki na kufuata sheria huwezi kuwa na amani ya kweli.  Hatuna haja ya kutetea waovu. Pia, hatuna haki ya kuwaonea bali kuwashughulikia kisheria.
            Makonda alipaswa kuhimiza vyombo vya dola kufanya kazi yake kwa weledi bila kumuonea wala kumpendelea mtu. Kuonyesha asivyojua dhana nzima ya utawala bora na wa sheria, aliongeza, “Kama wanataka kulalamikia haki za binadamu, basi waje kwangu.” Waende kwake kufanya nini na kama nani? Sijui kama Makonda anajua; yeye si bosi wa wanaharakati wa haki za binadamu. Bahati nzuri, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeishamwita. Kama tulivyosema awali, THBUB itoe mapendekezo kwa rais yakiwemo kubatilisha uteuzi wake, kumfikisha mahakamani  ili kutoa onyo kwa maafisa wengine wa serikali kujali na kuheshimu haki za binadamu bila kujali ukubwa wa vyeo vyao.
            Tuchukue fursa hii kuwataka wapenzi na watetezi wa haki za binadamu, kulaani amri za Makonda aliyewataka waandamane kupinga mauaji ya polisi. Hii si kazi ya watetezi wa haki za binadamu. Mbona raia wengi wanauawa na majambazi? Mbona, huko nyuma, polisi waliua wananchi wasio na hatia lakini watetezi wa binadamu hawakuandamana zaidi ya kuishauri serikali kufuata sheria na kulinda na kuheshimu haki za binadamu? Watetezi wa haki za binadamu si vikaragosi vya ktumiwa na wanasiasa kama ambavyo Makonda anataka wawe. Pia watetezi wa haki za binadamu si mashabiki wa vyama bali wao humtetea yoyote awaye hata awe mhalifu ilmradi ni binadamu.
            Mimi ninayeandika, nilichukizwa na ung’ang’anizi wa madaraka wa muda mrefu wa Muamar Gaddafi kule Libya; ingawa sikukubaliana na namna alivyoangushwa na serikali za magharibi kulipiza visasi na kulinda maslahi yao. Wala sikukubaliana na namna Gaddafi alivyokamatwa na kuuawa kinyama. Nilitaka afikishwe mahakamani ili mahakama iamue kama alikuwa na hatia ya makosa aliyotuhumiwa au la.
            Hawa wanaotuhumiwa kuua polisi bado ni watuhumiwa tu. Chini ya dhana ya presumption of innocence bado ni watuhumiwa hadi pale wakapofikishwa mahakamani, kusikilizwa, kujitetea, kutolewa ushahidi na kupatikana na hatia au la. Hata wakikutwa na hatia, hawatapigwa mawe wala nini bali watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Taifa la amani na huru kama Tanzania haliwezi kuendeshwa kwa jazba za watawala. Litaendeshwa na kanuni na sheria kama zilivyoainishwa katika katiba na vitabu vingine vya sheria.
            Kwa vile rais John Pombe Magufuli ameonyesha kutovumilia wateule wake wanaovurunda, anangoja nini kumwajibisha Makonda au kuna black sheep na sacred cows kwenye serikali yake? Tulishaonya na si mara moja wala mbili; kuna siku Makonda atamuaibisha bosi wake kiasi cha kuanguka ghafla kama alivyopanda.
            Ukandamizaji wa haki za binadamu na kutofuata utawala wa sheria si jambo jipya kwa Makonda. Rejea alivyowaweka watendaji wa manispaa ya Kinondoni ndani kinyume cha sheria kabla ya kuwalisha wengine viapo bila stahiki.
            Kilichomkweza Makonda ndicho kitakachomshusha.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: