Wednesday, 22 March 2017

Kijiwe champongeza Keinerugaba


            Leo Msomi Mkatatamaa ameingia kijiweni akiwa mwenye furaha japo si kawaida yake kuonyesha hisia zake. Anaamkua na kumpa gazeti Mchunguliaji na kusema “mmesikia yaliyomkuta daktari feki Makorongo Muhanga?”
            Kabla ya kuendelea mzee Maneno anauliza “huyo muhanga kama mnyana ana nini nasi na inawezekanaje mnyama akaitwa daktari?
            Msomi anajibu “kaka huyu si mnyama. Na kama ni mnyama basi ni mnyama wa kughushi. Mara hii mmesahau muishiwa wa Ukonga aliyejipachika udaktari wa falsafa na mwanaharakati Msematruth Keinerugaba akamuumbua yeye na wenzake alipofyatua kombola aliloliita mafisi na mafwisadi wa ilmu nchini?”
            Kapende anachomekea “Msomi nimekupata. Nilisoma kesi ya huyu jamaa aliyofungua kupinga kuumbuliwa akidai alidhalilishwa na kuvunjiwa heshima wakati ni kihiyo wa kawaida.”
            Mijjinga anampoka Kapende mic na kuronga “hata nami niliipata kuwa pilato alitupilia mbali kesi hii baada ya mlalamikaji na wakili wake kuufyata na kushindwa kuhudhuria kesi, hivyo, kumlazimisha pilato kuifutilia mbali akimbandika mzigo wa kulipa gharama zote za kesi ambazo naambia ni milioni kumi na moja na ushei.”
            Mipawa anakatua mic “hii kitu naijua sana; na ilikuwa ikinisumbua hasa zama hizi za akina Daudi Bashite ambaye anaonekana kukingiwa kifua na dokta Kanywaji asijue anajipinga, kujiuumbua na kuonyesha asivyotenda haki kwa wachovu wote.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe ambaye amevuliwa uanachama hivi karibuni anatwaa mic “huyu jamaa na genge lake wametuonea sisi. Ngoja Mungu awaumbue. Nangoja kusikia hatua atakazomchukulia huyu dogo kiherehere Bashite. Bila shaka hapa tutajua mbichi na mbivu. Halo haloooo! Ama kweli Mungu si Mpayukaji.” Ananitazama huku akitabasamu. Mie siongezi kitu zaidi ya kutabasamu.
            Mgoshi Machungi anakula mic “tiisema kuwa wapo wasomi wengi vihiyo tikachekwa. Sasa yako wapi? Niisoma kwenye gazeti la Danganyika Daima jana kuwa Makongoo Muhanga amebanwa kuipa uchache ambao hana. Aitaka eti awe anaipa laki tano kwa mwezi akini Keineugaba aikomaa na kutaka asweke upango hadi atapike njuuku.”
            Mpemba anakatua mic “wallahi mie nshangaa hawa vihiiyo. Kama wajua huna hiyo shahada wadai unayo ili uonekane nsomi wakati maamuma ili iweje? Mie nasema lazima huyu jamaa alipe hiyo njuluku. Pia nanshauri Keinerugaba awashitaki wale wote alowataja ili wapewe adhabu kama wengine. Hili la Bashite, kama hatoshughulikiwa, wallahi mie ntaandamana hata kama watanipiga mabomu na wapige.”
            Kanji anamchomekea Mpemba “sasa veve Pemba iko tafuta sida. Kama kuba naamua kula pini veve tafanya nini lazimisha yeye atimue hii Shite?”
            Kabla ya Mpemba kuendelea, Mheshimiwa Bwege anakwanyua mic na kuronga “mie sitegemei chochote cha maana kitendeke. Ukiona bingwa wa kutumbua amenyewe jua naye ameambukizwa hayo majibu aliyosifika kutumbua. Nyie mmeshikilia Bashite pekee wakati wapo wengi. Hamjui kuwa na Bill Lukuuuvi naye anatuhumiwa kuwa kihiyo anayedai ana masters wakati ni mweupe; na hata ndege wanajua kuwa ni kihiyo aliyeghushi?”
            Msomi anarejea “nadhani kuna haja ya kuepuka woga. Tuwakabili hawa jamaa watumbuane vinginevyo kwenye uchakachuaji ujao tuamke na kuwaambia wachovu madhambi ya hawa jamaa wanaolindana huku wakilipana njuluku zetu ukiachia mbali kupeana vyeo vinono wakati sisi wenye elimu za kweli tukidoda vijiweni. Huo ukubwa wa nkoa anipe mimi uone nitakavyoleta mapinduzi.”
            Mgoshi anarejea “kwanini jamaa hataki kuwa mkwei kwa nafsi yake? Mbona mgoshi Makambae aiweza kupata vyeo vya juu pamoja na kutosoma. Si aisema ukwei na akaeeweka? Huyu Bashite namshaui aonyeshe vyeti vyake yaishe; na aendeee kuchapa mzigo.”
            Kanji anarejea na kukatua mic “mimi iko jua hii Shite iko Hiyo. Kwanini naita vatu kuwa nauza bimbi bila shahidi ya kutosha? Hapana jua kuwa kama naita mtu bila shahidi navunjia yeye heshima yake? Kweli hii iko Hiyo kweli kweli.”
            Mijjinga anamchomekea Kanji “nakubaliana na wale wanaosema kuwa hakuna la maana litakalofanyika. Hebu fikiria. Dokta Kanywaji alizuia waishiwa na mawaziri kusafiri ughaibuni lakini hapo hapo akampa ofa Bashite na bi nkubwa wake waende kutanua kwa Joji Kichaka, Ufaransa na Dubai kabla ya juzi juzi kwenda Bondeni kuweka mambo sawa. Tunamdanganya nani na kwanini? Ama kweli ukisikia Danganyika basi si nyingine bali hii. Ni aibu kwa wanene kufumbia macho uoza huku wakituhadaa kwa kuhangaika na dagaa.”
            Msomi anarejea “umenikumbusha sakata ambalo halijapoa. Je mnajua kuwa Richomonduli imefufuka upya? Juzi nilisoma kwenye jarida moja la kimataifa kuwa Symbiosis bin Richmonduli imeishataki kaya na kupewa haki ya kulipwa madafu trilioni moja kwa kukatiza mkataba wa akina Kagoda. Hii maana yake ni kwamba akina Kagoda, sawa na IpTL wanaendelea kutuimbia wakati nasi tukishuhudia bila kufanya lolote.”
            Mipawa anakatua mic “Msomi sasa huu uchokozi. Hivi hamjui kuwa dingi alisema kuwa hawezi kufukua makaburi ili asishindwe kuyafukia. Hujui kuwa symbiosis, Kagoda, IptL na madude mengine yalianzishwa na wanene waliostaafu ambao wamefanikiwa kumtisha Dokta Kanywaji asiwatumbue?”
            Kijiwe kikiwa ndiyo kinakolea si alipita Makorongo Muhanga huku akilialia. Acha tumtoe mkuku ili kumfanyia kitu mbaya aache kughushi na kujiita daktari wakati ni hamnazo!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: