Friday, 24 March 2017

Bashite Kachape Kazi


Mwanangu Poo Makonda, nakuita usikie
Jinsi ninavyokupenda, ya watu usisikie
Najua wanakuponda, mwanangu usijutie
Wewe mwanangu mpenzi, niliyependezwa naye

Jinsi ninavyokupenda, wewe nenda utulie,
Najua kimewapanda, acha na kiwashukie
Awaye akakuponda, rungu limuangukie
Na bastola chukua, ndata wakusindikize

Mkono nitakuunga, nenda kazi jichapie
Najua wanakung’ong’a, ya vyeti uniachie
Hakuwa wa kukufunga, mambo yote niachie
Nchi nimeshika mimi, nani wa kunichezea?

Hata kama ulighushi, wao chawauma nini?
Umefoji si uzushi, wao yawahusu nini?
Ewe mwana shika mchi, adui dunda kichwani
Hongera kwa kazi njema, kuwavamia wanywanywa

Mwanangu na usitishwe, babayo najiamini
Mzigowo unitwishe, wa kunikabili nani?
Atayejitia ubishi, nisimNape kwanini?
Hii ni himaye yetu, mwanangu tulie ule

Nasema najiamini, sitishwi na wapuuzi,
Nimeushika mpini, ole wako uniudhi,
Takupa ngeu kichwani, ukuondoke uchizi,
Wa kudhani uko huru, not to that extent

Nenda ukachape kazi, tumbue unaotaka
Na usifanye ajizi, fanya utakalotaka
Timiza yako mapenzi,  fanya roho nataka
Hata ukitaka benzi, wabane wauza bwimbwi

Atayekukatalia, msakizie miunga,

Utakayemchukia, mwambie auza unga,
Lazima kuwawakia,watishie kuwafunga,
Sema watatumbuliwa, wale wenye madaraka

Mwanangu ninakuasa, na uwe na roho ngumu,
Washilawadu kwa visa, wao ni wasaga sumu,
Ulaji ni wetu sasa, hili ndilo la muhimu,
Bashite shika mpini, wabaya wakolomije

Usimwope yeyote, tuko juu ya sheria,
Utachotaka chochote, mie nitakufanyia,
Utapokuwa popote, mie nitakutwangia
Nitapokuwa popote, shurti kukusifia.

Ewe mwanangu Daudi, maneno yangu yashike,
Wewe ongeza juhudi, ewe mwana wa Bashite
Uzidi kutahidi, ili wao niwasute
Chapa kazi we Daudi, Albert wa Bashite

Nkwingwa kajagi lulu, kubyala gawiza,
Ukitaka kaa ikulu, hili bado naliwaza,
Sitataka kukufuru, ila mambo twayaweza,
Huoni wanavyonywea, nilipomNape mtu?

Acha nende bandarini, nenda kuwaibukia,
Hata kama usanii, kama wanavyodhania,
Hukuona ule mchuma, unayo namba bandia?
Kamera zilishakula, nani atafuta picha?

Muhimu ninakwambia, usiwaamini watu,
Kama ulivyowambia, hautatishwa katu,
Bora mkwara kutia, asikuchezee mtu
Waclouds watakaovimba, uutembeze undava.

Nimekwisha kupa ndata, sasa nini kikushinde?
Nenda wapigishe kwata, ata tume waunde,
Habari nikizinyaka, natumbua tena punde,
Hii ni himaye yetu, ngosha twanga mzigo.

Wadai  una nyingi mali, wataka uwe kapuku?
Wanataka maadili,  Bashite we kula kuku
Jipigie zako dili, kutawala ndiyo huku,
Bashite chapa mzigo, na ufanye utakavyo.

Wachimvi uwapashe, wajue umoja wetu,
Lazima uwasomeshe, wajue ukuu wetu,
Wala usiwakopeshe, uwapashe kila kitu
Wewe mwana mimi baba, wote ni kitu kimoja.

Wewe umo ndani yangu, nami nimo ndani yako,
Kilicho chako ni changu, kilicho changu ni  chako,
Ufanyacho ndicho changu, huu ni wosia wako
Sisi ni kitu kimoja, kututenganisha mwiko.

Baba kampenda mwana, hadi kampa ukuu
Ni wa mfalme mwana, aliyejaa ukuu,
Atakalo litafana, autumia ukuu
Baba kampenda mwana,  katoa kondoo wote

Mwana siyo kama Yesu, yule mwana wa Josefu,
Huyu ni Dav Bashite, tena mwana mshaufu,
Amesimama kidete, kufaidi utukufu
Kondoo wamfie, siyo yeye awafie,

Baba kampenda mwana, kasulubisha kondoo,
Kwa sababu yake mwana, na wafe wote kondoo,
Mradi apone mwana, kwa gharama ya kondoo
Haya mapenzi ya baba, kwake mwanae kipenzi.

No comments: