Wednesday, 9 January 2008

Suluhu Kenya: Ni ama Kibaki ang'oke au uchaguzi mpya

NANI alijua: mzee msomi na mtu aliyepigiwa upatu kuwa mwanamageuzi na mvumilivu kama rais-tata Mwai Kibaki wa Kenya angefanya madudu kama tuliyoshuhudia nchini humo?

Nani alishuku: nchi iliyoitwa jiko la uchumi katika Afrika Mashariki ingetumbukizwa kwenye maanguko ya kiuchumi kirahisi hivi? Yametokea na tumeyashuhudia.

Genge la manyang'au na mipapa ya kiuchumi imo vitani huku mwananchi wa kawaida asiye na hatia akipoteza hata uhai na mstakabali wake kisa alitimiza haki yake kwa nchi yake!

Mchukulie Kibaki utakavvyo. Ukweli unabaki pale pale: amegeuka aibu na machukizo kwa nchi na bara zima la Afrika. Kama akili ya kawaida haitapewa nafasi, yaliyotokea Kenya yamemvua nguo Kibaki na genge lake wapambe wasasi ngawira wanaoona damu ya binadamu kama kamasi hata imwagike sawa ilmradi lao litimie!

Kilichotokea ni machukizo kwa misingi na maana yote ya demokrasia na ubinadamu. Hizi ndizo wataalamu wanazoziita siasa za king'ombe-bovine politics.

Kwa upande mmoja tunaye king'ang'anizi Kibaki na genge lake wakitaka kuihadaa dunia kuwa alichaguliwa wakati alitangazwa na Samuel Kivuitu kwa hila na ghilba za kisiasa! Kenya inabakwa na kunajisiwa na genge hili lisilosikia la muadhini wala mchota maji! Kwao hata damu zikimwagika sawa!

Kwa upande wa pili tunaye Raila Amolo Odinga anayechukuliwa kama mshindi. Huyu anaonekana kuwa na hoja kiasi cha kuwashawishi wakenya kumchagua hata kuwa tayari kumfia.

Japo uhasama baina ya mafahali wawili umefunika hata maslahi ya kitaifa, ukweli unabaki kuwa wananchi walitaka mageuzi baada ya Kibaki, mzee, mgonjwa na asiye na jipya kuwachosha.

Ajabu huyu anayeng'ang'ania aliingia kwa njia hiyo hiyo anayoiharamisha alipomshinda mgombea wa Kanu Uhuru Kenyatta! Kibaki kwa afya na umri wake hafai kuongoza nchi kwenye karne ya 21 yenye kila aina ya mikiki inayotaka nguvu na akili.

Isingekuwa roho mbaya, uroho, upofu na ukosefu wa visheni, Kibaki hakuwa na haki wala sababu ya kung'ang'ania madaraka wala kuridhia umwagaji damu kama tulivyoshuhudia.

Huwezi kujua yaliyoko nyuma ya pazia. Huenda anataka afie madarakani ili afe na siri za uchafu wake utokanao na ufisadi. Na huu umekuwa ndiyo mchezo wa watawala wetu vidhabi Afrika.

Kinachokera zaidi ni kwa mtu yule yule aliyeamuru mbwa na polisi kuwaua na kuwatesa wananchi anayedai anataka maridhiano na umoja wa kitaifa! Umoja upi iwapo ushaupiga mapanga kwa tamaa zako?

Nani amesahau kejeli, kefule na machukizo ya Kibaki aliposimama eti kuwashukuru Wakenya kwa kumchagua kwa mara ya pili utadhani walimchagua wakati alipitishwa kiwizi na tume yake ya uchaguzi? Maridhiano na umoja wa kitaifa ni kwa Kibaki kuondoka na kwenda kucheza na wajukuu zake kule Othaya.

Hapa ndipo wanasiasa wanapotenda kama machangudoa wakiwa mabingwa wa kusema lolote wasitende chochote!

Huapa kwa jina la Mungu kuwatumikia watu ilhali moyoni wana lao kuwatumia watu kujineemesha wao na wapambe wao, walamba viatu hata mbwa wao! anayebishia hili ajiulize Afrika tuko wapi na katika hali gani?

Acha ukweli usemwe: inahitaji roho ya mwendawazimu kuwahadaa wananchi kuwa unawapenda wakati ukweli wewe ndiyo chanzo cha mateso na vifo vyao kama ilivyotokea kwa Kenya na Kibaki wake. Kibaki ondoka. Ndivyo wasemavyo wakenya tena kwa umoja na sauti kuu.

Inatisha mtu kuwa tayari kufia madaraka kwa njia ya kuwaua wengine kufikia lengo hili chafu!

Inahitaji ulimi wa nyoka aliyemdanganya Eva kuwaambia wananchi nawapenda achia mbali kuwashawishi wakati ukweli unachopenda ni madaraka na marupurupu yake ya kiwizi!

Utawapendaje iwapo unachopenda ni Ikulu ili uibe na wenzio wasasi wa ngawira? Utawapendaje ilhali wewe ni Mungu mtu tena mwenye tamaa kama za Nebkadnezza?

Hakika inahitajika uwe chongo kuona mstakabali wa taifa linaloelekea kwenye mauaji ya mbari kama ilivyo nchini Kenya. Mwenye kusema na kuona haya lazima awe na sifa moja. Nayo ni kama inzi - kukosa aibu!

Huwezi kujizungushia wasasi ngawira na madikteta na mafisadi wenzako wengine hata kama ni wakuu wa mataifa ya kigeni kudai maridhiano wakati huridhiki wala kuheshimu maamuzi ya umma.

Ajabu mpangaji huyu king'ang'anizi wa Ikulu anawaita wenzake eti wajadiliane kubariki jinai yake! Nao kwa unafiki wao wanaitika! Wataachaje ilhali wote ni wale wale?

Kinachostua zaidi na kutia mashaka ni ukweli kuwa nyuma ya "zoezi la kuleta suluhu na maridhiano" wapo watu wenye kutia kila aina ya mashaka.

Tanzania kama jirani yake tunataka kuingia kutafuta suluhu nchini Kenya . Inatia shaka kama tutaweza iwapo hali kama hiyo ndani ya nyumba yetu umetushinda!

Rejea mauaji yanayodaiwa kutokana na wizi wa kura kule Zanzibar vilivyozaa kinachoitwa mtafaruku uliotushinda kwa miongo sasa.

Ajabu na madikteta kama Yoweri Museveni, Paul Kagame nao wanahanikiza wasuluhishe wakati wao ndiyo wanahitaji kusuluhishwa na wananchi wao waliowaua na kuwadhulumu!

Ila ijulikane katika usanii huu, wanaoumia ni wapiga kura na walipa kodi wa Kenya. Je, Wakenya watakubali kugeuzwa wajinga na damu yao kumwagika bure huku kura zao zikiishia kuwa upuuzi?

Japo tunahitaji amani na utangamano Kenya lakini siyo kwa njia ya usanii kama unavyoanza kufanywa na mabingwa wa sanaa katika eneo hili.

Suluhu kwa Kenya ni Kibaki kusikia sauti ya umma na kuachia madaraka anayoyamiliki kwa wizi uliosababisha madhira makubwa kwa nchi na watu wake.

Hakuna suluhu nyingine ya kudumu zaidi ya hii. Ama aachie ngazi au arudie uchaguzi ulio huru na haki vinginevyo kinachoendelea ni matusi kwa wakenya na demokrasia kwa ujumla. Wale wote wanaoipenda Kenya na Kibaki wamwambie Kibaki ukweli: Kibaki ondoka. Ni hilo tu.

Acha Kibaki aondoke utangamano na amani viingie. Kwa nini taifa liangamie eti kwa sababu wachumia tumbo wachache wanataka kulinda maslahi yao ya jinai?

Kama hatutakwepa ukweli Kibaki kama ataendelea na njama zake na ung'ang'anizi wake ataipasua Kenya kiasi cha kuiingiza kwenye machafuko ya kudumu.

Hapa ni busara inayohitajika siyo kingine. Tuweke utani kando. Kinachoendelea Kenya kinanikumbusha machozi ya mamba ya mchawi amliliaye kichanga aliyemuua mwenyewe. Kibaki ni sehemu ya tatizo hawezi kuwa au kuleta suluhu akiwa bado ni Rais wa Kenya kwa urais alioupata kimizengwe.

Umefika wakati muafaka kwa Kibaki kuondoka hata wale wanaofanana naye. Afrika imechoka. Kibaki 'has to go and he must go now'. 'Kibaki go!'


Source: Tanzania Daima Januari 9,2008

No comments: