The Chant of Savant

Wednesday 14 December 2016

Kugomea uraia pacha ni kujikwamisha

Image result for bendera ya india

            Hivi karibuni, baada ya kubainika kuwa watanzania wanaochukua uraia wa kigeni hupotgeza haki muhimu ya kumilki ardhi, kumekuwapo mjadala kwenye mitandao ya kijamii. Tokana na unyeti wa suala zima, napenda kutoa maangalizo yafuatayo kama mwana diaspora:
            Kwanza, nilishangaa kuona kuwa bado tunaendelea kuwa na mawazo ya kijima ya wakati wa vita baridi ambapo nchi za magharibi na mashariki zilitutengeneza kuwa kama maroboti yenye kushikiana na kuchukiana bila hata kujua ni kwanini. Zama zile tuliogopa na kukata uraia pacha kwa hofu ya kuweza kuingiza wapelelezi na mawakala wa maadui zetu kutuchunguza na kuhatarisha usalama wetu. Je kwa sasa tunahofia nini zaidi ya kutumia mabaki ya ukoloni (colonial carryovers)? Ajabu, wakati sisi tunabaniana uraia pacha, wale waliotutawala na kutujengea shaka na uadui wanaruhusu! Ukiachia hili, sisi tuna nini cha kuhofia wakati ni nchi tegemezi zilizoharibiwa kiasi cha wananchi wake kuzikimbia kutafuta riziki kwingine?
            Pili, inapaswa kufahamika kuwa wakati sisi tukisuasua na kubaniana uraia pacha, nchi tajiri hazizuii wageni waliochukua uraia wao kubaki na uraia wao wa kuzaliwa. Kama ni kuogopa kuhujumiwa basi hizi ndizo zingeogopa hili kwani zina mali na fedha nyingi za kupoteza. Nchi nyingi za kiafrika zinategemea fedha inayotumwa na wana diaspora. Kwa mfano gazeti la Mail and Guardian (2 Juni, 2015) linaripoti kuwa nchi za Eritrea zinategemea pesa toka kwa diaspora kwa kiasi cha  38%, Cape Verde, 34%, Liberia , 26%, na Burundi 23% ikilinganishwa na pato la taifa. Hii si pesa kidogo na rahisi kwa nchi kuipata. Japo sina takwimu za Tanzania inaingiza kiasi gani, kutokana na uzoefu binafsi, najua inaingiza fedha zinazoweza kuelezwa kuwa zinakwenda kwa watu binafsi. Huu ni ushahidi kuwa wana diaspora wana mchango mkubwa kwa nchi zao jambo ambalo linapaswa kuwa kama njia mbili yaani nipe nikupe (twoway traffic).
            Tatu, kuonyesha kuwa bado tunaendelea na mawazo ya kijima, kuna taarifa nyingi toka Tanzania ambapo wageni wanaopewa uraia wa Tanzania huwa hawabanwi kama watanzania wanaochukua uraia wa kigeni. Wengi wa wageni hawa hubaki na uraia wao kiasi cha kutumia status hii kuifilisi na kuiibia Tanzania wakati ikuzuia wazawa wake kuwa na uraia pacha. Mifano ya wahalifu walioibia Tanzania mabilioni ya fedha kama vile Chavda Group ambaye mwaka 1993 aliyetumia mashamba ya mkonge kukopa fedha na kuyatelekeza na Saileth Vithlania wa kashfa ya rada inaweza kukueleza hali ikoje ukiachia mwingine wa hivi karibuni Hermant Patel aliyejitwalia ardhi ya Tanzania ipatayo hekari 35,000 na kwenda ulaya kwenye mabenki kuiweka kwenye poni. Je tunamkomoa nani; na ili iweje au ni kwa vile matapeli na wahalifu wa kimataifa wanashirikiana na maafisa wa juu wa serikali kama ilivyokuwa kwenye kesi mbili hapo juu?
            Nne, sheria ya ardhi ni kimeo. Inawazuia watanzania waliochukua uraia nje kumilki ardhi wakati ikishindwa kuwadhibiti waliochukua uraia wa Tanzania kuutumia kuiibia kama tulivyoonyesha hapo juu. Je mhusika akiwa na makaburi ya wazazi wake nayo serikali itayachukua? Je kwa zuio hili, ni busara kwa diaspora wenye uraia wa kigeni kuwekeza Tanzania wakati hawakubaliki? Mbona nchi nyingine za kiafrika kama Rwanda zimeruhusu uraia pacha? Nadhani Tanzania bado tuna mawazo ya kizamani ya enzi za vita baridi.
            Nini kifanyike?
            Kwanza, kushawishi serikali ya Tanzania kuruhusu uraia pacha au kuzi-lobby nchi zilizoendelea zilizotoa uraia kwa watanzania kuhakikisha watu wao wanapodhulumiwa ardhi nazo zisitishe misaada na ushirikiano hata ikiwezekana kuingilia kati.
             Pili, kuna haja ya kujiuliza: Kwanini watanzania wanachukua uraia wan je? Wanafanya hivyo ili wapate fursa ambazo hazipo nyumbani. Serikali ambayo inapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kuweka mazingira mazuri kwa watanzania kupata fursa kama hizi haipaswi kupewa mamlaka ya kuamua nani awe na uraia pacha au la. Kwani, kimsingi, serikali ndiyo chanzo cha haya yote. Watu wanataka elimu bora, maisha safi, kuaminika wanapotaka kusafiri nje na mengine mengi tu. Wekeni mazingira bora kwanza ndiyo mkataze watu kuwa na uraia pacha. Mbona nchi tajiri zenye kila huduma bora zinawaruhusu watu wenu kuchukua uraia wao, kufaidi huduma zao na hata kutuma fedha huko wanakonyimwa uraia pacha?
            Tatu, kwa mjibu wa mtandao wa dualcitizenshipmalawi.blogspot.ca nchi zipatazo 23 za kiafrika zinaruhusu uraia pacha. Hivyo, Tanzania inapaswa kujifunza toka kwa nchi kama hizo tena jirani kama vile Kenya na Rwanda zinazoruhusu uraia pacha na namna zinavyofaidika nao ikilinganishwa na kuupiga marufuku. Bila kubadilika, Tanzania itajikuta inaruhusu raia wa nchi jirani ambao watatumia fursa ya kujipatia ardhi Tanzania na kubaki na uraia wao huku watanzania wa kuzaliwa wakinyimwa ardhi. Rejea kilichotokea baada ya RPF kuchukua madaraka nchini Rwanda, wanyarwamnda wengi waliokuwa wamepewa uraia wa Tanzania waliutelekeza na kurejea kwao bila kizuizi cha kuhitaji kuomba upya kama ilivyo kwa Tanzania ambayo ilikula hasara kwa kuwasomesha na kuwatunza tangu wengine wazaliwe hadi walipoondoka.
           Nne, Tanzania iache kupoteza muda kuwazuia wananchi wake wa kuzaliwa uraia wa pacha wakati ukiugawa kama njugu kwa matapeli wa kimataifa wanaoutumia kuhijumu tofauti na wana dispora wanainufaisha kwa kutuma fedha kwa watu wake. Pia ifahamu kuwa Afrika kwa mtu yeyote mweusi ni mama ambayo hakuna namna yoyote ya kuitenganisha na watoto wake kwa sababu za kijima na wakati mwingine hata ujinga na roho mbaya. Kwanini wakenya na wanyarwanda, kama si roho ya korosho waweze Tanzania ishindwe? Nadhani uraia pacha ni haki na si suala la nani watake au kutoa kama ofa. Wote tunahitajiana. Rekebisheni kinachowasukuma watu wenu kukimbilia nje uone kama kuna atakayelalamika.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

3 comments:

Anonymous said...


Salaam Mwalimu Mhango,
Wache nianzie katika paragraf yako uliyomalizia maandishi yako pale ulipoandika "Pia ifahamu kuwa Afrika kwa mtu yeyote mweusi ni mama ambayo hakuna namna yoyote ya kuitenganisha na watoto wake kwa sababu za kijima na wakati mwingine hata ujinga na roho mbaya".Ukwli uliokuwa wazi kwa maoni yangu ni kwamba NI ROHO MBAYA tu ambayo iliyojikita katika kadhia hii ya URAIA PACHA.Kwa kwa kukumbusha tu Mwalimu Mhango ni kwamba hadi hii leo,inapotokea kwa Mtazania mwenye uraia wa Tanzania kuwepo ughaibuni ambae hatambuliwi rasmi kiserikali kuwepo kwake ughaibuni,inapotokea raia huyu kuwa na matatizo binafsi hata ya kubadilisha Pasi yake baada muda wake kumalizika na akaenda ktk Ubalozi wake utakuta maofisa husika Ubalozini hawampokei Mtanzania huyo kama yupo nyumbani kwake,lakini atakutana na maswali ya ajabu ajabu kana kwamba ni marufuku kwa Mtazania kusafiri nje ya nchi yake na hata kutothaminiwa kama Mtanzania na wakati Ubalozi pamoja na kuiwaklisha nchi lakini muhudumiwa wa mwazo na wa mwisho ni Mtanzania.Lakini balozi zetu hatuyaoni hayo na hata wakati mwingine utakuta pia kuna Uzanzibari katika baadhi ya balozi zetu,kwa maana akiwa ofisa wa ubalozi kutoka Zanzibar na ane muhudumiwa ni Mzanzibari utakuta kwamba Mzanzibari huyo atapewa huduma hiyo kwa wepesi sana na Mtazania alietoka Tanganyika atakutana na vikwazo,kunyanyaswa na kudhalilishwa ndani ya nchi yake mwenyewe(UBALOZINI)ka sababu tu ni Mtanganyika.
Na hata tukiauchia mbali ufafanuzi wako wa wakati wa vita baridi hapana budi ukweli hapa usemwe kwamba Serikali yetu haina aina yoyote ile ya kuwapenda,kuwakubali na kuwasapoti wananchi wake wenye uraia wa Tanzania waliopo Ughaibuni labda Mtanzania huyo awe na rangi isiyokuwa nyeusi.Nadhani Mwalimu Mhango,umeshuhudia mara nyingi tu saikolojia ya wananchi wenye kupendwa na serikali zao mara tu wananchi hao wanaporudi katika nchi zao za asili mara tu ndege inapokaribia kutua uwanja wa ndege jinsi gani wanavyokuwa na furaha kwamba wanarudi nyumbani. Na utaona jinsi gani wanavyopokelewa na maofisa wao wa uhamiaji katika nchi zao bila ya kusumbuliwa,kudhalilishwa au kubughudhiwa.Lakini kwa Mwananchi wa Tanzania anapotuwa uwanjani katika nchi yake mwenyewe angalia jinsi gani anavyopokelewa kwa kudhalilishwa,kunyanyaswa na kubughudhiwa kana kwamba habebi Pasi ya kitanzania na utashangaa jinsi gani wageni wanavyopokelewa,kukaribishwa na kupokelewa utadhani wao ndio wenye nchi yao.
Sasa ikiwa huyu ni Mtazania Asili mwenye uraia wa kitanzania anabughudhiwa na kunyanyaswa na serikali yake NDANI YA NCHI YAKE MWENYEWE na hata ukiisoma saikolojia ya baadhi ya Watanzania walioutema Uraia wao pamoja na kupigania nafasi za kuboresha Mustakbali wao Ughaibuni lakini Watanzania hao hawakuwa wanaridhika na jinsi gani wanavyonyanyaswa,kutothminiwa na kudharauliwa wanaporudi kwao wakiwa wamebeba uraia wa kitanzania.Na wameelewa kwamba ufumbuzi ni kuchukua uraia wa nchi zilizoendelea kwani kwa uraia huo huwa wanajikuta wenye kuthaminiwa na kuheshimiwa wakiwa na Pasi za ughaibuni,na matokeo yake kutouthamini uraia wa Tanzania.
Inaendelea........

Anonymous said...

Kama ulivyo fafanunua katika kadhia hii mapunguvu yake na kutoa usgauri wa busara wa kulitatua swala hili na kuwafanya Watanzania wenye uraia wa ughaibuni kuwa FAHARI na nchi yao na uraia wao wa asili umefika wakati kwa serikali yetu kuwaondolea kero na shindikizo la moyo Watanzania kwa sheria hii ya ujimi na ya roho mbaya ya kutoruhusu uraia pacha ili tusiwafanye kuwa na nomgwa na nchi yao na tusije tukakipoteza kizazi cha awali na kijacho cha kitanzania kilichozaliwa Ughaibuni.Tunaziona nchi zingine jinsi gani wanavyo uthamini mchango wa raia wao waliopo ughaibuni wenye uraia pacha kwa kila nyanja kwa kuwaita nyumbani kila baada ya muda serikali unao upanga na kufanya mkutano maalum ambao serekali hizo uwaita raia zao hao kuja kushiriki kwa kubadilishana nao maoni na kuchangia majaribio yao mbali mbali waliyopata Ughaibuni kwa maendeleo ya nchi na maendeleo yao wananchi hao wa ughaibuni.Je serikali yetu italipa umuhimu mchakato huu wa uraia pacha kwa manufaa ya nchi na watanzania waliopo Ughaibuni kwa kutoa Uraia pacha?

Mwalimu Mhango,wacha nifungie maandishi yangu haya kwa kuchukua nafasi hii ya kukupa salamu za utangulizi za mwaka mpya na sherehe za Krismasi wewe na familia yako.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon,
Karibu tena kwenye uga wako na michango yako motomoto. Sitaki niharibu uhondo uliotoa. Ila naweza kusema neno moja, sisi waswahili ni wabaguzi kuliko hata magabacholi hasa ikizingatiwa kuwa tunabaguana sisi kwa sisi wakati na wengine wote wakitubagua kwa kujificha kwenye siasa, biashara na hata dini. Hili la balozi zetu sikulijua kwa sababu huwa siendi huko na wala sioni hata kwa nchi maskini na ombaomba kuwa na ubalozi. Kama hapa Kanada tuliletewa uaji lililomtesa dk Ulimboka kuwa balozi. Huyu ni mhalifu aliyepaswa kuwa ukonga na si ubalozini. Wanateuana kwa kujuana na kuhongana. Unategemea nini. Kikwete alinyea nchi kiasi cha kugeuka kama danguro huku akiwajaza vimada na marafiki na jamaa zake ubalozini. Zetu si balozi bali magenge ya wahalifu yaliyoko nje kulinda uhalifu wa waliowateua. Najua siku hizi wanachunguza na kupeleleza mitandao. Acha wasome hapa wafanye watakavyo. Kugomea uraia pacha usiwatishe. Kuna siku wataachia. Kwa wale waliokwishachukua uraia wa nje, nendeni mkawekeze kwenye nchi jirani mtakapopokelewa. Kwani mlango mmoja ukifungwa mia inafunguliwa. Wao wameona ardhi ni big deal. Nani anaihitaji sana wakati hakai kwenye ardhi hiyo. Acha magabacholi waendelee kuifaidi kwa kuipora na kukopea wakati waswahili wenzetu wakishikilia majungu na roho mbaya wakati wanazidi kuumia. Kama una vijisenti vyako na unataka kurejea Afrika nenda Botswana, Malawi hata Namibia ukawekeze au Zimbabwe baada ya Mugabe kurejesha namba. So, simple. Kenya na Uganda au Rwanda sikushauri. Usalama wa kule ni mdogo na ubaguzi upo juu sana. Kama waswahili wameweza kuwapa uraia al shabaab kama Kinana na wenzake na kufanikiwa kuwaruhusu kuwatawala wewe ni nani? Watawala wetu wengi wana roho ya korosho na hawasomi alama za nyakati. Ndiyo maana wanagomea uraia pacha kwa waswahili wakati wakiuruhusu kwao na ndugu zao na magabacholi wao. Hata hivyo, tusikate tamaa. Tuendelee kukomaa. Maana ni haki yetu.