Thursday, 31 January 2008

CCM,kufilisika,kufa mafisadi na saa ya Ukombozi.

Kwanza nilicheka kwa huzuni; niliposoma habari kuwa CCM imepora hoja ya ufisadi wa BoT iliyoibuliwa na waandishi wa habari kwa kuipenyeza kwa kambi ya upinzani. Nilicheka na kuhuzuni sana kutokana na ukweli kuwa ni upuuzi, urushi na kutapatapa kwa CCM kutoa madai ya kitoto kama haya bila aibu.

Nilicheka zaidi niliposoma kuwa CCM inasema mafisadi wafilisiwe! Nilicheka kwa sababu tuendako CCM haiwezi kukwepa kuhusika na ufisadi uliotikisa taifa letu. Kwa mujibu wa taarifa zilizomkariri John Chiligati, Katibu wa Uenezi wa CCM, kamati kuu ya chama eti imetaka wote watakaobainika kuwa walipora pesa BoT wafilisiwe! Kwanza ifahamike kuwa CCM inajua kuwa watakaopatikana ni mbuzi wa shughuli na vidagaa wachache; watakaobeba msalaba wa vigogo wa CCM na serikali. Mbona vyombo vya habari vimeishafichua njama hii? Rejea lead story ya gazeti la Raia Mwema la Januari 31, kuwa, mashahidi watakaojitokeza mbele ya tume ya rais ya kuchunguza kadhia hii wasiwataje vigogo wa chama na serikali.

Hivi CCM inadhani watanzania wana mafyongo na upogo kiasi cha kutoona zengwe linalotembezwa? Nani hajui kuwa kashfa hii inashughulikiwa kinamna namna kwa kutafuta ku-buy time na kuwahadaa wananchi? Kwanini serikali ya CCM imeshindwa hata kuiomba rasmi Marekani kumrejesha nchini Ballali? Rejea taarifa ya balozi, Mark Green, wa Marekani kwa wanahabari siku chache kabla ya CCM kuja na usanii huu? Mbona rais anapata kigugumizi kuomba Ballali arejeshwe haraka? Badala yake, serikali imepata kisingizio kwa kupigia upatu ujio wa rais George Bush wa Marekani utadhani ni big deal!

Nina sababu mahsusi kwa hili.

Kwanza, CCM ndiyo inayounda serikali zote tangu uhuru. Ukiondoa serikali ya awamu ya kwanza na ya kidogo, awamu ya pili, serikali zilizobaki ni uoza mtupu. Je hapa CCM itakwepaje kuwajibika kwa uchafu wa serikali na watendaji wake? Anayebishia hili ajikumbushe kashfa zinazomkabili rais mstaafu, Benjamin Mkapa, mkewe, watoto wake na marafiki zake huku mwenyekiti wa CCM hii hii akimkingia kifua kuwa hawezi kuchunguzwa. Tulishasema kinga ya urais inatumiwa vibaya kulinda wezi. Tulishahoji kutochukuliwa hatua kwa Anna Mkapa, Nicholaus Mkapa na Daniel Yona ambao ni washiriki wakuu wa Mkapa. Je nao walikuwa marais nyuma ya pazia?

Pili, CCM -na serikali zake- ndiyo iliyoasisi na kuneemesha mfumo mfu wa watawala kujiibia watakavyo. Hapa napo CCM haiwezi kukwepa lawama na kuwajibika. Hebu rejea kuendelea kufichwa kwa kigogo wa serikali anayejulikana kuwa nyuma ya kashfa ya Richmond. Rejea kuendelea kulipwa pesa kwa kampuni kama IPTL, Richmond na nyingine nyingi hewa kama Deep Green.

Tatu, CCM kwa kutumia wingi wa wabunge wake bungeni ilidiriki hata kuzuia bunge kujadili ufisadi wa BoT hadi upinzani uliposimama kidete na kuiibua upya kupitia majukwaani. Kwanini CCM inasahau iliyosema jana? Mbona CCM na serikali, mwanzoni zilizisema: madai ya ufisadi yaliyokuwa yakitolewa na wapinzani ulikuwa umbea na uongo mtupu? Yaani CCM ilivyotembezwa zengwe hadi mhusika mkuu, mbuzi wa kafara Dk. Daudi Ballali akawaita waandishi wa habari na kuwaambia, "Sina wasi wasi na morale ya kazi iko juu."!? CCM mara imeishasahau yote haya!!!

Nne, CCM ndicho chama tajiri barani Afrika; kikimilki mali nyingi za wizi kama viwanja vya wazi vya umma vitumikavyo kama maegesho ya magari ukiachia mbali viwanja vya michezo kama vile CCM- Kirumba.

CCM haishii hapa. inamiliki miradi iliyojengwa kwa fedha ya umma kama makao makuu Dodoma, Chuo cha CCM Kivukoni na mali nyingine nyingi.

Tano, CCM ndiyo inayotajwa sana kunufaika na chumo la wizi la Benki kuu lililotumbukizwa kwenye uchaguzi aghali kwa viwango vyote. Ukitaka kujua namaanisha nini, hebu jaribu kujumlisha gharama za kununulia Khanga, vibandiko, T-shirts, mabango, matangazo, nauli za kuzunguka nchi nzima, pesa ya malazi mahotelini, per diems zilizolipwa kwa wajumbe na wapiga kampeni wa CCM nchi nzima, magari na vikorombwezo vingine halafu ulinganishe na pato halali la CCM. Utapata pesa kubwa kiasi cha kutisha. Hii maana yake ni kwamba ufisadi unaoongelewa ni mkubwa kuliko huu kiduchu tunaopewa.

Hapo bado hatujaangalia mali za vigogo wa serikali wanaoishi kama wafalme kwenye bahari ya umaskini wa kutupwa. Hapa bado hujagusia ile pesa inayotoroshewa nje na wageni wa CCM na serikali zake yaani akina Chavda, Patel na makanyabwoya wengine.

CCM kwa kutoa madai ya kipuuzi kama haya inaonekana bado ina mawazo kuwa watanzania ni wajinga wa miaka ya 60 ambapo wangeweza kukaa na kubishania milioni moja ina sufuri ngapi! Imesahau: watanzania sasa ni mabingwa wa kutumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya internet kiasi cha kuwa taifa la kwanza duniani kuutumia mtandao kufichua kashfa kubwa ya kifedha kuliko zote nchini!

Sasa tuangalie taarifa kuwa kuna baadhi ya wana CCM safi wenye uchungu na nchi yao wanaotaka mafisadi wote watajwe bila kuangalia sura zao. Hawa wakishikiria msimamo huu wanaweza kurejesha chama chao kwa wanachama toka mikononi mwa wezi na wasaka ngawira. Kabla ya kifo chake, mwanzilishi wa CCM, mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutishia hata kujitoa kwenye chama alichosema siyo mama yake. Hii ni baada ya chama kuporwa na wachuuzi wa roho na miili ya watu walioua azimio la Arusha kwa kuanzisha la Zanzibar.

Hadi Nyerere anafariki, alikuwa mtu aliyekata tamaa na kuchukia sana. Rejea maneno yake, "Nawaombea watanzania wangu’" Hii licha ya kuwa laana ni kauli ya kukata tamaa. Tunamshukuru Mungu: maneno ya gwiji hili yamedhihirika hata kabla ya kuoza. Rejea aibu na kihoro vinavyompata rais mstaafu Mkapa ambaye licha ya kumvua nguo Nyerere aliyemuwezesha kuwa rais asijue alikuwa bomu, ameifuja nchi yake na misingi yote aliyoiweka akaipigania na kuifia.

Na bado. Mkapa anaweza kukwepa kifungo leo kwa sababu Kikwete -kwa sababu anazojua mwenyewe- amemkingia kifua. Lakini ajue nchi hii siyo ya Kikwete wala Kikwete hataishi milele akiwa rais wa nchi. Na isitoshe, yeye akiponyoka hawa wengine arobaini yao itafika.

Huenda utabiri wa Nyerere kuwa CCM itakuja kufa --kama haitaacha kuwakumbatia matajiri kwa kuwatelekeza wanyonge-- ndiyo inatimia. Nani haoni wafanyabiashara wachoyo waliojipenyeza kwenye chama na kupata vyeo wanavyoipeleka CCM kuzimu?

Ukitaka kujua hatari hii, chunguza ni wabunge wangapi wako bungeni kulinda himaya zao za biashara kwa mgongo wa CCM --ambayo kama fala-- nayo imewapokea na kuwapa madaraka makubwa isijue; lao ni matumbo yao; na siyo taifa; kama ilivyokuwa agenda ya kuanzishwa kwa CCM.

Hivyo, wana-CCM wenye uchungu na nchi hii wanaweza kushirikiana na upinzani na vyombo vya habari kuwafichua manyang’au waliomo chamani walioshiriki kwenye uchafu wa BoT ili umma uwape adhabu wanayostahili. Kama mwalimu Nyerere, wasichelee lolote. Kwani CCM siyo mama zao wala Mungu wao.

Kuna haja ya kuanza kuchimba kaburi la CCM. Maana kaka na dada zake iliozaliwa nao wote wameishakufa kuanzia Ghana, Kenya, Zambia, Malawi, Senegal, Uganda, Nigeria na kwingineko. Umefika wakati wa ama CCM kuuawa na mafisadi au wana-CCM wazalendo na wasafi kuinyakua CCM toka kwenye pango la wezi wanaoichuuza yenyewe na watu wake.

Tuhitimishe. Kama CCM inataka mafisadi wafilisiwe, wa kwanza kama haki itatendeka itakuwa CCM yenyewe.

Nihitimishe na kituko. Rais Jakaya Kikwete amekaririwa akiwataka mawaziri na wabunge ama kuchagua biashara au siasa ili kuondoa mgongano wa kimaslahi. Nina maswali madogo. Kwanini angoje wawe matajiri ndipo aseme? Mbona anakatalia kutaja mali zake na wenzake?Je hii nayo ni kamba nyingine? Je waliokwishaneemeka na jinai hii wafanywe nini na ni wangapi? Je umefika wakati wa kuinusuru CCM toka kwa wafanyabiashara? Mwisho atatoa lini ombi kwa Marekani kumrudisha Ballali? Na je ataanza lini kuwashughulikia mafisadi, mabaroni wa unga, wala rushwa bila kusahau nyumba zetu?

Mungu ibariki Tanzania.
Iepushe na mafisadi,
Iondoe kwenye mizengwe na usanii.

No comments: