The Chant of Savant

Friday 16 November 2007

Wananchi pingeni Kamati ya kurekebisha Mikataba.

*Kabwe na wapinzani wamepewa kitanzi wajinyonge.
*Wananchi wameletewa kiini macho kingine.
*Kikwete hana udhu wa kuunda kamati ni mshiriki.

Nimesoma maoni ya watu mbali mbali waliohojiwa baada ya Rais Jakaya Kikwete kuteua kinachoitwa Kamati ya kuchunguza mikataba ya madini. Wengi licha ya kumuunga mkono, walionyesha kufurahishwa na hatua hii. Huenda hii ni kutokana na kuchoshwa na unyang'au na hasara vilivyosababishwa na neema hii inayoonekana kuwa balaa zaidi.
Kwa mtu ambaye amekuwa akifuatilia ahadi za Rais tangu aingie madarakani, atakubaliana nami kuwa aliwahi kuwahakikishia Wananchi kuwa:

Mosi serikali yake isingeingia mikataba mipya kabla ya kurekebishwa ya zamani. Ajabu na sikitiko ni kwamba ndani ya miezi miwili ya kutoa hakikisho hili, iligundulika kuwa mkataba mpya na balaa maarufu kama Buzwagi ulisainiwa kwenye nyumba ya kulala wageni huko London Uingereza.
Wengi wameeleza kuwa kusainiwa kwa mkataba huu nje si tatizo bali:
a) Kusainiwa nyumba ya wageni badala ya ubalozi.
b) Kufanywa siri ilhali anayesaini-serikali- hufanya hivyo kwa niaba ya wananchi ambao kimsingi walipaswa kutaarifiwa kilichomo.
c)Kusainiwa mkataba kwa masharti ya zamani ya kinyonyaji ambayo ndiyo hasa sababu ya kutakiwa kuwapo marekebisho ya mikataba yote.
d)Serikali kuonyesha wazi kujua kilichoko nyuma ya mkataba huu kuwa ni ufisadi wa watu wachache ambapo taarifa za hivi karibuni zilimkariri mwandishi wa waziri mkuu akimtetea Waziri Mkuu, Edward Lowassa, baada ya Gazeti moja kudai alikuwapo kwenye kutia saini mkataba huu na ndiyo maana ukasainiwa nje ya ubalozi ili kulinda usiri huu.

Pili, Rais alinakiriwa hivi karibuni wakati wa sakata la mkataba huu kufumka kiasi cha kusababisha Mbunge kusimamishwa, kuwa mikataba ilikuwa inakaribia kuisha kurekebishwa. Bahati mbaya hakutangaza kamati ya kufanya hivyo kama alivyofanya kwenye kamati hii tata japo inaonekana kushabikiwa.

Je Rais aliudanganya umma na kwanini? Je Rais anapodanganya anakuwa bado na uhalali wa kuendelea kuwa madarakani kwa kujenga taaswira ya mtu muongo na asiyemainika?
Kitu kingine ambacho kimsingi kinafanya nioneka kama anachofanya Rais ama ni kupitisha muda, kutapatapa, kurejea uongo au hata kutaka kuwaingiza wengine kwenye uchafu uliotamalaki kwenye serikali yake, ni ile tabia ya Kikwete kuwa na sura nyingi. Mfano Rais amekuwa hatekelezi ahadi alizojiwekea mwenyewe na ambazo ndizo zilizowashawishi wananchi kumchagua.
Je kwa kuunda Kamati ndilo jibu? Je Kamati itafanya kazi yake vizuri na kutoka na suluhu ilhali watuhumiwa waliosababisha iwepo haja ya kurekebisha Mikataba bado wako maofisini wakiharibu na kuficha ushahidi?

Wananchi wamezugwa na kuteuliwa kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zuberi Kabwe ambaye naye ameonekana kushabikia na kuuingia mtego huu! Je Kabwe peke yake atafua dafu miongoni mwa Makada wa CCM? Je Kabwe ana utaalamu gani wa Mikataba hata Madini? Je huku siyo kutaka kumnyamazisha kwa kumpa ulaji? Je kama yeye ndiye alikuwa mlalamikaji katika sakata zima hadi kusimamishwa kuhudhuria vikao, inaingia akilini mlalamikaji awe kwenye jopo la Majaji au wachunguzi? Ushahidi muhimu ambao amekuwa anadai anao atautoa kwenye jukwaa lipi? Kwanini Rais ambaye naye licha ya kutuhumiwa kufaidika na ufisadi uliosababisha kusainiwa Mikataba feki-akijizungushia Marafiki zake anaowakingia kifua-anafaa vipi kuunda Kamati asiwe na ushawishi? Je ni vigezo gani ametumia kuunda Kamati hii? Kwanini Kamati isiundwe na Bunge au hata kutokana na makubaliano ya Vyama vya siasa, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Wanataaluma, Watu binafsi na wananchi kwa ujumla? Je hapa haki kweli itapatikana?
Maswali ni mengi kuliko majibu.

Kwa mtu anayejua usiri, ujanja ujanja, ulaghai na kulindana, Kamati hii haitakuja na jipya zaidi ya kuja na kiini macho kama cha Takuru cha kuwasafisha Mafisadi walioko nyuma ya uchafu wa Richmond ambao sasa umezuka upya.

Kwa mfano wakati gazeti la Mwanahalisi lilipokuja na tuhuma kuwa Waziri Mkuu alikuwapo wakati wa kusainiwa Mkataba wa Buzwagi naye akakanusha, ungefanyika uchunguzi haraka kubaini ukweli ni upi? Na kwanini karibu kila kashfa Waziri Mkuu anahusishwa hata kama anakana na bado anaendelea kukaa madarakani tena bila kuchunguzwa?

Suala la Waziri Mkuu linaingizwa humu kutokana na kuhusishwa na Mikataba ya Richmond na Buzwagi. Na huyu ndiye mshauri na msaidizi wa Rais anayesimamia utendaji wa kila siku wa serikali. Je kwa mtu kama huyu kuachiwa bila kuchunguzwa au hata kutimuliwa siyo kufanya viini macho?
Kama Kamati inataka kuwasaidia Watanzania kutafuta suruhu yafuatayo yafanyike.
a)Vitolewe vigezo vya kuunda Kamati hii ambayo inapaswa kuwa huru na isiundwe na Rais. Rejea kilichotokea kwa tume za Jaji Joseph Warioba na Robert Kisanga zilipokuja na mapendekezo na findings zilizomkera Rais.
b) Waliosababisha kusainiwa Mikataba hii na wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine waondolewe ofisini ili kuchunguzwa vizuri. Mfano Mawaziri kama Andrew Chenge, Nazir Karamagi, Ibrahim Msabaha, Edward Lowassa, Basil Mramba,Juma Ngasongwa na wale wote walikuwa kwenye Cabinet ya Mkapa walioko kwenye ya sasa wafukuzwe ili haki itendeke.
c)Zitolewe hadidu za rejea za kamati husika, mipaka yake, nguvu zake kisheria na vitu kama hivi.
c)Iundwe na wataalamu wa Madini na sheria badala ya Wanasiasa ambao ni hao hao walifanya uzembe au kuendekeza tamaa zao hadi nchi ikaingia kwenye zahama. Hawa tunaowashabikia kuwa wana Kamati ni wale wale wanaoshinda na kukesha Dodoma kwenye vikao vya Bunge wakitaniana na kutumiana ujumbe mfupi wa simu. Namaanisha wanajuana na wanaweza kulindana.

Kwanini serikali hiyo hiyo inayotuhumiwa iwe ndiyo Mpelelezi, Hakimu, Shahidi na hata Askari wa Mahakama? Je Kikwete haoni anajipinga? Maana juzi juzi amekaririwa akiwatuhumu wapinzani kuwa vyote katika yote wakati naye ni yote katika yote. Au alikuwa ana-preempty alichokuwa anadhamiria kukifanya kwa kujijengea mazingira? Pia ifahamike kuwa wengi wa Wajumbe wa Kamati hii tunayoishabikia ni wale wale wanaokwamisha karibu kila Miswada yenye maslahi kwa umma wakisimamia upande wa serikali ya chama chao-Rejea ukaaji kama Kamati ya Chama kuhujumu miswaada muhimu. Je hawa wameokoka lini? Je hawa hawatakwenda kulinda chama na serikali yao ambavyo kimsingi ndiyo vijiko na mashamba ya ulaji wao? Kwa ufupi ni kwamba tunapeleka kesi ya tumbili kwa nyani au ya kasa kwa kobe hata mashitaka ya nundu ya ng'ombe kwa ngamia. Ni ujuha kiasi gani?

d) Kipengele kingine muhimu ni kuhusu mbunge Kabwe. Kama mikataba ina walakini ukiwamo na wa Buzwagi, je Kabwe na Wananchi anaowawakilisha hawakuonewa kwa adhabu aliyopewa na usumbufu uliojitokeza?

e) Je tume ina kinga na mamlaka yapi dhidi ya kuingiliwa na Rais au hata Mawaziri? Ina mamlaka yapi kumfikisha mtuhumiwa mbele yake na hakikisho lipi kuwa mapendekezo yake hayataishia yalipoishia ya tume tajwa hapo juu? Tunaleta siasa kwenye mambo ya kitaaluma!


Tukirejea kwenye ithibati ya Rais na serikali yake ambayo imeonekana kuwa na soft stand on corruption, je ilichofanya siyo kupora madaraka toka kwa wananchi ili kuweza kujisafisha haraka ili kurejesha imani ya wananchi? Hii ni sawa na kituko cha kumuondoa John Malecela kwenye umakamu kwa vile ni Mzee na kumteua mzee tena mwenye umri kama wake!
Kwanini kwanza Rais asibanwe akaeleza ni kwanini aliudanganya umma akijua wazi kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria? Kwanini tusiwaulize wananchi wanamhukumuje kwa jinai hii? Pia kwanini waziri mkuu asibanwe naye akaeleza ukweli ni upi badala ya kuridhika na kanusho ambalo kwa wanasiasa ni jambo la kawaida? Rejea Kikwete kuwashambulia wapinzani na kesho yake kusema alikaririwa vibaya.

Je tume hii ya Rais isiyo na meno wala uhalali inachunguza mikataba hii ili iweje? Hasara ambayo tumeishaingia inawekwa upande gani na nani atawashughulikia wahalifu waliotenda jinai hii iwapo kwa mfano rais alishasema wazi kuwa hana mpango wa kuwashughulikia. Rejea sakata zima la Mkapa mkewe, wanae na marafiki zake kwenye kujiingiza kwenye uhujumu wa taifa hadi kuibuka na makampuni kama ANBEN, Fosnik, Tanpower.

Nani anategemea tume iwe huru na stahiki iwapo Rais mwenyewe akiwa Waziri wa mambo ya nchi za nje alishiriki moja kwa moja kuidhinisha na kupigia chepuo mikataba hii? Rejea kusainiwa kwa mkataba wa ovyo wa IPTL chini ya wizara aliyokuwa akiisimamia rais mwenyewe-wakati ule. Tuuchukulie kama mfano mwongozo. Je utakapoletwa mezani kujadiliwa Mkataba wa IPTL unaojulikana kuwa na wino wa Kikwete mwenyewe, wateule aliowateua kwa sababu na masharti anayojua mwenyewe wataweza kumshughulikia ilhali ndiyo amewapa ulaji huu? Je hapa hayatarejea yale yale ya Remmy Ongala: zinaibiwa shilingi mia, inaundwa kamati ya kuchunguza na kula laki?

Kama tumeamua kurekebisha Mikataba hii ya jinai, yafuatayo yafanyike:
Mosi iundwe na watu huru wasiowajibika kwa serikali wala yeyote bali taifa.
Pili iundwe na Wataalamu na siyo wanasiasa.
Tatu waliohusika kwa njia yoyote kwanza watimuliwe wakingojea kuadhibiwa bila kujali vyeo vyao au ukaribu wao kwa Rais.
Nne, kamati ifanye shughuli zake wazi wazi kila mwananchi kushuhudia kinachoendelea. Ifanye kazi kama Mahakama zetu zinavyofanya kazi ili haki ionekane ikitendeka badala ya utaratibu uliozoelekea wa kujifungia kwenye Mahoteli ya kifahari na kugawana mishiko.
Ushauri: Kabwe angekataa kuwa mjumbe wa kamati kwa vile ni mdai na ana ushahidi muhimu unaopaswa kutolewa kwa kamati huru ukiwa na ulinzi wa kisheria. Kama atapuuzia ajue wazi kuwa ushahidi wake utachukuliwa na kuharibiwa na baadaye utamrudi mwenyewe kiasi cha kuharibu kazi yote pevu iliyokwishafanyika.
Kitu kingine kwa uadui na madhara aliyosababishia serikali na walioko nyuma ya jinai hii-ambao ni wazito na wana ushawishi- akae chonjo anaweza kuundiwa hata rushwa ili wammalize. Anything can happen. Asiwe kama panya kuuawa na uroho wa kula punje ya karanga.
Hitimisho, Kikwete wala serikali yake kwa viwango vyovyote vinavyoingia akilini hana udhu wala nia ya kuunda kamati ya kuchunguza uchafu wake na wenzake. Hii ni danganya toto na janja ya kuwamaliza akina Kabwe. Alichofanyiwa Kabwe na upinzani kwa ujumla ni sawa na mtu anayenuka harufu ya chooni kukukaribisha mkaongelee chooni. Utatoka na harufu mbaya ushindwe kumcheka wala kumbaini kuwa ananuka. Ingekuwa ni amri yangu, ningependekeza uitishwe uchaguzi mpya. Maana serikali imeshindwa vibaya sana. Haijulikani ni ya nani kati ya Wananchi na Mafisadi.
Mungu ibariki Tanzania.
nkwazigatsha@yahoo.com http://www.mpayukaji.bogspot.com/

No comments: