Wednesday, 2 January 2008

Tunapoumaliza mwaka 2007 kwa kashfa

KWA safu hii mwaka 2007 una kila aina ya sifa na tathmini. Ni mwaka wenye pande mbili sawa na malimwengu mengine-mema na mazuri.

Mwaka 2007 kwa Tanzania una mema machache na mabaya mengi.

Safu hii itaudurusu kwa kuenga pande zote mbili-mema na mabaya. Tutalalia kwenye mabaya sana ili tuweze kujirekebisha. Na isitoshe ubaya huvuma kuliko wema.

Mwaka 2007 uliweka historia kuwa mwaka wenye kufumua kashfa nyingi kwa upande mmoja na wenye kuzizima nyingi kwa upande mwingine.

Bado kashfa mama wa kashfa ya Richmond inatuhangaisha huku pesa yetu tunayoipata ama kwa shida au kudhalilika - ile itokanayo na kukopa au kuomba - ikiendelea kuibwa na kutapanywa.

Rejea kufichuka hivi karibuni kuwa serikali itatoa pesa kwa Kampuni ya Dowans iliyochukua nafasi ya kampuni nyingine ya Richmond.

Rejea kutapanywa kwa pesa yetu kwenye kutafsiri bajeti yenye maumivu tuliyoibeza tangu mapema.

Rejea kufichuliwa kwa matumizi mabaya ya kodi ya umma na serikali na baadhi ya serikali za wilaya na wizara za serikali iliyofikia kiasi cha trilioni moja na ushei.

Rejea malalamiko dhidi ya safari hasara za watawala wetu ughaibuni huku wakitoa kila uongo ilmradi wakatanue na kujilipa 'per diems'.

Rejea kuzidi kuporomoka kwa sarafu yetu huku waongo wachache wakitujaza takwimu za kupika.

Mwaka 2007 unaendelea kuwa mwaka wa kashfa. Nani amesahau kashfa iliyoiacha Serikali ya Awamu ya Nne katika sura mbaya? Hii ni kashfa ya BoT na minara miwili ghali 'Twin Towers'.

Kashfa zinaendelea. Ni mwaka huu ambapo mahabusu walishikia bango upendeleo, kujuana na uvujaji wa madaraka ya umma pale ilipoibuka kashfa ya mauaji yaliyopigwa zengwe na kugeuka ya kuua bila kukusudia ya aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Hakika ni mwaka ulioweka historia ya mawaziri kuzomewa huku wakijikanganya kuelezea na kutetea kisichowezekana.

Ni mwaka ambao ulegelege na ulaghai wa wakubwa uliwekwa hadharani ingawa kwa kutumia jeuri na udhaifu wa kimfumo waliweza kutuliza vumbi bila kufua dafu. Nani amesahau jinsi TAKUKURU ilivyojivua nguo pale ilipogeuzwa nguo ya kusafisha uchafu wa wakubwa?

Mwaka 2007 bado utabakia kwenye historia kutokana na kushuhudia umaarufu wa serikali na rais wake vikimomonyoka huku wahusika wakitapatapa kila uchao kwa kuzidi kutoa ahadi lukuki ilhali zile nyingine lukuki walizotoa mwaka 2005 hawajatekeleza.

Mwaka 2007 hata hivyo unakwenda kwenye maweko ya historia kama mwaka kwa serikali iliyochoka hata kabla ya kuanza kazi maarufu kama kasi mpya ambayo kimsingi imeonekana kuwa kasi mpya kuelekea maanguko.

Ni mwaka ambapo kwa upande wa mema machache ambayo nayo hayana mchango wa serikali yalionekana. Kwani upinzani kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii uliamka na kuonyesha makucha.

Kupitia uamsho huu, upinzani uliweza kuishika serikali ulipoibua na kusimama kidete kuhusiana na kashfa kama Richmond, Buzwagi, BoT, ANBEN, Fosnik, mifuko ya mashirika ya umma na kutaja majina ya watuhumiwa wa ufisadi.

Ni mwaka ambao kwa mara ya kwanza vyama vyenye kuonyesha kuanza kujijua na kujitambua vya CHADEMA, CUF, TLP, na NCCR -Mageuzi viliunda umoja ulioonyesha cheche kiasi cha serikali kuanza kusalimu amri taratibu.

Mwaka 2007 unaisha na kuacha nyuma kazi pevu kwa Watanzania wapenda maendeleo. Unaacha nyuma kazi ya kufuatilia na kuhakikisha kinajulikana. Ni kazi ya kuhakikisha umma hauendelei kugeuzwa mbuzi wa shughuli huku wachache wakitanua ilhali umma unateketea.

Ni mwaka ulioacha somo kuwa 'inawezekana kama umma utajijua na kusimama badala ya kuishia kulalama'.

Mwaka 2007 unaondoka na kubakiza historia japo ya maudhi kwa vile wananchi hawajapewa walichoahidiwa.

Lakini ni mwaka uliowasha moto kiasi cha kutabiri uwezekano wa vigogo kung'olewa na umma kama utakubali kuwa kuleta maendeleo na kusimamia haki ni jukumu lake nambari wani, bila kuchelea patilizi, ukandamizaji na kila aina ya mizengwe na mbinu chafu za watawala wanaoonyesha kushindwa dhahiri.

Mwaka 2007 ulikuwa ni wa vyama vya upinzani kuonyesha njia.

Mwaka 2008 - bila shaka utakuwa ni mwaka wa wananchi nao kutimiza wajibu wao kwa kuviunga mkono vyama vya siasa kupambana na ufisadi uliokwishageuka kansa na donda ndugu kwa nchi yetu.

Mwaka huu uwe ni mwaka wa uamsho wa umma. Uwe ni mwaka wa kumalizia kazi iliyoanzishwa mwaka 2007, uwe ni mwaka wa kufuta kashfa kwa kuwashughulikia walioko nyuma yake badala ya kuwasafisha au kuwavumilia.

Tunapojiandaa kumaliza mwaka 2007 tukiri na kutia nia kuukaribisha mwaka wa mapinduzi wa 2008 ambapo uzoefu unaonyesha kuwa watawaliwa wanaweza kuamka na kushika hatamu za nchi zao.

Ni mwaka ambao bila shaka mambo muhimu kwa taifa yanaweza kufanyika. Muhimu ni kudai katiba mpya ili kuondokana na katiba viraka na ya kale tuliyo nayo tangu chama kimoja.

Mwaka 2008 uwe ni mwaka wa kuhakikisha kuwa tunatawaliwa tunavyotaka na inavyotakiwa na si kutokana na matakwa ya kundi la kikundi kidogo cha watu wenye kujuana ili ilhali sie tukiishia kuwa waathirika wa ghiliba na njama zao chafu.

Ni mwaka wa kumshinikiza rais kwa mfano atimize ahadi zake. Uwe ni mwaka wa kumtaka rais atekeleze kwa vitendo asemayo kila uchao kuwa yupo madarakani kwa ridhaa na kwa ajili ya watu na si watu fulani wa karibu naye.

Tumtake kwa mfano rais ataje mali zake na maofisa wake.

Awatimue marafiki zake wote waliochemsha mwaka 2007.

Wakati tukitakiana heri ya kumaliza na kuanza mwingine, safu hii inatoa changamoto kwa rais kuvunja baraza lake la mawaziri.

Maana miujiza haiji kila mwaka. Amefanikiwa kukwepa kuwajibishwa mwaka 2007 kutokana na silka na subira ya Watanzania.

Lakini mwaka 2008 asitegemee hili kuendelea kuwa kinga na nguzo ya utawala wake. Mafanikio au maanguko yake yatategemea ni kiwango gani amebadilika kuelekea mbele au kuendelea kukumbatia hasara ili impate.

Kikwete, ufanye mwaka 2008 kuwa wako kwa kufanya vizuri na kuwaondoa madarakani viongozi wasiofaa.


Source: Tanzania Daima Januari 2, 2008

No comments: