Friday, 11 January 2008

Nenda Balali. Bado Kikwete na genge lake.

Ingawa hatimaye, rais Jakaya Kikwete amekumbuka blanketi asubuhi baada ya kutosikia la mkuu, kumfukuza kazi gavana wa zamani wa Benki Kuu, Daudi Balali na kumteua Profesa Benno Ndulu, hakuwezi kupita bila kujadiliwa.

Kwanza je ni kweli Balali amefukuzwa kazi au ni dili? Je aliyemrithi ni safi? Mbona anaonekana kuwa na sifa kama za Balali? Maana kama Balali naye anatokea huko huko Washington kunakopikwa kila upuuzi unaoutuumiza.

Je atakuwa na jipya zaidi ya kuzidi kuvuruga ushahidi muhimu ambao haujafikiwa na wakaguzi? Je mfumo uliomtengeneza na kumneemesha Balali na wenzake umerekebishwa?

Je matokeo ya "kazi’ ya Balali kwa uchumi na sarafu yetu ni yapi? Maana tumekuwa tukipewa takwimu chafu na za kubuni toka kwa akina Balali ili kulinda uchafu wao.

Je mbali na Balali na kundi lake, wanufaika wa uchafu huu wengine ni wapi? Je kama kwa kuthibitika kuwa madai ya wapinzani ni ya kweli, rais haoni kuwa naye anahusika hasa ikizingatiwa kuwa alitajwa kwenye list of shame? Je watanzania kwa mara nyingine watakubaliana na usanii huu? Je wanajua kinachofanyika na kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa? Maana tatizo letu siyo BoT na Balali bali serikali nzima na taasisi zake zote na karibu watendaji wake wote kuanzia Kikwete mwenyewe.


Kimsingi Kikwete alipaswa kufanya yafuatayo haraka na kwa uwazi kama ana nia ya kulisaidia taifa analoongoza kuelekea kwenye maangamizi:


Angepaswa ajiuzulu na serikali yake. Lakini kwa vile kitu kama hiki kwenye nchi zenye demokrasia maneno kama Tanzania hakiwezekani basi angalau rais angefanya yafuatayo:

Kwanza awaombe msamaha wananchi kwa kichwa ngumu yake na kuchelewa kuchukua hatua huku akipuuzia na kuwadharau waliompa ushauri huu.

Pili aiombe msamaha kambi ya upinzani iliyoibua uoza huu. Na si kuomba msamaha tu bali afanyie kazi mapendekezo yake.

Kwa mfano ahakikishe Balali na wote waliohusika wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake tena bila kuingiliwa na serikali kwa namna yoyote.

Pili akamate mali zao wakati kesi zao zikiendelea. Maana wanajulikana hivyo na mali zao zinajulikana.

Tatu awawajibishe wote waliohusika na uchafu huu mara moja bila kuangalia sura au ukaribu wa mtu kwake au wakubwa wenzake.

No comments: