Tuesday, 7 March 2017

Kijiwe chastukia matapeli wa maombi

                    Baada ya kuudhiwa na makanjanja na wachunaji wanaowekeza kwenye kuombea kaya yetu wakati wakiibia, Mgoshi Machungi ameamua kuwatolea uvivu kwa kuleta mada kijiweni.
            Baada ya kuamkua anatoa la moyoni “wagoshi, hivi huwa mnajishikiaje mnaposikia makee ya kutaka eti kuombea kaya ambayo siku hizi yamegeuka kuwa fesheni?”
            Mpemba anajibu “yakhe hata mie hawa matapeli wa kiroho waliojaa uroho waniudhi kweli kweli. Wao wahitajiombea lakini bado wadai wataka kuombea kaya. Kwani kaya yetu ni kaya ya wafu?”
            Kabla ya kuendelea Mijjinga anamchomekea kwa kuhoji “hivi wachunaji na maaskopo wa kujipachika si wafu kiroho? Hivi viongozi wa kiroho waroho ambao dini yao ni ukwasi si wafu kiroho? Hebu tujaribu kufikiri kabla ya kufanya jambo.”
Kapende anaongeza “sijui kama mchungaji msimbe yaani asiye na mume aliyetangaza hivi karibuni kuwa ataombea ndoa kama anaweza kumuombea mwenzake apate mume wakati yeye ameshindwa kupata wake. Sijui kama tapeli aliyejivika joho na utukufu ana udhu wa kumwombea mwenzake akafanikiwa wakati yeye anahitaji maombi hayohayo. Mie sijui.”
            Msomi Mkatatamaa anakula mic “msemayo ni kweli. Kwani hivi karibuni, kaya yetu imegeuzwa mfu kiroho kiasi cha kuhitaji kuombewa. Kweli twaweza kuendesha kaya kwa kutegemea maombi badala ya kuchapa kazi? Tunamdanganya nani kwa kujidanganya wenyewe kama jamii? Je ni kweli kuwa kila asemaye anataka kuombea kaya tumkubali wakati wengine ni wenye dhambi kuliko hata huyo shetani mwenyewe? Kwanini kutangaza wakati mtu anaweza kwenye faragha yake akaliombea taifa hata wale wote anaowataka? Tumegeuka jamii ya matangazo uchwara na imani za kishirikina kirahisi hivi!”
Kabla ya kuendelea mzee Maneno anakula mic “Msomi umetoa madai mazito. Je una aya au ushahidi?”
Bila kungoja aendelee Msomi anajibu “kama una biblia fungua Matayo 6:6.
Msomi anafungua mkoba wake na kutoa biblia na kusema “ Biblia  inasema kuwa “bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha funga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.” Hawa wanaotangaza mikesha na matamasha ya kuomba wanapata wapi?” 
Mzee Maneno anaomba apewe biblia. Anasoma hiyo aya na kusema “hapa mzee umenipata. Sina ubishi.”
Msomi anajibu “hata ukitaka Kuruani wewe sema.” Anafungua mkoba na kutoa Quran na kumpa mzee Maneno na kuendelea “japo maombi ni kitu kinachoonekana kuwa kizuri, kina namna yake. Si kila anayeomba hukubaliwa. Na isitoshe, kila aliye hai apaswa kujiombea. Tusipende kuombewa kana kwamba tu maiti. Anayeombewa mara nyingi ni maiti au asiyeweza kujiombea.”
Mipawa anakwanyua mic, “nakuunga mkono Msomi. Hivi kama kila mtu anahitaji maombi, anapata wapi nguvu na mamlaka ya kumuombea mwenzake wakati naye anahitaji hayo maombi? Wapo watu wengi wamewekeza kwenye kuombewa. Wakati mwingine hudiriki hata kudanganywa na wale wanaopaswa kuombewa kutokana na kuwa marehemu kiroho kuwaombea. Inakuwaje tuhitaji maombi kwa wafu wa kiroho wanaohitaji kuombewa?”
Sofia Lion aka Kanungaembe anabusu mic “ni kweli. Hata kama maombi ni muhimu, sidhani kila anayetaka kuomba ana sifa za kufanya hivyo. Kwanza, kaya yetu haina dini. Hivyo, kila mtu anayetaka kuiombea, hana haja ya kutupigia mikelele. Aende aombe hata uchi; hazuiliwi. Hili la kutangaza mikesha ya maombi nadhani ni gea ya kutaka kuwa karibu na ulaji kama siyo kutafuta umaarufu wa dezo na rahisi.”
Kanji anampa tafu mshirika wake Sofi “mimi pende veve naweka hii kitu.” Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchokoza “Kanji acha matusi na mafumbo. Umependa kitu gani aliyoweka na ameiweka wapi kama huna lako?”
Mheshimiwa Bwege anaamua kuokoa jahazi baada ya kuona utani unaanza kunyemelea mada “jamani tuache utani. Kaya yetu inatapeliwa na kila tapeli. Hamkusikia yule tapeli wa kigabacholi aliyechomoa njuluku kibao akiahidi kujenga mradi wa maji wa N’gapa hadi dokta Kanywaji akaingilia? Hii ndiyo kaya ya wajinga wanaoweza kudanganywa na kila tapeli kuanzia miradi ya maendeleo hadi maombi. Sijui huyu naye watamuombea amalize mradi kwa shinikizo la mkuu? Madudu kama haya hayahitaji maombi bali kutumia just common sense. Kesho sitashangaa kusikia wakijitokeza watu kuombea kaya iwe tajiri wakati tunaibiwa na wachukuaji wanaoitwa wawekezaji ukiachia majambazi kama EPA, Escrow, UDa, Ng'apa, SUKITA na mengine mengi yaliyojaa kwenye makaburi aliyoogopa kuyafukua bwana mkubwa ili yasimshinde kuyafukia. Je naye anahitaji kuombea apate ujasiri wa kulinda raslimali zetu?”
Kabla ya kuendelea Kanji anarejea “mimi iko ombea kuu ipate jasiri ya kuteua bibi kuba yangu kama anateuva Salima Kwete kuwa ishiwa.”
Kabla ya kuendelea Mgoshi anarejea “waahi kaka usintie vidoe machoni. Sitaki kusikia hii kitu. Kwani inafanya nikumbuke enzi za mfaume Kimwei wa kue Vuga aivokuwa akiteua vimada wake na wa maafiki zake kuwa washaui wa mfalme.”
“Yakhe mie sikujua kumbe ufalme na usultani vyaanza kurejea kwa nlango wanyuma!”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la mchunaji Gwajimmy akienda kumwombea David Bashite Poo! Acha tumwendee kumuuliza nani anamwambea au kumuumbua yeye!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: