The Chant of Savant

Thursday 11 February 2010

CCM ife, Watanzania wakombolewe

KATIKA harakati za kujinasua (bila mafanikio) kutoka kwenye ufisadi, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekumbwa na migawanyiko ambayo inaonyesha kitazidi kuparaganyika na, hatimaye, kufa.

Huu ni ukweli. Si fikra wala ndoto tena. Hapa ndipo utabiri wa muasisi wa CCM Hayati Mwalimu Julius Nyerere utakapotimia.

Hata kifo cha hivi karibuni cha muasisi mwingine aliyekuwa amesalia, Mzee Rashidi Kawawa, aliyekuwa na mvuto na uwezo wa kufanya mambo nyuma ya pazia, ni pigo jingine kwa CCM.

Hata hivyo, kuna faida kwa mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, hasa kutoka kwa wapenda maendeleo walio wengi. Faida hii itapatikana kama atacha CCM ijifie ili Watanzania, akiwamo yeye, wakombolewe.

Wachache wanaofaidika na utawala wake watamlaumu. Watajaribu kujinasua toka kwenye pigo hili takatifu lisilozuilika sasa, ingawa kwa bahati mbaya, muda umeshewatupa mkono. Walichelewa kusoma alama za nyakati. Wanasukumwa na matukio na si mipango na mikakati.

Kama Kikwete atahakikisha CCM inazikwa wakati wowote kuanzia sasa, atajizolea umaarufu kama alivyofanya kiongozi wa mwisho wa Muungano Kisoshalisti wa Jamhuri za Kisoviet wa Urusi (USSR), Mikhail Gorbachev.

Hapa, kuna shuruti. Salama ya Kikwete itategemea atakavyoshughulikia mafisadi papa waliotamalaki kwenye chama na serikalini, ambao wengi ni washirika, wawezeshaji na maswahiba zake wa karibu.

Lakini kuwashugulikia hakuwezekani bila kurejesha maadili ya uongozi. Hili nalo linaweza kumpatiliza hata yeye; maana watu wenyewe wanajua siri na udhaifu wake.

Ana mtihani sawa na ule alioupata Mfalme Suleiman alipoletewa kesi ya wanawake kugombea mtoto mmoja.

Kuepuka hili anaweza kufanya mambo yafuatayo:

Ama afumbe macho awatose mafisadi ili yeye anusurike, au aanzishe chama chake kama alivyofanya Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika.

Kuacha CCM indelee kumeguka kama ilivyotokea kwa KANU huko Kenya, kimsingi, ni furaha kwa Watanzania maskini. Hii imeshaanza kujitokeza kutokana na kuundwa kwa chama kipya kinachozungumzwa sana sasa (Chama Cha Jamii (CCJ)).

Anaweza kuunga mkono chama hiki kisiri siri kiwe kama mtumbwi wa uokozi kwake hata kama hatakuwa madarakani. Rais Amani Karume amefanya hivyo na hasimu wake mkuu, Katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Seif Shariff Hamad. Hili linawezekana. Kwenye siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu bali maslahi ya kudumu.

Kama tetesi kuwa chama hiki kinaundwa na vigogo wasioridhishwa na mwenendo wa mambo ndani ya CCM ni kweli, Kikwete hana jinsi bali kukiunga mkono. Pia hii itategemea kama kitapata usajili na kushiriki kwenye uchaguzi ujao.

Bado kuna upenyo mwingine kama msajili wa vyama atawatilia kauzibe. Kuna vyama kama CHADEMA na vingine. vitawapokea. Na katika anguko hili, CHADEMA, kama alivyotabiri Mwalimu Nyerere, itavuna na kuweza hata kuchukua dola. Huenda hii ndiyo sababu ya mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu wake Dk. Wilbroad Slaa kutoonyesha nia ya kugombea kwa vile wanajua yupo aliyetabiriwa atakayekuja na kusimama.

Watanzania wengi waliochoshwa na ufisadi na ubabaishaji wangetaka hili lifanikiwe haraka ili waachane na CCM waliyokwisha kuichoka licha ya CCM yenyewe kuchoka na kuchakaa.

Jaribu kupiga picha ya balaa litakaloikumba CCM kama vigogo wanaokubalika ndani na nje ya chama kama Spika wa Bunge Samuel Sitta, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM mstaafu John Malecela, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Philip Mangula, wabunge machachari kama Dk. Harrison Mwakyembe, Lucas Selelii, Fred Mpendazoe, Christopher ole Sendeka, Anna Kilango Malecela, William Shellukindo na wengine wanaotambulika kama vinara wa vita dhidi ya ufisadi wakikihama chama.

Hapa bado hujaweka vigogo kama Joseph Warioba, Joseph Butiku, Juma Nkhangaa, Mateo Qares na wengine wanaoonyesha dhahiri kutoridhishwa na mambo katika CCM. Hawa hawana tofauti na lile kundi la ODM lililokifisha chama cha KANU kule Kenya. Hawa ni lulu na almasi inayouzika kwa wapiga kura wetu maskini walioahidiwa vinono wakaishia kulishwa shubiri.

Hawa si wanasiasa wepesi, na hoja yao (kupambana na ufisadi) si nyepesi pia. Wana mtaji mkubwa. Kama ilivyokuwa kwa Wakenya, Watanzania wemeishachoshwa na CCM na madudu yake.

Vyovyote iwavyo, lazima Kikwete achague mojawapo. Je, muda uliobaki kuelekea uchaguzi na shinikizo lililopo mbele yake vinamtosha kufanya mabadiliko yanayoweza kuzuia chama kuzidi kudhoofika na hatimaye kukata roho? Je, kwa timu aliyonayo anaweza kukiokoa hata kama muda utaruhusu?

Hakuna ubishi. Kwa sasa CCM na Kikwete wanakabiliwa na changamoto kuu nne.

Mosi, kuna ufisadi ambao Kikwete aliacha umuamrie hatima ya utawala wake.

Pili kuna maelewano ya hivi karibuni baina ya Rais Karume na hasimu wake mkuu, Maalimu Seif Shariff Hamad. Licha ya kumtega, yamezaa shinikizo kutaka katiba ibadilishwe ili Karume aongezewe muda kinyume cha matarajio ya wengi.

Huu ni mtihani mkubwa kwa Kikwete na CCM. Maana asipounga mkono tendo hili linaloonekana kama ukombozi kwa Zanzibar, uungwaji mkono visiwani utatoweka.

Tatu, ni Kikwete, CCM na serikali yake kushindwa kukidhi matarajio ya Watanzania ambapo kila kitu ni shaghala baghala kiasi cha kufanya wakongwe wa CCM kung’aka wazi wazi kuwa hafai kuruhusiwa kugombea muhula wa pili.

Nne, ni kushindwa kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2005. Hili linakuwa pigo takatifu ikizingatiwa kuwa uchaguzi mkuu uko mlangoni. Maana yake ni kwamba Kikwete hana wala hatakuwa na cha kuwambia wapiga kura.

Maana uzoefu unaonyesha kuwa kugombea na kushinda uchaguzi awamu ya pili hutegemea taarifa ya utekelezaji aitoayo mgombea aliyeko madarakani.

Hili linategemea mambo makuu mawili, yaani mwitikio wa wapigakura na jinsi wapinzani watakavyolielezea kwa wapiga kura.

Je, CCM inaweza kuepuka kikombe hiki? Uwezekano ni mdogo. Rejea kichwa ngumu ya viongozi wa CCM ambao huwachukulia watanzania kama mataahira.

Hebu tunukuu maneno ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, akijipa moyo: “Naomba nikuulize, Bwana Augostino Mrema zamani alikuwa chama kipi? …na alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, na sasa yupo TLP. Pia huyo Bwana Seif Hamad wa CUF alikuwa CCM na alihama. Hivyo sisi tupo na tutaendelea kuwepo.”

Huu nidyo upeo wa Makamba. Kama akili za viongozi wa CCM wa juu ni hivi, tutarajie nini?

Rejea kuchafuka kupita kiasi kwa serikali ya sasa na chama tawala. Pia unaweza kujikumbusha hatari ya mitandao ya kimaslahi ndani ya chama.

Hivyo vyote vikichangiwa na uongozi usio na visheni inayoeleweka, ndiyo basi tena. CCM haiwezi kupona piga ua. Yawezekana huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM, na utimilifu wa utabiri wa mwanzilishi wake?
Chanzo: MwanaHALISI Jan. 27, 2010.

No comments: