Wednesday, 2 January 2008

Tutasema na kusema lakini hafukuzwi mtu 2008

Mpayukaji Msemahovyo


BAADA ya Kijiwe kuwa bize kwenye chaguzi za Kenya na masuala mengine kama kufuatilia ziara ya mkuu wake kule kwenye nchi ya matumbuizo na makamuzi ya Boyz II Men, leo kimerejea kwenye hoja yake kuu-ufisadi.

Leo tunaangalia kigogo mwingine maarufu aitwaye Dadi Dalali Balaa wa Belly of Tembo (BoT-siyo Bank of Tanzania).

Mpemba anaingia akiwa na lundo la magazeti Tanzania Daima ikiwa juu ya yote. Sijui kamkopa nani hadi apoteze njuluku kwenye magazeti au kuna la mno!

Anaanza, "Yakhe mmeona huu uchafu wa sanaa chafu? Eti mkuu wa Kijiwe anasema Dalali (Sio wa Simba) hajaleta barua ya kujiuzulu? Hivi angojani huyu Yarabi?"

Kabla hata ya kufafanua vizuri kulikoni, Mgosi Machungi anadanda na mic chap chap. "Mgoshi hujui kuwa huyu hawezi kujiuzuu! Ataacha kama ataamua. Akini Mkuu kumwajibisha subutu. Nani amwajibishe nani iwapo wote ni Waarabu wa Pemba?'

Anakohoa kidogo baada ya kuvuta sigara yake kali na kuendelea. "Tilishasema akini wanakaya hawastuki. Tinapaswa kutafuta mbinu mbadaa kupambana na genge hii hata kama wana madaaka."

Kumbe kachokoza nyuki! Makengeza anaingia bila ndula. "Hebu angalia kichwa hiki cha habari." Anaanza kusoma gazeti, "Mkuu awakata ngebe wanaosema Dalali amejiuzulu".

Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu anamchomekea. "Hivi nani aliyewaroga nyinyi mnaomtofautisha jamaa na Dalali? Kwani pesa aliyokwanyua ilikwenda wapi kama siyo kumuwezesha jamaa kuja na Tsunami baada ya kutembeza takrima na aiskrimu, vitenge, khanga na manywaji? Siku Dalali akijiuzulu jua kesho yake…. Nasikia ni mgonjwa?"

Mzee Maneno naye anachangamkia mic. "Nyie hamjui. Mmesahau."

Kabla ya mzee Maneno kumaliza mipasho yake, Kapende naye ana usongo. Anakula mic, "Adui yako muombee njaa na balaa.

Kinachonishangaza ni je, atakabidhi ofisi kwa mtandao? Ama kweli alijisemea mzee Ruksa: Kaya hii ni bichwa la mwendawazimu vinyozi kujifunzia kunyoa! Hapa mkuu hatuna na kama tunaye kama alivyosema Mgosi, unashindwa umuweke upande gani."

Wakati Kijiwe kikitafakari maneno mazito ya wachangiaji, Mchunguliaji akiwa anampa gazeti Mbwa Mwitu anasema, "Mmeshikilia politiki zilipendwa za Dalali. Hamkusoma habari ya Mkuu kukanusha kuvunja baraza lake la ulaji! Tunamshangaa Dalali wakati waliomtuma afanye madudu haya wanaendelea kutanua tena na Boyz II Men! Ama kweli mwaka huu umekuwa wa dhihaka. Kijiwe kinateketea mkuu yuko na Boyz2!

Mkurupukaji kama jadi yake anakurupuka. "Laiti maneno yangekuwa ni matendo, tungewapeleka hawa majambawazi wetu Ukonga kama alivyopendekeza Dokta Silaha. Nijuacho mimi hata tunavyoongea njuluku zinazidi kukimbizwa ughaibuni." Anachukua gazeti la Thisday na kunukuu.

"Bilioni takriban 40 na ushei zalambwa kwa kulipwa kampuni ya Kadoga! Hapa hujajumlisha na za akina Deep Freezer na wengine. Hata hii kampuni ya Malkia wa Mkuu siku hizi tumeilazia damu! Kaya hii inaliwa na kila kinyama cha mwituni. Huoni hata mkuu, Lu-washa na Aziza wanavyozidi kunawiri huku wakijifanya kupuuzia madai yote yanayowahusu.

Ile Tsunami tuliyoambiwa sasa ndiyo imo kazini. Tutateketea kama kule Phuket. Tsunami hii itaua wangapi nani anajua?"

Kabla ya kuendelea, mzee Mzima natoa tangazo. Nawakumbusha wanakijiwe kununua kahawa.

Maana meza imenuna na muuza anaonekana kukereka. Msomi anatoa noti ya mia nami naongeza gwala ili watu wanywe kahawa na kutafakari. Kila mmoja anaonekana kufurahia juhudi hizi.

Msomi akiwa amechukia anakula mic. "Wazee namuunga mkono msemaji wa mwisho. Hii kweli ni Tsunami tuliyoambiwa. Nguvu za Tsunami ziko kila wizara zikifanya vitu vyake. Majambazi na maharamia wamefunga ndoa kiasi cha kutishia usalama wa Kijiwe.

Tutasema na kusema lakini hafukuzwi mtu. Kimsingi ni kama tunapeleka kesi ya ngedere kwa tumbili.

Watu wanataka gwena la walaji na majambazi livunjwe na mkuu wake! Tangu lini nguruwe akamwadhibu ngiri au chui, mbweha?

Mwenzenu nilianza kutokwa imani hasa nilipoona sura alizokuja nazo jamaa kwenye kasi ya maangamizi kwa nguvu na ari ya machukizo. Cha ajabu sura zile zile ambazo baadhi zimefanya madudu kiasi cha kumwagusha, ndizo anazoingia nazo tena mwaka 2008. Twafwaa!


Watu wamehanikiza Lu-washa kwa mfano atimliwe. Wamehanikiza Pesa tatu, Chwenge, Msolowa, Kadamage, Mungahai, wa Kupuyanga na wengine wapumzishwe. Hapa kama jibu ni kutimua basi ni kutimua genge lote bila kuangalia nyani usoni.

Wenzenu wanatuona mafala. Leo tunashinikiza Dalali Balaa ajiuzulu. Mbona hatuongelei watoto wa vikaka waliojaa ofisini mwake wakihami milki za baba na mama zao?"

Anatoa leso na kujifuta jasho huku akikamua kombe lake la tangawizi na kuendelea. "Tunaongelea wizi wa akina Balaa. Je, hamjui kuwa na deni nalo linazidi kuumka huku wanakijiwe tukiendelea kukondeana kama ng'onda.

Nani anajali iwapo wao wanashiba na kusaza wao watoto wao hata nyumba zao ndogo? Ingekuwa ni amri yangu, ningesitisha mikataba yote hata ya kuingia madeni mapya ambayo kila uchao yanafutwa magazetini na kukua kwenye nyaraka za umma. Tunaibiana mchana hapa.

Umdhaniaye ndiye siye. Mkuu kaishachemsha. Hili liko wazi. Hata ukisikiliza hotuba zake utaliona hili. Iko wapi kamati ya Kabwela iliyopigiwa kila upatu.

Watu wamekatiwa chao na sasa kinachoendelea ni usanii kama kazi. iko wapi kamati ya Mr. Six? Wamo mahotelini wakipeana vitu huku siye tukikaukwa makoo kwa kulalama. Nilishasema siku zote. Tuwatolee uvivu. Maana shibe imewalevya na lao ni inzi kufia kidondani. This is business as usual plus mendacity and hypocrisy."

Kabla ya kuendelea mzee Kidevu anatoa tahadhari. "Msomi ukichukia unaongea umombo. Hebu tufafanulie jamani."

"Sorry mzee wangu. Ni kweli nimekasirika. Nasema hawa watu pori wanaendelea kujiibia kama kawaida na uongo unaendelea mtindo mmoja. Tusipoamka na kuingia mitaani, jua tutakwisha.

Tatizo letu ni kuwa kama mbuzi. Mbuzi ana sifa ya kusahau. Hata anusurike kutafunwa na fisi sehemu fulani, kesho atarudi pale pale.

Hapa kuna haja ya wanakijiwe kuanza kutumia busara zetu kupata haki zetu. Maana tumetumia diplomasi haikusaidia zaidi ya kuonekana majuha.

Leo tunaambiwa Mkuu hawezi kuvunja genge lake wala Dalali hawezi kujizulu! Tunangoja nani? Malaika ashuke kuja kutuokoa? Ajabu ya maajabu bado tunamlilia yule yule anayetucheka na kufurahia vilio vyetu huku akitupuuzia na kutupa stori za kufanya machukizo kila aina kila uchao!"

Anakwamwa na hasira na kukohoa na kuendelea. "Jamaa zangu wa inteligensi wanasema jamaa ameamua kucheza mchezo wa nduli.

Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu anauliza. "Upi?"

Anajibu. "Kuchapisha pesa na kuongeza mishahara."

Tukiwa tunajiandaa kuishambulia mada, zinasikika habari kuwa waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Benazir Bhutto amepigwa risasi. Mtu mmoja anajisemea. "Heri yao wanaojua kujipigania hata kama wameamua kutoana roho, ingawa hilo hatuliungi mkono." Tunatawanyika kwenda kusikiliza.


Source: Tanzania Daima Januari 2, 2008

No comments: