Wednesday, 22 March 2017

Kwanini Magufuli anawadhalilisha mawaziri wake

Image result for photos of magufuli mwakyembe, mhagama and simbachawene
            Hakuna ubishi. Rais John Magufuli ana sifa nyingi za uchapakazi japo ameanza kuonyesha sifa nyingine zinazokinzana na uongozi bora. Hivi karibuni alijiongezea sifa ya kutaka kujua na kufanya kila kitu kiasi cha kuwafanya mawaziri wake waonekane kama viranja mbele ya mkuu wa shule ukiachia mbali wengine kuabishwa. Mfano, hivi karibuni, waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe, alitoa amri kuwa kila atakayetaka kufunga ndoa, lazima awe na cheti cha kuzaliwa. Baada ya amri hiyo, rais John Magufuli alitoa amri ya kupingana na Mwakyembe kwa kusema “kwa hiyo, ndugu zangu Watanzania, msiwe na wasiwasi wowote. Endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti za kuzaliwa ndipo aoe au kuolewa, nitamuelekeza waziri Mwakyembe apeleke bungeni kikarekebishwe.”  Japo hoja ya rais ina mashiko, hii inatafsiriwa kuwa serikali ya Magufuli haina mfumo mzuri wa mawasiliano.  Kwanini rais hakuwasiliana na Mwakyembe kupitia taratibu za ndani ndipo akampa nafasi ya kurekebisha kifungu husika hata kukitengua? Je rais anafanya hivi kutokana na kutojua sheria au ubabe tu? Je rais haoni kama anawapa mishale wapinzani wake kuanza kumpa majina mabaya kama vile dikteta uchwara?
            Mfano, ukiangalia umri wa wanaoa kwa sasa, uwezekano wa kuwapatia vyeti ni mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa wengi wamezaliwa kwenye hospitali au zahanati. Kwa amri hii, rais amesaidia wageni kujipenyeza na kuja kuishi nchini tena wengi wakitumia visingizio vya kuoa wasichana wa kitanzania ili waendelee kuishi nchini ukiachia mbali kutoa upenyo wa watu kuoa watoto kwa kisingizio cha kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa. Serikali, kwa muda mrefu, imefanya uzembe kuwaacha watanzania wajiishie kama wanyama huku wageni wakiingia na kujazana nchini hadi wengine kufikia kupata uongozi wa juu bila stahiki. Wengine wanatumia mfumo huu uchwara na kujipata afya na elimu bure wakati si raia.
            Ajabu, kila unapofika msimu wa kampeni wanasiasa wanawaaminisha watanzania kuwawatawapeleka kwenye karne ya 21. Yaani hadi karne hii serikali haina uwezo wa kutoa hata vyeti ya kuzaliwa kwa raia wake. Hii maana yake ni kwamba Tanzania ni kama pori ambako mnyama yeyote toka mahali popote anaweza kuingia na kutoka bila kujulikana. Wenzenu nchi zilizoendelea humwandishi mtoto shule wala kufanya lolote bila cheti cha kuzaliwa. Ili kuondoa watu kuishi bila kujulikana, kila anapozaliwa mtoto, awe raia au mkazi hupewa cheti cha kuzaliwa haraka ili kuweza kutambulika na kujua idadi ya watu ambao serikali huwahudumia.
            Kuna haja ya kuibana serikali iache uzembe kama alivyokiri rais aliyekaririwa akisema “hadi sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.” Je nini maana ya kuwa huru iwapo watu hawawezi kuwa na haki ya kuwa na cheti cha kuzaliwa? Msisingizie hali ya wengi wa watu wetu kuishi vijijini. Inakuwaje waweze kupata simu na noti washindwe kupata hati muhimu kama cheti cha kuzaliwa?  Kama serikali ingekuwa makini na nia, watanzania wote wanaweza kupata vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya uraia. Bila kufanya hivyo, ni kwamba unaruhusu wageni wafurike nchini mwako na kutishia usalama wako ukiachia mbali kutumia raslimali zako bila stahiki.
            Kimsingi, rais licha ya kuingilia mamlaka ya waziri, amemdhalilisha kwa kutengua amri yake na kupingana naye tena hadharani bila kujali kuwa naye ana mamlaka yake kisheria. Kwa wenzetu, alichofanya rais kingewasukuma baadhi ya wananchi kwenda mahakamani kupinga amri yake isiyo ya kisheria.  Hapa uko wapi utawala bora na wa sheria kama waziri hana mamlaka wala hajui mipaka ya mamlaka yake? Wapinzani wakilalamika na kuhoji mawaziri kufanya kazi bila vitendea kazi wanakamatwa na kuonekana wachochezi. Basi tutangaze kuwa Tanzania ni nchi ima isiyo ya kidemokrasia au ya kifalme.
            Magufuli amekuwa akiingilia maamuzi ya wasaidizi wake bila kufuata sheria wala kuwapa staha kwa watendaji wake. Rejea kufuta agizo la kuondoa machinga mijini lililokuwa limetolewa na waziri wa  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) George Simbachawene ukiachia mbali mawaziri wengine Nape Nnauye (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), na Jonista Mhagama waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu). Rejea mazoea ya kutoa maamuzi hadharani na si ofisini. Imefikia mahali sasa mawaziri wanafanya kazi kwa hofu kama viranja wa shule mbele ya mwalimu mkuu. Wamegeuka sawa na watumishi wa mfalme ambao hawana ubavu wa kumpinga au kumlazimisha aheshimu maamuzi na madaraka yao. Rejea kuendelea kumkingia kifua mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda licha ya kuchafuka kwa shutuma za kughushi vyeti. Rejea kumteua mtuhumiwa wa kashfa ya Escrow waziri Sospeter Muhongo bila kutoa hata maelezo ya kufanya hivyo kama ishara kuonyesha alivyo mbabe na asiyewajibika hata kwa wale waliomchagua.
            Tumalizie kwa kuwataka mawaziri wenye udhu kujiuzulu au kwenda mahamakani pale mamlaka yao yanapoingiliwa.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

3 comments:

Anonymous said...

Yaani ulichoongea ni ukweli mtupu. Kwa sasa Tanzamia inaobgozwa na mwalimu mkuu na mwalimu wa kawaida mmoja Bashite viranja tu.

Tazama hili la Clouds analichukulia poa. Kwani alilijua ndo maana wiki zilopita alisema Napenda Shilawadu.Inaonesha kabiså alijua mwalimu mwenzake atakuwepo.
Watanzania tukiungana. Hatutotawaliwa kibabe.
Amani ndo nguvu yetu

Anonymous said...

Nimerudia namaumivu. Tanzania inaenda ktk udiktea. Sauti ya mtu haisisiki leo hii.Katika utawala ulosikiaga na Magufuli na Bashite Marinda.
Nape Nape utaenda Lea kuwa mfanö wa walioana haki sio kutaka sifa. Macho yangu yanaona jinsi damu itavyomwagwa na huyo MagufulI na Bashite.
Anataka kuwatawala watu kama anavyomtawala Mkewe

NN Mhango said...

Anon.
Tanzania siyo inaenda kwenye udikteta. Iko kule tayari. Ni aibu na pigo kwa watanzania kama watajirahisi na kukubali hiki ambacho Tundu Lissu huita udikteta uchwara.