Wednesday, 14 September 2016

Ahadi za kunasa wazungu wa bwimbwi vipi?

Image result for katuni za wauza unga
          Baada ya kushuhudia zinavyozikwa kashfa kama vile Escrow, Lungumi, UDa na nyingine nyingi, kijiwe kimeamua kukumbushia na kuhoji ilikoishia vita ya kuwanyaka wazungu wa bwimbwi. Baada ya zungu la ungu jirani yake na Kapende kununua bonge ya nyumba anayopanga Kapende, anaamua kukilazimisha kijiwe kurejea kadhia hii ambayo wanene wengi wanaiogopa.
            “Mwenzenu sina raha leo,” Kapende analalamika. “Kwanini ndugu yangu na nini kimekusibu? Anauliza Mbwamwitu.
            Kapende anajibu, “mwenzenu sina pa kulala baada ya kupewa notisi ya haraka ya miezi mitatu baada ya zungu la unga jirani kununua nyumba kana nane hivi ili kujenga casino kwa ajili ya kuchezesha kamari.”
            “Wewe una bahati wala hupaswi kulalamika. Hukuwasikia wenzako wa Migomigo Kota walivyokuwa wametapeliwa na site hadi mzee mwenye dokta Kanywaji akaamua kuingilia na kuokoa ngoma? Nenda kwa dokta Kanywaji upeleke malalamiko. Huyo dingi wa bwimbwi atanyakwa kama wale jamaa zetu wa NSSF waliokuwa wakitaka kutuuzia uwanja Kigamboni mabilioni. Sijui nao wameishia wapi?” anajibu Mipawa huku akibwia gahawa yake.
            “Wale miji ya NSSF sasa naoze pango hadi sirika yao ya bedroom napata bwana nyingine. Kama na uza bimbi nasugulikiwa kama hii kuba ya NSSF iko zani sasa kaya kuwa huru kabisa bila bimbi. Mimi dhani ile uza bimbi hapa sikwa. Veve nafanya chezo. Ile honga data na kubakuba nyingine wakati hii ya NSSF kuwa choyo kula peke yake dio maana nasikwa natupa pango rahisi.”
            Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akibofya ki-Samsung 7 Galaxy anakiweka pembeni na kula mic, “ushauri wako brother Mipawa ni mzuri ila ufahamu kuwa hapa kwenye kaya–pamoja na vitisho na ukali wa dokta Kanywaji–kuna wadude hawaguswi. Hawa ni wale wa Escrow, Lungumi na UDa. Hebu jiulize. Tangu aingie kwenye ulaji hawa wajambawazi wamefanywa nini zaidi ya yule wa UDa kugawiwa mangwalangwala yaendayo kasi? Niambie ni wauza bwimbwi wangapi wamekamatwa wakati wabwiaji maeneo ya Lumumba, Migomigo na kwingineko wanazidi kuongezeka?”
Mpemba anakula mic, “yakhe nkubaliana nawe. Hii vita ya wauza bwimbwi ni danganya toto wallahi. Mie alipoapishwa huyu waziri wa mambo ya chumbani apendaye kuvaa magwanda na bendera ya kaya nilijua ndo kilikuwa kiama cha wauza bwimbwi nisijue ataja wagwaya na kukimbilia kuvaa magwanda ya ndata.”
            Mijjinga anamchomekea Mpemba na kusema, “hii kitu ogopa sana. Huu mtandao si cha mtoto. Mara hii mmesahau alivyodedishwa Amina Chifwupa alipojitiatia kula huku na kule? Nani awakamate wauza bwimbwi wakati wao ni lisirikali ndani ya lisirikali. Hamuwaoni wanene wa bwimbwi wanaotanua chamani au mpaka tutaje majina?”
            Mgosi Machungi aliyekuwa kimya akivuta tasbihi yake anaamua kula mic, “usemayo ndugu yangi ni kwei tupu. Kia siku wanasema titakamata wauza bwimbwi akini hatuoni hata mmoja akikamatwa. Wakijifaagua wanakamata wabwiaji ambao nao wameishapigika. Kwanini wasiwabane hao wabwiaji wakawaonyesha wanaowauzia nao wakawaonyesha wanaowauzia hadi ndata wanaowalinda kama kwei wamezamiia au ni mapambano hewa hasa ikizingatiwa kuwa kaya yetu ni ya kia kitu hewa?”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kula mic, “nami nakubaliana na Mgoshi hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa wahusika wanasema mengi na kutenda machache. Kunasa wauza bwimbwi ni rahisi kama alivyosema Mgoshi. Kamata wabwiaji wakuonyesha wanaowauzia na wanaowauzia wawataje wanaowauzia hadi mazungu yenyewe. Pia nashauri wahusika waangalie namna ya kuwabana matajiri uchwara wa kuibuka ghafla bin vu wataje walivyochuma utajiri wanaoringia wakati ni jinai tupu. Bila kufanya hivi, tunapoteza muda; na hakuna haja ya kutupigia mikelele na vita dhidi ya bwimbwi wakati biashara yenyewe inazidi kushamiri hasa wakati huu dokta Kanywaji alipoamua kubana kila kitu.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kula mic, “da Sofi kumradhi sana. Ngoja nikuchomekee kidogo,” kabla ya kuendelea kijiwe hakina mbavu namna mheshimiwa Bwege anavyoomba kumchomekea da Sofi.
            Anaendelea, “kusema ule ukweli, sidhani kama biashara ya bwimbwi itakuja iishe hasa ikizingatiwa kuwa watumiaji wengine ndiyo hao hao wanaopaswa kupiga vita balaa hili. Mara hii mmesahau namna mzee wa Mjengo Jobless alivyosema kuna waishiwa tena waliopo mjengoni wanavyobwia hii kitu nao wasikanushe? Hapa unategemea nini kama siyo kufungana kamba. Kamateni mtutangazie kama mnavyotangaza waliotumbuliwa bila kujali ukubwa wa vyeo vyao. Simple.” Anapiga chafya na kuendelea, “kama walivyonena wanenaji wa awali, bwimbwi, Lungumi, Escrow na UDa ni sirikali ndani ya sirikali tena yenye siri kali sana tu. Heri wajinyamazie kama ishara ya kushindwa.”
            Mzee Maneno anakula mic, “kama tumeshindwa kama kaya kupambana na mibwimbwi basi wanyonge tumekwisha. Kwanini tusitumie ujasiri tunaotumia kuwachoma vibaka tuwachome wazungu wa bwimbwi ambao wengi wanaishi nasi’ na tunawajua kwa majina hata sura kama kweli tunachukia jinai hii? Hata dogo wa wendawazimu wa haki za binadamu simsikii akilaani wauza bwimbwi au kule hakuna ujiko na kama upo ni wa hatari?”
            Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga, si akapita teja moja. Wote tuligeukiana na kuangaliana kwa mshangao hasa ndata alipopita akimfuata nyuma bila kumtia nguvuni! Ama kweli ukishangaa ya Escrow, Lungumi na UDa, utaona ya wazungu wa unga!
Chanzo: Tanzania Daima leo Jumatano.

No comments: