Sunday, 19 March 2017

Keinerugaba usisamehe fisadi wa elimu

Image result for photos of makongoro mahanga
                Hivi karibuni, sakata la kughushi limetawala kwenye vyombo vya habari nchini hasa baada ya kuibuka madai kuwa mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda, alitumia vyeti visivyo vyake kujipatia elimu ya juu; ukiachia mbali kutumia majina bandia. Mbali na hiyo, kesi iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya mwanaharakati wa haki za binadamu Msemakweli Keinerugaba kwa madai ya kumchafua Makongoro Mahanga Mahanga aliyekuwa mbunge wa Ukonga na waziri wa zamani katika serikali ya awamu ya nne ambayo iliamu kunyamazia kashfa hii iliyowahusisha vigogo wengi wakiwamo mawaziri imekoleza moto uliokuwa umeanza kuzimika. Hii ni changamoto kwa serikali ya awamu ya tano ambayo rais wake Dk John Magufuli alisema hana simile na walioghushi na wafanyakazi hewa watokanao na kadhia hii.
Kimsingi, Keinerugaba aliposema ukweli kwa kuandika kwenye kijitabu chake cha Orodha ya Mafisadi wa Elimu Tanzania alijua alichokuwa akifanya ukiachia mbali kuwa kashfa ya kughushi ni tatizo linalofahamika kitaifa japo halishughulikiwi. Keinerugaba alipodai kuwa Mahanga hakuwa na shahada ya Uzamivu Doctor of Philosophy (PhD), alionekana mzushi na kituko hadi kutishiwa kushitakiwa kama asingeomba msamaha na kufuta madai yake. Kwa vile Keinerugaba alikuwa na ana ushahidi wa alichoandika, alikataa kuomba msamaha huku akiwahimiza watuhumiwa waende mahakamani. Muda ukapita bila Mahanga kuchukua hatua zozote za kisheria kama alivyokuwa ametishia. Baada ya kuzongwa akaamua kujitoa kimasomaso na kufungua kesi ambayo ilitupiliwa na Mahakama hivi karibu; na hivyo, kuamuru Mahanga amlipe Keinerugaba gharama za kesi zipatasho shilingi milioni 11 na ushei. Mwaka 2009, Mahanga alifungua kesi ya madai namba 145/2009 dhidi ya Msemakweli ambayo ilifutwa Julai mosi, mwaka 2014 na Jaji Salvatory Bongole baada Mahanga na Wakili wake kukwepa kuhudhuria kesi mara nyingi tu.
            Baada ya maji kuzidi unga na ushahidi kuonyesha kuwa kweli Mahanga hana hiyo PhD hivyo si daktari wa falsafa, eti anamwangukia Keinerugaba!  Ili iweje? Viko wapi vitisho na majigambo wakati mhusika ni kihiyo wa kawaida tu?  Je wako Mahanga wangapi ambao serikali–kwa sababu ijuazo yenyewe–imeshindwa kuwachukulia hatua huku ikiwaandama wadogo? Kama Mahanga alikuwa akijua alikuwa anakana ukweli, kwanini aliruhusu alimtisha, kumpotezea muda na fedha Keinerugaba wakati akijua ukweli? Anajua Keinerugaba aliathirika kiasi gani kwa vitisho vyake, ukiachia mbali muda wote alipokuwa mshitakiwa? Kwani alimshirikisha au kumomba ushauri Keinerugaba alipoamua kufungua kesi husika? Ana bahati Keinerugaba hajamfungulia kesi nilizogusia hapo juu. Isitoshe, kama Mahanga angempata Keinerugaba, sidhani kama angemsamehe zaidi ya kumtumia kujifisia kuwa ana elimu ya kutosha wakati hana hata chembe.
            Keinerugaba amfungulie Mahanga kesi nyingine ya udanganyifu, kujipatia fedha bila stahiki, kujitambulisha kwa utambulisho usio wake, kujipachika sifa asizokuwa nazo. Kulidanganya na uliibia taifa, kughushi huku akiwaunganisha na wengine aliowataja wakiwamo akina Deodorus Kamala, Emannuel Nchimbi, Mary Nagu, David Matayo David, Raphael Chegeni na Victor Mwambalaswa ambao walidai wana PhD wakati hawana ukiachia mbali wengine kama William Lukuvi Hii itasaidia kutoa onyo kwa vihiyo wengi waliotamalaki nchini wakati waliogopa umande.
Pia Msemakweli aitake mahakama itamke kuwa serikali ina wajibu wa kupambana na kadhia hii na yule atakeyeshirikiana au kuwalinda waliogushi naye aunganishwe kwenye jinai hii bila kujali ukubwa wa cheo chake au taaisi yake hata kama ni serikali yenyewe. Pia mahakama iitake serikali kutangaza wazi wazi kuwa wanaojipachika vyeo vyovyote wanatenda kosa la jinai. Imefikia mahali udaktari unadhalilishwa kiasi cha wanganga wa kienyeji na matapeli wengine wa kiroho kujiita madaktari au maprofesa wakati hawajui hata maana na thamani ya udaktari wa falsafa.
Kama mahakama itatoa hukumu dhidi ya kadhia hii, naamini ukimya na kutowajibika kwa serikali dhidi ya kadhia hii vitakuwa historia. Haiwezekani mtu atuhumiwe kughushi aendelee kuwa kwenye ofisi ya umma wakati kitendo alichofanya ni jinai ya wazi. Hapa sijui wahusika wanaolindana wanamdanganya nani zaidi ya kupingana na ahadi zao za kufufua elimu na kupambana na jinai hii inayoanza kuota sugu nchini kiasi cha kuwakatisha tamaa watanzania wanaojituma kuisaka elimu kihalali.
Kwa vile imeshathibitika kuwa Mahanga hana elimu aliyodai kuwa nayo, basi alipe fidia huku akingoja kushitakiwa kwa makosa mengine yaendanayo na jinai aliyotenda. Pia tutumie fursa hii kuiasa serikali iache kulinda wahalifu hata kama wana madaraka makubwa au wako karibu na wakubwa wa serikali. Tuwataje, tuwashitaki na kuwaumbua ili umma uwajue na kuwadharau ukiachia mbali kuwaadhibu vihiyo ambao ni maadui wa elimu Tanzania.
Tumalizie kwa kumpongeza Keinerugaba kwa mchango wake adhimu na muhimu katika mapambano ya kurejesha thamani ya elimu nchini. Pia tumsisitizie kuwa hana haja ya kusamehe mtu aliyechipachika cheo asichostahiki huku akimpotezea muda na fedha mahakamani. Nadhani hili licha ya kuwa somo kwa wengine, ni cheche ya kuanza kuwasaka na kuwawajibisha matapeli na vihiyo wote wanaotumia sifa wasizokuwa nazo kihalali. Tutumie fursa hii, pia, kumpa changamoto rais Magufuli awatumbue watuhumiwa bila simile wala kupepesa macho. Kwani wanakwamisha na kulihujumu taifa letu ukiachia mbali kusababisha aibu kwa kujenga dhana ya kutoaminika kwa wasomi wetu wa kweli.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: