Wednesday, 23 January 2008

Vigogo mnangoja nini kijiweni?

LEO mzee mzima napayuka na kupayuka na kupayuka si kwa sababu ya ulabu kama kawaida yangu.

Nimelewa hasira na njaa kusema ukweli. Jana niliichapa pombe kiasi cha kuamka na hangover. Nimeishazoea, kuutundika ili nao mbu nikirejea wanitundike kabla ya mshirika wa bedroom naye kunitundika kwa kuniibia akiba ya mama.

Zamani wezi walikuwa wanaume, hasa walevi kama Mpayukaji ambao bila kuzamisha chupa iwe ya boa ulanzi au mataputapu mengine, siku haiendi.

Mambo yameenda yakibadilika siku hizi. Hata akina mama nao wamo kwenye kukwanyua njuluku hasa za kaya!

Hebu chukulia mfano huyu Iron Lady utadhani ameumbika kwa chuma. Juzi ameamua kukiri kwamba alishauriwa vibaya na Ballaa Dadi Dalaliii wa Band of Thugs ambayo kwa kuifupisha waweza kuiita BoT.

Zamani vibaka walikuwa vijana wasio na mbele wala nyuma, juu wala chini. Siku hizi ni watu wazima na nafasi zao, tena za kupewa na umma wanaouuma kwa uma utadhani hatujui!

Nani angelidhani waziri mzima, tena wa njuluku angejikurupukia kama ndugu yangu na mwana kijiwe mwenzangu Mkurupukaji na kuidhinisha malipo yasiyostahiki kwa Kampuni ya Kagoda? Sasa kama Kagoda kamemuingiza mjini akaukwaa mkenge, kitakapokuja kigoda si atamaliza njuluku za Kaya? Sijui naye anangoja nini?

Ajabu ya maajabu hata Mkuu wa Kaya ya Kijiwe naye ameuchuna utadhani maneno ya kujinyonga ya Iron Lady ni muziki. Au ni kwa vile Iron Lady na mkuu hawakusomea sheria kiasi cha kutoimanya? Mbona wanasheria huita hali hii ‘self-inculpatory evidence’ au ‘admission’ kwa lugha rahisi?

Je, Mkuu wa Kijiwe anangoja wapingaji wahanikize kumtaka amtimue huyu mama ambaye kama Hill Clint-on wa kule kwa Joji Kichaka Pori anavyobabaika kwenye kutoa maamuzi? Aliunga mkono majeshi ya Kichaka na Diki Chini kumvamia na kumfurusha Saadaam Husseinii eti kwa kuwa na silaha hewa za maangamizi ya umma (Weapons of Mass Destruction). Mara kwenye kampeni ya kutaka kukaa kwenye jumba jeupe lisilo jeupe bali jeupe kisera, anajikanyaga kiasi cha akina Obamaaa kumbamiza na kumkanyaga kanyaga!

We mama unangoja nini iwapo mkono wako ulibariki maasi yaliyosababisha kuangamia kwa pesa ya umma? Huoni kuwa maamuzi yako nayo ni Weapons of Money Destruction kwa Wadanganyika? Je, unangoja nini?

Ngoja nikutolee uvivu nipayuke zaidi tena bila woga wala kupinda maneno. ZM au Iron Lady pack and hit the road. Siku hizi nimesoma na naumanya ung’eng’e. Nasema mama kitoe huna dili wala sera hata kama una dola pamoja na akina Kagoda, ANBEN, Fosnik, Tanpower na wengine.

Leo nimeamua kutoa dozi tena kwa mapozi. Ngoja niwashukie wakubwa tu wanaojifanya hatujui chafu yao. Nanyi mna kosa la kigaidi la kuwa na zana za maangamizi ya njuluku au Weapons of Money Destruction.

Yupo huyu Eddie Lu-washa ambaye alikiri mwenyewe kwamba alikurupuka kuipa ulaji Richmond iliyopata mimba na kuzaa Dowans kama ilivyo mitandao ya nambari wani inavyopata mimba hovyo hovyo na kuzaa mitandao mingine midogo ya kumalizana. Hayo tuyaache. Acha nipayuke.

Eddie, una habari kitendo chako cha kukiri baada ya kuitetea Richmond kama walivyofanya wale watu wa rushwa wa TUKUKURA, ni kosa sawa na alilokiri huyo mama juu niliyempa vipande vyake?

Juzi nilipokea tuhuma kuwa binti yako naye kumbe yumo BoT akikamua na kutanua. Je, analinda hisa zako au ndiyo hayo kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka?

Eddie Lu-washa, hata kama mkuu wa kijiwe ni swahiba yako ujue una udhaifu kwa kukurupuka kama Iron Lady halafu ukasimama kwenye kijiwe cha Idodomya ukautetea huu uoza na baadaye ukakiri ulilazimika kutokana na uhitaji wa nishati. Kaka jiondoe maana huna sera kwa sasa.

Yupo kaka Basi Shilingimbili. Wewe hata kama umekula kobisi na jiwe, tunakujua ulivyosuka dili la akina Bangue of Tanzanie. Je, kaka nawe unangoja nini? Kitoe. Tumechoka na michosho.

Leo nimeamua kupayuka tena kwa herufi kubwa na kinywa kipana. Acha nipayuke kabla hamjanikolimba au kunibenea na kunigambwage kwa tindikali. Ila mjue hilo si jibu wala suluhu bali kuchokoza hasira za umma mnaouuma mkidhani ni maamuma.

Leo sijautwika. Nina mapwenti kama Mchonga na usongo kama Sokoine na Lyatonga.

Siogopi vigogo wala Wagogo. Hata vikwea na Wakwere siwaogopi. Mie natoa dozi kama kazi wala sitaki upuuzi hata ujambazi.

Kaka Ibra M7ha nawe unangoja nini iwapo, kama Iron Lady, uliridhia Richmond? Nawe kitoe hata kama unatoka eneo moja na mkuu wa kijiwe.

Siwezi kumaliza mipayuko yangu bila kumpa salamu rafiki yangu Enderea Chenga. Wewe ulishirikiana na Tunituni kuiingiza kaya kwenye balaa la mikataba mibomu ya madini. Japo uliwalamba chenga akina Tunituni na Chekacheka, jua hutaulamba chenga zako umma ambao uliishakustukia. Ujue mie naongea kwa niaba ya umma.

Tena umma wenyewe si wa kuuma bali wa kuzomea na baadaye kutoa kichapo. Wewe ni loya.

Ohoo! Nilitaka kusahau salamu za swahiba zangu wawili Niziro Kadamage na Rostitamu Aziz. Nyie nanyi yenu twayajua hata kama mnazo, lakini si za wizi kama za yule jamaa yetu ponjoro Jitu Patili? Kumbe tulidhani madingi na wazito kumbe wakwanyua njuluku za umma. Angalia Kadamage alivyoshikwa pabaya kule Landani kwenye hoteli ya… Oh! Nimesahau jina.

Rostitamu Aziz tunaambiwa ndiyo unaendesha kijiwe kwa kutumia mitandao na mitandio ya chama! Jamani, yaani hii kaya kweli hovyo! Jitu linatoka sijui wapi huko linakuwa na say kwenye kaya yetu!

Hivi Mdanganyika anaweza kwenda umangani au uhindini akafanya chafu kama hii bila kulipuliwa kama Benazir Bhutto? Je, tatizo ni sisi au hawa kunguru? Where is the problem ya matatizo jamani?

We naona unacheka. Usicheke. Hii si habari njema. Don’t cheka wakati unaliwa, you must lia na kuomboleza. Usichekecheke kinafiki kama Cheka Cheka anayechenga chenga na kudana dana kwa kutumia vicheko.

Naona na yule anashangaa maneno haya. Mbona hushangai urithi wako kugeuzwa sadaka ya vyangudoa wa nje na ndani? Mbona hushangai jamii ya makondoo na kuku? Acha uvivu wa kufikiri kama Tunituni aliyeishiwa fikra, kwa uvivu akanenepa kiasi cha kiuno na shingo kulingana huku akiwabeua wenzie kwamba ni wavivu wa kufikiri!

Acheni uvivu wa kufikiri nyie. Msijidanganye, mambo hayatabadilika au umma kuwabadilikia kama mlivyoubadilikia. Acheni kudhani wataendelea kuwa kondoo. Wanaweza kugeuka chui kama Daktari Silaha wakageuza kibao. Shauri yenu! Kalagabaho.

Nimegukie Mkuu wa Kijiwe. Bro, bado unachekea chekea matatizo haya! Bado unawavumilia magaidi wenye Weapons of Money Destruction! Una habari zamani Osamaa alikuwa best wa akina Kichaka? Alipoamua kuwa gaidi kama wao wakamtolea uvivu. Hata Saadamu alikuwa best wao pia. Alipojiingiza kwenye Weapons of Mass Destruction, walim-destroy.

Nawe mshirika huna jinsi. Achana na uswahiba na magaidi wa njuluku ya umma. Wafanyie kweli. Kwa vile wewe ni mswahili huna historia ya kujilipua, basi watimue urejeshe confidence ya wanakijiwe waliokupa kula kama Tsunami wasijue Tsunami kweli!

Nihitimishe kukumbusha. Wafuatao lazima mwaka huu watimke.

Iron Lady Zakhiya Mengi-Jii, Eddie, Enderea Chenga, Basi Shilingi mbili, Ibra M7ha, Niziro Kadamage, Rostitamu Aziz et al.

Loo! Kumbe napayuka tu! Acha nitimke kusaka pesa ya kula. Sijui ya kuishi nitaisaka lini?

Msomaji usijali, naongea peke yangu baada ya kusikia taarifa kuwa mama wa njuluku amekiri kuingizwa mjini na Dalaliii. Sijui wote hawa wanangoja nini? Mkuu naye sijui anangoja nini!

mpayukaji@yahoo.com

Source:Tanzania Daima ya Januari 23, 2008.

No comments: