The Chant of Savant

Thursday 11 February 2010

Zanzibar leteni hoja kuvunja Muungano

MAONI ya msomaji wangu aliyejitambulisha kwa jina la Hilal, kutoka Zanzibar, yamenifanya niandike makala hii. Japo msomaji aliniandikia matusi, sikumjibu. Badala yake nimeona nijadili kiini hasa cha tatizo ambacho wengi wanakwepa kujadili.

“We chogo, mambo ya Zanzibar tuachie Wazanzibari, nyie yawahusu nini? Tunapochinjana mnachekelea. Tuachieni hii fursa tuamua mambo yetu,” alisema Hilal.

Mwanzoni nilidharau maoni ya mpendwa huyu. Niliposoma makala ya Salim Said Salim yenye kichwa: ‘Mambo ya Zanzibar waachiwe wenyewe,’ nilizidi kukuna kichwa.

Kabla ya kuzama kwenye kile kinachowashinda wakubwa zetu hata CUF, ngoja nimnukuu. “Baadhi ya waandishi wa habari wa Dar es Salaam ambao hata Zanzibar hawajafika na kuona harakati za uchaguzi ambapo watu kutoka Bunju, Kawe, Bagamoyo huja kupiga kura wamekuwa wataalamu wa masuala ya Zanzibar .”

Wao wataacha mambo ya Bara? Rejea kuwa na wabunge kwenye Bunge la Muungano ambapo hawatoki nje yanapojadiliwa mambo yasiyo ya Muungano.

Nukuu ya pili ya Salim: “Sijuwi wapi baadhi ya viongozi wa bara wamepata ujabari wa kutaka kuwaamulia watu wa Zanzibar mambo yao. Labda walitakiwa ushauri na kama ni hivyo ni nani hao waliowapa kazi hiyo?”

Ni kwa sababu wanatekeleza sera ya CCM chama tawala kilichowapa huo ulaji akina Karume wanaoonekana wa maana sana sasa kuliko chama.

Kwa kifupi, nilipata maoni mengi sana na Bwana Salim, mwandishi mkongwe, naye aliandika mengi.

Chanzo cha yote hayo ni muungano. Muungano ulifanywa na watu wawili. Hii ilikuwa sahihi wakati ule lakini si sasa ambapo umekuwa mama wa matatizo yote (si chaguzi kama tunavyoaminishwa bali muungano ambapo serikali ya muungano hutuma majeshi kuwahujumu Wazanzibari).

Japo ni pigo na aibu kwa taifa kuvunja muungano, kama Wazanzibari na Watanganyika wataridhia na iwe. Maana wakubwa zetu wameshikilia masilahi binafsi kwa muda mrefu na kuacha muungano uoze na kuchakaa kiasi cha kuonekana hauna maana. Ethiopia ilipogundua inatumia muda na raslimali nyingi kupambana na Eritrea iliridhia kuiacha iende kivyake. Na hii iliepusha hasara kubwa katika mali na roho za watu.

Wazanzibari wanaona kama Bara imekuwa kikwazo cha uhuru na maendeleo yao. Ni kweli. Ukirejea kwenye kadhia ya mauaji ya 2001 na mitafaruku mingine, kuna ukweli usiopingika ingawa ukilinganisha faida na hasara za muungano, hili si jibu pia.

Watanganyika nao wanajiuliza. Kwanini kung’ang’ania kijisehemu ambacho hakifikii hata ukubwa wa Wilaya ya Kahama?

Kutokana na haki na shuruti za muungano kutowekwa wazi kwa Watanzania, kila mmoja anamshuku mwenzie hata kwa makosa.

Kama tumeshindwa kuishi pamoja, basi tuachane au kuridhia kukata kiungo kama alivyosema Salim.

Nitatoa sababu: Kwa sasa muungano wetu si muungano kitu bali mgongano uliowekwa chini ya busati na wakubwa wanaofaidi matunda yake.

Pili, bila kuurekebisha (kuurudisha kwa wananchi wa pande zote mbili) utaendelea kutupotezea muda na raslimali. Ingawa waasisi wa muungano waliungana kwa nia nzuri, hawakufuata utaratibu (kuanzishwa na kuridhiwa na wananchi). Ndiyo maana umeshindwa kuwaunganisha vilivyo walengwa. Hata ukivunjika hawatajali japo wapo watakaojutia.

Watawala walizoea kusema: wakati ule hatukuwa na uwezo kielimu kuhusishwa kufanya hivyo. Lakini sheria ya mahusiano huwa haiangalii kiwango cha elimu bali utashi, ulazima na kufuata kanuni.

Tatu, hata baada ya wananchi kupata hicho kiwango cha ‘elimu’, bado hawakuhusishwa hadi leo licha ya kupiga makelele mengi kutaka wahusishwe.

Nne, muungano umeendelea kuwa mali ya watawala huku wananchi wakilazimishwa kuukubali kwa kuaminishwa ni kitu bora kuwa nacho. Ndiyo muungano ni kitu bora. Lakini ni hiari kukipata na kukimiliki.

Wananchi wamekuwa wakiaminishwa na kulazimshwa kuukubali muungano kutokana na watawala kuutumia kusimikana na kugawiana madaraka. Mfano, kama si kutumia kichaka cha muungano, Amani Karume asingekuwa rais wa Baraza la Mapinduzi (SMZ).

Maana kwa anayekumbuka uchafu na wizi uliotembezwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi wa 2005 na hata kabla ya hapo hawezi kuona mantiki ya mtu huyu kuwa madarakani.

Hivyo, kinachofanyika kwenye kivuli cha muungano, ni CCM na kundi la watu wachache kuikalia Zanzibar huku wakiishika mateka. Kwanini umma wa pande mbili uumie kwa ajili ya masilahi ya kundi dogo la watu?

Muungano umeifanya Zanzibar ijihisi kuwa kikaragosi cha Bara. Rejea ilivyotaka kuwa mwanachama wa OIC ikafurushwa na kukaripiwa kama mkoa badala ya nchi yenye mamlaka na haki zake kwenye muungano.

Pia kuna mawazo kuwa Zanzibar inabebwa na ni zigo kwa Bara. Rejea utitiri wa wabunge na wawakilishi ilio nao Zanzibar. Hebu angalia kijisehemu kisicholingana hata na Wilaya ya Kahama kuwa na wabunge na wawakilishi wengi kuliko wilaya za Tanganyika. Hii ni nini kama si kuwabagua Watanzania kwa njia ya sehemu watokako?

Angalia kiwango cha maisha. Wakati ni juzi juzi tu Zanzibar wameanza kulipia ankara zao za umeme wakati mtu wa Mtera akilanguliwa umeme unaozalishwa uani mwake. Lakini mtu wa kilometa zaidi ya mia tatu kisiwani alikuwa akitanua kwa kuufaidi bure!

Kifupi, muungano umechakaa; unahitaji kufanyiwa marekebisho; lakini baada ya kupitishwa kura ya maoni kuona kama wananchi bado wanautaka au la.

Kulikuwa na sakata la Zanzibar kutaka Wabara wabebe vitambulisho kuingia Zanzibar huku Wazanzibari hawafanyi hivyo wanapokuja Bara. Hili linachukua nafasi ya paspoti zilizotumika muda mrefu kama alama ya ubaguzi na ukosefu wa ulinganifu na haki sawa.

Kuna maswali muhimu ya kujiuliza. Je, hii ni tabia ya chako kitamu changu kichungu au ni ile hali ya Zanzibar kuona kama haifaidiki na Muungano? Mwanzo wa ngoma ni lele. Kwa wenye akili, tamko hili lina maana na maanawia. Je, na Bara ikiwataka wafanye hivyo wataridhika?

Jana walitutakisha vitambulisho kuingia Zanzibar bila kujiuliza: hao Wakenya au Waganda watakaotokea Bara si watahitajika kugongesha upya kwenye pasi zao?

Je, ina maana Wazanzibari hawajui haki ya usawa kwa Watanzania ndiyo inafanya kila Mtanzania awe na uhuru wa kwenda popote na kuishi popote ndani ya Jamhuri, uhuru ambao wanautumia kuliko hata hao wabara wenyewe wanaowatakisha vitambulisho? Tunadhani wanajua tena sana.

Who will get the cat out of the hat? Je, Bara, kutaka kuonyesha kuwa inajua kinachoendelea, iwatakishe Wazanzibari vitambulisho kwa ajili ya usalama wake?

Je, huu ndio mwanzo wa kuuchokana na kuanza kuupekenyua Muungano ili hatimaye uvunjike? Je, ukivunjika nani atakosa nini na nani atapata nini? Hatujui nani atakuwa wa kwanza kulia!

Wakati tukitafakari hayo, hebu tuzingatie baadhi ya matukio na hali ambazo zina ukweli na ushahidi wa kutosha juu ya umuhimu wa Muungano, nani ananufaika nao na nani hanufaiki.

Historia ni shahidi. Nje ya Muungano hakuna yeyote kati ya hawa wanaotumbua marupurupu ya ukubwa atakalia kiti alichokikalia. Nje ya Muungano serikali ya Zanzibar itaundwa na Chama cha Wananchi (CUF) na si CCM, taka usitake.

Rejea chaguzi tatu zilizopita ambapo Baraza la Mapinduzi na serikali yake vilishindwa ikabidi Bara iingilie kuwaokoa kijeshi. Je, hawa wamesahau au kuna sehemu wanatarajia kupata masilahi zaidi nje ya Muungano?

Tujalie hao Wabara nao wakianza choko choko wakaanza kuuliza, hivi Zanzibar ina nini cha mno kutubagua kiasi hiki? Je, nani anauhitaji Muungano zaidi ya mwingine?

Je, hili si changamoto kwa Rais Jakaya Kikwete aliyeahidi kuudumisha Muungano uliokuwa umesahauliwa na mtangulizi wake, Rais Mkapa? Je, atakubali kuuona Muungano unayoyoma akibakia kuonekana ameshindwa?

Kupitia chaka la Muungano, wakati dunia inapambana na ongezeko la watu, wao hawana tatizo na hilo maana wana mahali pa kupeleka watu wao wa ziada.

Wakati dunia inapambana na wakimbizi wa kiuchumi, Zanzibar hawana hili tatizo; kuna pa kukimbilia. Si kwa hayo tu. Hebu jikumbushe kadhia zao zote. Walikimbilia wapi kama si Bara? Leo hili halionekani! Tunaambiwa. Tuache wafaidi uhuru wao!

Leo wanatuzushia kuwa kikwazo. Kesho watazusha pesa na baadaye hata uraia huru. Kimsingi, kama tukizingatia maana ya Tanzania kuwa ni Tanganyika + Zanzibar, hakuna haja ya kuwa na Wazanzibari. Kuzaliwa kwa Tanzania kuliua utanganyika na uzanzibari. Kama hali hii itaendelea, watakuja kurejea Watanganyika. Hapa ndipo Christopher Mtikila anapoona mbali zaidi ya watawala wetu.

Ni wakati muafaka kwa wataalamu wa Katiba kutupa namna ya kuvunja huu Muungano ili tuache kulaumiana na kupoteza muda bila sababu.

Kabla ya kuanza kugawana mbao, ni vizuri Serikali ya Muungano na SMZ kutangaza mgogoro wa kikatiba mbele ya Mahakama ya Katiba ili uamuzi utolewe.

Kama siyo, kuna haja kuepuka mizengwe ambayo, badala ya kutatua matatizo ya Muungano, huyalimbika kwa kutimua wanaochafua ‘hali ya hewa’ na matatizo hubakia pale pale yakizaliana.

Lakini kuna haja ya kujua hatima ya nchi hii ambamo kila upande unaona kama unaumizwa na kutumiwa na upande mwingine. Je, haya si madhara na matokeo ya watu wachache kujichukulia mamlaka na kupitisha maamuzi yanayougusa umma bila kuushirikisha?

Je, hii ni changamoto kuwa wakati umefika wa Muungano kupelekwa kwa wenyewe au kuuchinja?

Kwa maana nyingine, kinachofanyika ni ishara kuwa maandishi yako ukutani- Muungano una mshikeli. Muungano ni watu, si watawala na vyama vyao.

Japo Muungano ni mali ya wananchi walioachwa nje muda mrefu kufanya maamuzi, wasiuchukulie kama kitu kisicho na faida bali wapewe muda wa kutafakari njia ya kuchukua kuelekea hatima ya Muungano.

Ni vizuri Muungano ukawa wa Watanzania badala ya watawala. Si kupiga chuku. Kwa sasa, nchi inatawaliwa chini ya Muungano wa watawala unaoitwa Muungano wa Tanzania!

Zingatio: Matatizo ya Muungano hayawezi kuachiwa ama kutatuliwa na watu wawili au vyama viwili bali wananchi wa pande zote.

Tuwatoe wananchi kwenye kiini macho cha masilahi ya Zanzibar yanayowaengua Wabara wakati wa neema na kuwahitaji wakati wa dhiki.

Kwa vile sasa hatuaminiani wala kuhitajiana, basi leteni hoja ya kuvunja Muungano ili kila mtu afaidi vyake, inagawa binafsi bado naupenda Muungano na nauunga mkono.
Chanzo: Tanzania Daima Feb. 10, 2010.

1 comment:

Anonymous said...

mimi nisaidie kwenye hili moja tu, ten years ago nilimuuliza baba angu na alishindwa kunijibu.
Wizara za muungano ni ngapi?
na zisizo za muungano ni ngapi na ni zipi?

kwanini si za muungano? na hizo zilobaki za muungano at that time zilikua nne budget yake ikoje ukilinganisha na budget ya Tanzania na Zanzibar kati ya hizo inapata ngapi?
(fikiria kilimo, elimu na ufundi, viwanda na rasilimali afya na ustawi wa jamii, miundombinu.. Mimi hizi ndio sekta muhimu kwenye nchi yoyote kuikwamua kimaendeleo)
Zanzibar ina bodi mbili za mapato, serikali ya Zanzibar inahitaji kuendeshwa na TRA inasubiri kutoka Zanzibar pia. tunapochanga hatuchangii wizara zisizo za muungano tunachangia Tanzania nzima! where expensive Ministries hazimo kwenye Muuangano, Ministrie zinapokea misaada kwa wingi hazimo kwenye Muungano, na zikiwa hazimo kwenye Muungano zipo chini ya serikali gani?
Jee kweli huu ni Muungano?