Sunday, 26 March 2017

Kashfa ya Makonda: Inatakiwa busara si ubabe

Image result for photos of magufuli na makonda
Kauli ya rais John Magufuli kuhusiana na sakata la mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda kughushi vyeti vya kitaaluma imestukua, kusikitisha, kukwaza na kushangaza wengi ukiachia mbli kumtia aibu yeye mwenyewe na mamalaka ya rais. Hata kabla ya mstuko na hasira kwisha, rais alimfukuza kazi waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alivuliwa madaraka kwa kumgusa kipenzi cha rais, jambo ambalo ni kinyume na matarajio ya watanzania na ni hatari. Kama alivyosema mwenyekiti wa Wamilki wa Vyombo vya habari Reginald Mengi, kilichotokea ni aibu kwa taifa hivyo, hakikwepi lawama. Hata hivyo, wanaomlamumu Magufuli wanafanya makosa kutokana na faida itokanayo na hatua yake ya kumkingia kifua ambayo imeonyesha sura ya rais na namna ya utendaji wake. Rais alijigamba kuwa yeye ni rais anayejiamini na watu wasipoteze muda kujadili personalities naye akaishia kujadili hizo personalities kama wale aliowalaumu. Nadani kujiamini tu bila kuaminika inaweza kuwa bure.
  Licha ya kutostahili, kauli ya Magufuli haikutegemewa kulalia upande mmoja; na ni ya kulaaniwa kwa hasira na uzito unaostahili. Je nani anamtumia nani kati ya Magufuli na Makonda? Haiwezekani, kwa mfano, mtu atuhumiwe kughushi vyeti ambalo ni kosa la jinai, halafu rais anayejipambanua kama mpambanaji dhidi ya jinai hii amkingie kifua hata kwa kuwaumiza wengine. Huku ni kijichanganya na kujipiga mtama kwa lugha ya watoto wa mjini.
 Haiwezekani Makonda huyu huyu awatukane Waheshimiwa Wabunge lakini bado rais huyu huyu amkingie kufua kusiwe na mgongano baina ya mihimili hii miwili ya dola. Sijui bunge na wabunge waliotaka kumwajibisha Makonda wanajisikiaje. Haiwezekani Makonda huyu huyu avamie kituo cha Televisheni usiku wa manane akitumia vyombo vya dola kienyeji ukiachia mbali kitendo chake kuvunja katiba bado akakingiwa kifua na rais na kusiwe na namna. Wakati rais akimkingia kifua, waziri mhusika alilaani kitendo hiki jambo ambalo ni kama serikali kupingana yenyewe. Hapa lazima kuwa na uhusiano wa wawili hawa usio wa kawaida. Ama kweli mwenye mapenzi haoni! Kama haitoshi, bunge limetuma kamati yake. Bila subira wala simile, rais anamtetea mtuhumiwa ambaye hata waziri wake ameunda tume ya kuchunguza sakata hili. Sijui kama kauli ya rais haitaathiri matokeo ya uchunguzi. Maana rais ameishaonyesha upande wake katika sakata hili. Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Bunge Peter Serukamba alikaririwa akisema kuwa Kamati ya Bunge itachunguza na kutoa ushauri kwa serikali. Sijui ushauri gani huo ambao utamshawishi Magufuli wakati alishatoa hukumu hata bila kungoja kusikia matokeo na ripoti za tume husika.
Je ni kwanini Magufuli ameamua kufa na Makonda ilhali akiwatumbua wenye makosa madogo kuliko yake? Je Magufuli anatoa mfano gani kwa taifa? Si rahisi kujibu swali hili. Wapo wanaodhani kuwa ni sababu ya ukabila. Hata hivyo, ukiangalia namna Magufuli alivyomtimua Waziri wake wa kwanza wa Mambo ya Ndani Charles Kitwanga, unaondoa dhana hii japo lolote linawezekana. Je ni kwanini Magufuli ameng’ang’ania Makonda pamoja na kuchafuka hivyo? Kitendo cha Magufuli ni kwamba anatumia mamlaka yake kwa upendeleo na visasi. Rejea alivyonyamazia jinai ya kuwekwa ndani kwa Mbunge wa Arusha Godbless Lema kwa miezi minne kinyume cha sheria.
Je sababu inaweza kuwa kujuana kunakotokana na mmoja kujipendekeza na kumuabudia mwenzie? Inawezekana; hasa ikizingatiwa kuwa Magufuli ni aina ya viongozi wanaopenda kuabudiwa jambo ambalo Makonda ameonyesha ubingwa kulitekeleza hata kama ni kwa kuwasaliti au kuwachongea wenzake. Kimsingi, hapa kuna usanii ambao mwisho wake unaweza kuwaumbua wote ukiachia mbali wawili hawa kugeuka maadui hasa kila mmoja atakapoujua malengo ya na ukweli wa mwenziwe. Hakuna urafiki wenye kuvunja kila kanuni unaoweza kudumu milele. Wawili wakiudumisha, waliowazunguka watauvunja. Jikumbushe urafiki wa imla wa zamani wa Libya Muamar Gaddafi na Abdullah Senussi mkuu wake wa usalama ambaye wengi walimwita blackbox ya Gaddafi kama angekuwa ndege. Pale Kenya, Nicholas Biwott alimponza Daniel arap Moi. Je uhusiano na kulindana kwao viliishia wapi? Nani hajui kuwa wapambe kama kanali Isaac Malyamungu walimpotosha Idi Amin hadi akavamia Tanzania na kupata cha mtema kuni? Wengi wanauliza. Makonda anapata wapi hiki kiburi cha kufanya atakavyo? Nadhani jibu ni rahisi. Kiburi kinapatikana ikulu.
Inashangaza kwa rais ambaye huwa mwepesi wa kutenda kuchukua muda mrefu kuongelea kashfa za mteule wake na mwana wa pekee. Rejea alivyobatilisha maagizo ya kuhama wamachinga na waoaji kutakiwa kuwa na vyeti vya kuzaliwa. Je kwanini kwa Makonda amepata kigugumizi? Kuna tusiyoyajua yanayowaunganisha wawili hawa? Hata hivyo, urafiki na kazi za umma vinapaswa kuwekwa kando. Tokana na kumkingia Makonda kwenye makosa makubwa kama haya, inaanza kujengeka dhana kuwa Magufuli ndiye anayemtuma Makonda kuyatenda anayotenda. Bila hivyo, haiwezekani akawatukana wabunge sasa anaambiwa achape kazi. Hata hivyo, Makonda ametusaidia kuona na kujua sura ya pili nay a kweli ya Magufuli ambaye kwa msimamo wake anahubiri maji na kunywa mvinyo. Sakata hili limeibua picha nyingine kuwa katika utawala wa Magufuli kuna sacred sheep; yaani wasioguswa hata watende machafu kiasi gani.
Bila kujali urafiki wao au madaraka yao, watanzania wenye kuheshimu demokrasia na katiba walaani kitendo hiki cha hovyo na kiovu. Lazima tufanye hivyo tukizingatia kuwa rais si Mungu asiyekosea. Hapa amechemsha kweli kweli. Madaraka waliyo nayo ni ya wananchi na si yao wala marafiki au wapendwa wao. Je Makonda hata Magufuli ni zaidi ya Tanzania? Sijui mkanganyiko na udhaifu huu vinajenga picha gani kwa taifa? Je tumechoka amani hadi tunafikia kupinda haki ili kuokoana na kulindana? Inahitajika busara na tafakari vya kina.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: