Sunday, 28 February 2010

Tanzania, Afrika, nani ameturoga?

KAMA siyo kuibuka utata na mabishano juu ya pendekezo la kutumika kitabu kimoja kwenye shule za sekondari, huenda nisingeandika makala hii.

Tunaambiwa kuna utafiti umefanyika na kukuta wanafunzi wanafeli kwa kusoma vitabu vingi. Je, hata wakisoma hicho kimoja wakafeli itabidi kiondolewe?

Je, hili ndilo jibu la tatizo au sehemu ya tatizo? Huu ni uhuni unaofanywa kwa watoto wetu na mfumo wetu wa elimu. Mbona hawa wanaotushauri kuanzisha utaratibu wa kitabu kimoja walisoma vitabu vingi na havikusababisha kufeli?

Mbona huko wakubwa wanakokimbizia watoto wao wanasoma vitabu vingi? Naona ajabu sana. Binti yangu wa darasa la tano hapa Kanada ameishasoma noveli zaidi ya tano, ukiachia mbali nyingi za mwingine wa darasa la tisa ambaye ameishasoma novei nyingi na hawalalamiki wala hawafeli.

Tunajenga jamii gani ya wasomi isiyofikiri na kulinganisha, kupambanisha mambo na kupembua? Je, ule msemo kuwa ukitaka kuficha ukweli kwa mswahili ficha kwenye vitabu, unaanza kujirudia?

Akina Jumanne Maghembe wanaosingizia kufeli kutokana na kusoma vitabu vingi, wao wamesoma vitabu vingi na hawakufeli. Hata hivyo tusiwashangae sana.

Kwanza, wana uwezo wa kusomesha watoto wao nje, ukiachia mbali kusoma bure na kuwauzia wengine elimu waliyoipata bure.

Hata huko Kenya na Uganda wanapokimbizia watoto wao, baadhi ya Watanzania wenye kipato hawasomi kitabu kimoja.

Laiti wangejua kuwa wakati Kenya wakiwaletea walimu wao feki; wao wanapeleka watoto wao Uganda, wasingepoteza pesa na muda wao hivyo.

Badala ya kujenga shule na kuimarisha mfumo wetu wa elimu, tunaubomoa na kuwekeza kwenye upuuzi kama grosari na nyumba za kulala wageni.

Nani ameturoga? Msipoangalia hata Rwanda itatupita hivi karibuni. Tatizo letu ni kuwa na tawala zilizopatikana kwa njia za rushwa; zinazoendeshwa na matukio badala ya mipango mikakati.

Leo utasikia kelele juu kuhusu “Kilimo Kwanza.” Utashangaa hata hayo matrekta ya kulimia tunayoahidiwa yanaingia utata hata kabla ya kufika.

Tuna uwezo wa kuingiza mashangingi ya wabunge na watendaji wengine wasiopaswa kuwa nayo; lakini hatuna uwezo wa kuingiza matrekta.

Watawala wanalenga kuwahadaa wapiga kura. Lengo lao ni leoleo na kura na siyo mstakabali wa taifa. Je, hawa si rahisi kuuza ardhi hata watu wetu ambao wanaendelea kufanywa wajinga? Nani ameturoga?

Leo watu wazima na akili zao wanasamehe kodi ilhali wakiwalangua elimu tena dhaifu watoto wetu. Ukilinganisha kiwango cha kodi zinazokwepwa, kusamehewa na kufujwa, kama tungekuwa na mfumo na utawala bora, zingetosha kusomesha hata kutibia watu wetu bila taabu.

Je, ni wangapi wana ubavu wa kuwasomesha watoto wao nje kwenye elimu nzuri tunayoiabudia? Nani ameturoga?

Wasomi gani hawa? Leo watu wetu wanakufa njaa ilhali tunakodisha ardhi kwa wageni kuzalisha chakula kwa ajili ya watu wao; hata kutulangua sisi, kwa vile wanaweza kuwahonga asilimia 10 baadhi ya waroho walioko madarakani.

Hivi unaposoma makala hii, watu wengi wa Ethiopia wanakabiliwa na tishio la njaa. Lakini wakati hili likiendelea, makampuni ya kigeni yamo nchini humo yakikodisha ardhi na kuzalisha chakula kwa ajili ya watu wao.

Kampuni la kihindi la kuzalisha maua la Karuturi limo likizalisha maua wakati Waethiopia wakiendelea kufa kwa njaa.

Kadhalika nchini Sudan, ambamo watu yapata milioni tano wanaishi kwa kutegemea mashirika ya kimataifa kuwalisha, kuna nchi za kiarabu zinalima mpunga na kusafirisha kwao.

Abu Dhabi yenye watu milioni nne imeishawekeza nchini humo kwa ajili ya kulisha watu wake wakati Wasudani wakiendelea kuteketea. Nani ameturoga?

Kenya yenye idadi kubwa ya watu wasio na ardhi nayo imo kwenye mchakato wa kuridhia ukoloni huu kwa kukodisha ardhi yake yapata heka 40,000 kwa kampuni moja ya Qatar kando ya mto Tana ili ilime chakula kwa ajili ya watu wao.

Ajabu Kenya hiihii inataka kutuhadaa tuungane nayo ili itumwagie watu wake wasio na ardhi; waje kuzoa yetu baada ya watawala wao na walowezi wa kizungu wachache kuipora yao. Wanatulaumu kwa kutoharikisha mchakato wa kuungana.

Lakini hao hao wanapinga kuharakishwa mchakato wa kuwa na sarafu moja ya Afrika Mashariki. Wao wanataka ardhi yetu na kulinda sarafu yao. Kwetu wanasemaje? Tusiogope Wakenya wala Wanyarwanda; bali tushindane nao bila maandalizi. Nani ameturoga?

Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) Dk. Jacques Diof ameishaonya kuwa hii ni aina mpya ya ukoloni. Leo tunafukuza watu wetu kuwapisha wageni wazalishe chakula.

Rejea taarifa ya kijiji cha Namwala inayozunguka kwenye intaneti ikionyesha aina hii mpya ya ukoloni. Maana hakuna sheria zinazolazimisha wageni kuuza chakula kwa nchi zinamozalisha chakula hata wakati wa baa la njaa.

Ajabu habari hizi zinafichwa kwa vyombo vyetu vya habari hadi kutangazwa na vyombo vya nje. Habari hii ilirushwa na Shirika la Habari la Kijapani (NHK).

Nchini Madagascar utawala wa Rais Victor Ravalomanana ulidhoofishwa na kuangushwa na kashfa ya kutoa ardhi kwa kampuni ya Korea nchini humo mwaka 2008.

Rovalomanana alikodisha ardhi kwa miaka 99 yenye ukubwa wa eneo sawa na nusu ya Ubelgiji, tena bila ya kulipwa hata senti moja.

Si kwamba hawakulipa kitu. Nchi haikulipwa lakini wapenda rushwa waliokuwa na madaraka walilipwa badala ya nchi. Nani ameturoga?

Leo tunapata taarifa za kuhuzunisha kuwa mzungu mmoja huko Kagera ametangaza jamhuri yake kwa kuwanyang’anya watu wetu ardhi akisaidiwa na mgambo. Tunachekelea na hatuchukui hatua haraka.

Watu wanakodisha ardhi yetu hata kulima maua wakati watu wetu wanakufa kwa njaa au kutegemea jembe la mkono. Nani ameturoga?

Leo hii biashara zote za maana na tenda hata za ulinzi zinafanywa na kupewa watu wa nje, tena wanaoishi ughaibuni.

Leo nyumba nyingi za Msajili wa Majumba (sasa chini ya Shirika la Nyumba la taifa – NHC), zinakaliwa na raia kutoka nje wakati wafanyakazi wa serikali inayozimiliki wakiteseka huko “madongo poromoka” wanakolanguliwa pango. Nani ameturoga?

Leo watoto wa wafanyabiashara wenye kutia mashaka wananunua ubunge sisi tunaangalia tu. Tusishangae hata kesho wakinunua urais na sisi tukiwa tumekodoa macho tu. Jamani nani alituroga?
Chanzo: MwanaHALISI Feb. 2010.

No comments: