Wednesday, 9 January 2008

Msimamo wa Kijiwe kuhusu Mwali Kibaka

BAADA ya kumtwanga salamu za onyo Mkuu wa Kijiwe kwenye ujio wa Mwaka Mpya, tumeonelea tutoea salamu kama hizo kwa mwenzao mzee aliyetia aibu ya mwaka, Emilio Stanley Githinji Mwai Kibaki.

Tukiwa tunashuhudia utitiri wa maponjoro wanaokimbia Kenya , ilibidi tuitishe kikao cha haraka ili kuelezea msimamo wa Kijiwe.

Kwanza tunalaani ujambazi wa kujifanya wananchi yakitokea machafuko unaikimbia nchi! Ni mpuuzi gani awezaye kuikimbia nyumba yake ikishika moto badala ya kuuzima!

Machungi ndiye analianzisha. "Ami yae yaiyowatokea kue Pemba sasa yako Kenya. Kwei Afiika imelaaniwa kuwa na watawaa michosho kama Mwali Kibaka wa Kenya! Tazama mzee mzima anavyojitia aibu na kuitia nchi yake matatani kwa sababu ya uchoyo utadhani ni mwanachama wa nambai wani!"

Kabla ya kuendelea Mpemba anadakia. "Yakhe usinkumbushe Wallahi. Kumbe wanasiasa wote mzazi wao mmoja! Nani alitarajia shehe kama Kibaki kufanya utwahuti namna hii Yarabi? Ajabu ya maajabu eti Mkuu wa Kijiwe aihadaa dunia enda suluhisha wakati ya Pemba yanshinda!"

"Nyie mnaongelea utumbo wa Kibaka Mwai, mbona hamuongelei la Maponjoro kukimbia nchi ilhali wao ndiyo wanaofaidi uchumi wa nchi ile? Namanga, Arusha,Tanga hata Musoma wamejazana wakingoja hali itulie wende kuchuma! Kweli Afrika imelaaniwa kama alivyosema Mgosi pale!" Anachomekea Makengeza.

Kapende anaongezea msumari. "Afrika hatuna viongozi bali manyang'au wanaotuchuuza kwa unafiki, uroho, roho mbaya na urongo. Nakumbuka Kibaka alivyotoa mpya aliposema kwenye hotuba ya kubariki ujambazi wake. Acha niseme tena kwa herufi kubwa; Kibaka toka ukacheze na wajukuu". Anawageukia Mbwa na Mzee Maneno waliokuwa wakinong'ona.

Anaendelea. "Acheni hizo. Hamkusikia akiwadhihaki wakenya: eti nipo hapa kwa utiifu kuwashukuru kunichagua tena! Nani alimchagua zaidi ya tume ya uchafuzi? Na la Msanii wetu nalo kinyaa. Mara utasikia maafriti kama M7 na Kagame nao wakija na zao. Ama kweli kwa unafiki Afrika inaongoza!"

Mkurupukaji anakurupuka. "We unashangaa utiifu! Mbona hushangai aliposema anaipenda Kenya na yuko tayari kuitumikia kwa moyo mmoja utadhani hata kuua watu ndiyo mapenzi! Wezi wetu wako hivyo. Wanajidai wanatupenda wakati wanapenda mafisadi na wizi wao wa kura na pesa ya umma".

Mbwa Mwitu anakurupuka na kuchomekea. "Unashangaa kusema utiifu! Mbona alisema tena "mapenzi ya hali ya juu"! Wenzenu wanajua jinsi ya kuwaingiza mjini majuha kwa kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa! Kama anawadanganya nanyi mnaupwakia urongo kwanini asiwatie madole?"

Mzee Maneno anaamua kupiga ngumi kubwa zaidi. "Jamaa wanatupenda kweli. Nyie hamjui. Damu na jasho letu ni vitamu kweli kweli. Hata biashara ya kutuuza kwa wawekezaji na walaji wengine inawalipa vilivyo. Nani aliwahi kumwambia ng'ombe au kuku wake anamchukia? Tunapendwa ila ni kwa faida yao hasara yetu uhai wao msiba wetu"

"Usemayo ni kweli tupu". Anadandia Mzee Ndomo. "Huoni mapenzi ya Mkuu kutumia njuluku ya Makapuku kujirusha na malkia wake Majuu! Ama kweli wamejua kutupenda wadudu hawa! Kumbe hata funza huupenda mzoga hadi akauozesha! Kweli mapenzi ya wadudu!"

Mgosi anakatua mic tena. "Tiambizane ukwei. Kama haya ni mapenzi basi ni ya changudoa ya kuambukizana miwaya! Au ndiyo ushanii tinaobambikwa kia siku?"

Msomi alikuwa amejiinamia utadhani yu alala kumbe alikuwa ndiyo akisikiliza kwa majonzi makubwa.

Alianza. "Afrika ilie sana. Lia sana mama Afrika. Huu ndiyo wimbo pekee unaoweza kukufaa. Nani alijua kuwa wale tuliowaingiza kwa mbeleko ya demokrasia wangegeuka kuwa madikteta wa kutupwa? Kibaki si wa kwanza wala wa mwisho.

Anakatua andazi lake na kutamia tangawizi na kuendelea.

"Mmesahau upuuzi aliojaribu Bakili Muluzi na Frederick Chiluba. Heri yao walishindwa. Huyu Kibaka sijui Kibaki katia fora! Kwanza jitu lenyewe limeisha expire achia mbali kufaa"

Kabla ya kuendelea kumsiliba Kibaka, Makengeza anachomekea. "Asha-ekispaya au ameishakufa! Mijitu mingine bwana, inataka ifie madarakani ili midhambi yake isijulikane. Hata Tunituni angejua yangemfika yaliyomfika hata kama Chekacheka kamkingia kifua si haba angefanya mambo"

Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu anaingilia. "Kwani hakufanya kweli kwa kula dili na jamaa yake na alivyorahisisha ujambazi pale BoT?"

"Jamani acheni Msomi atambae" Anashauri Kapende akiwa anamtolea macho Mbwa Mwitu.

Msomi akiwa anatabasamu kwa kutetewa anaendelea kumwaga sumu.

"Kibaka is a rigger not a winner" Kabla ya kuendelea anagundua kosa lake anarekebisha lugha. "Huyu si mshindi bali mwizi wa kura wa kawaida sawa na kule kwa akina yakhe." Anamgeukia Mpemba ambaye naye anatingisha kichwa kumuunga mkono huku akitabasamu.

Anaendelea. " Hata hivyo Kibaka anaonekana ni mchovu kifikira. Kipigo kilichopata chama chake cha Panua Kibaka apite (PANU) kilimtosha kutia akilini.

Kinachomsaidia hana mpango wala sera ya kutawalia vinginevyo kwa kutokuwa na wingi wa wabunge kungemgharimu. Lakini kwa vile wingi wa wabunge mara nyingi kwa serikali za kijambazi ni chanzo cha ruzuku na kupitishia uchafu wake, Kibaka anaweza kuiba na kuacha wabunge wagomee kila upuuzi au awahonge na kuhamia kwenye genge lake la PANU."

Anainua kombe lake na kukwapua tama mbili tatu na kuendelea. "Nikija kwa hili la mkuu wetu wa kaya kuombwa afanye mazungumzo, sina la kusema zaidi ya kulaani unafiki huu.

Unawezaje kuona punje kwenye jicho la mwenzio wakati lako limejaa tumbawe? Lakini jamaa hajakosea.

Kama umaarufu umeshuka Kijiweni kwanini asiusake nje ya Kijiwe? Isitoshe anaweza kuambulia safari na njuruku za per diem na siku zikaenda.

Kama wakenya watakuwa wakweli kwa nafsi zao, hawahitaji msaada wowote toka Kijiwe chetu.

Kwa kilichotokea Kenya wale mbweha wetu wa genge la Chagua Chizi Mkome au CCM (si Chama Cha Mapinduzi), wanashangilia kilichotokea.

Kwani katika uchafuzi ujao watapa mbinu ya kufanyia uchafu wao. Kilichotokea wataalamu wa makufuru hukiita wanachukua, wanaweka waaa! Au unamlamba mtu goli la kisigino. Hii ndiyo lugha ya kijambazi inayotumiwa na majambazi kama Kibaka kuhalalisha uchafu na ujambazi wao. Kwani hamjui!"

Akiwa anajiandaa kumwaga lazi, mara tulisikia kuwa Kibaka amepata shinikizo la roho kutokana na uzee na kuzidi kubanwa. Hivyo tulitawanyika haraka kwenda kusikiliza radio zetu na wenye kwenda internet, walikwenda.


Source: Tanzania Daima Januari 9, 2008

No comments: