The Chant of Savant

Tuesday 2 February 2010

CCM, CCJ na UUU tutaona nani zaidi

MWENZENU nimo msibani. Nimo mashakani. Ulaji wangu, watu wangu, Bi, Mkubwa na washirika zangu mmo hatarini. Si jamaa wale wenye husda wanaonisingizia kuwa nalinda ufisadi kijiweni wameanzisha Chama Cha Jeuri (CCJ) baada ya Chama Changu cha Ugali Nyama na Maharagwe (UNM) kukibadili jina na kukiita Chama Cha Mafisadi (CCM) na wengine Ufisadi, Ujambazi na Ubabaishaji (UUU)!

Basi mwanawakwa, kijiwe hakikaliki tena hata kahawa hainyweki. Nasikia hata nguo za ndani zinanibana. Presha ishanipanda sana. Majaliwa yangu hadi sasa siyajui. Nimewasiliana na waganga, wapiga ramli hata mashushu wangu. Lakini ngoma bado nzito!

Wapo wanaosema nijilaumu baada ya kutowasikiliza kina Msomi Mkata tamaa aka Daktari Sam Sixx, Mzee Mwaminifu aka Joe Butiko, Msemakweli aka Mat Qarez na wengine wengi.

Unajua hawa jamaa waliniambia sikusikia! Nawalaumu walioniponza hasa mgosi Machungi aka Joe Makambale ambaye alizidi kunisifia nisijue nilikuwa nasifiwa ujuha.

Hata mzee wangu Kimdunge Mwehu anaonekana kupwaya kwenye zali hili. Pamoja na kuwatumia wachumia tumbo kunitabiria ushindi mnono, mambo si mambo. Je ni muujiza gani utatokea nipone na chama hiki cha jeuri bengw’e?

Japo nilishamtonya mtu wangu Joni Tendua akitendue na kukiengua kisishiriki uchaguzi, je hawa jamaa wanaokiunda wakihamia vyama vingine kama CHAKUDEMA nitakuwa mgeni wa nani mwaka huu? Je nikidondoka, nani atanilinda kama nilivyomlinda Tunituni na Anna Tamaa wake?

Hawa jamaa wa CCJ wamejua kutuvua nguo. Wanasema eti sera zao ni kulinda kahawa na kashata na raslimali nyingine kama walevi na wateja wengine! Mbona wanatisha kama ukoma hawa?

Tuache utani, walevi wamechoka, uongozi wangu umechoka na kila kitu kimechoka. Nadhani hata ndege na samaki na wadudu wamenichoka kutokana na ufisadi wangu kiasi cha kuwapa watu jeuri ya kuanzisha chama tena cha jeuri.

Mzee mzima sikubali kufa bila kufurukuta. Nikitoka hapa nawatimua Mgosi Makambale Machungi, Mbwa Mwitu Ewassa, gabacholi Rosti Tamu Kanji na mafisadi wengine ili kurejesha imani ya walevi. Hapa sina ujanja. Nisipofanya hivi nimekwisha. Maana hata rafiki yangu Karumekenge ameingizwa mjini na Madevu kiasi cha kuhatarisha ulaji wangu. Lakini huyu simlaumu. Anatetea ulaji wake na madhambi yake na kila mtu lazima abebe salaba lake ati.

Hata huyu mama aliyejiunga na kijiwe chetu hivi karibuni Wa Kupayuka Sofii Yanga naye namfukuza. Maana domo lake litakuja kuniponza zaidi. Mama linapayuka utadhani halina ubongo! Kwa nini niliache liendelee kujambisha domo lake na kuhatarisha ulaji wangu?

Hebu kwanza nijaribu kutafakari. Kwa nini hawa wadudu wameamua kuanzisha chama cha jeuri? Ahaa nimekumbuka! Ni kwa vile sera yangu ya ufisi, ufisadi na kulindana imetoa mwanya. Maana kwa sasa kila mwizi anajinywea kahawa na kujilia kashata atakavyo kana kwamba mali yenyewe haina mwenyewe. Pia Rost Tamu kanirostisha kwa kuzidi kuiba pesa kwenye fuko la kijiwe chini ya mradi wangu naye wa WEPA ambao watani wangu huita We Panya Acha kutoboa fuko la kijiwe.

Pia nadhani huu mradi wa makaa ulioletwa na Mbwa Mwitu Ewassa na gabacholi wake umezidi kunirostisha. Nimejaribu kupiga chenga kashfa hii ili ijifie bila ufanisi. Wabunge wa kijiwe nao wameshupalia kiasi cha baadhi yao kuniundia chama cha jeuri!

Hapa anayeniponza zaidi ni Mgosi Makambale ambaye inaonekana ana maslahi binafsi kwenye uchafu huu. Kila wakija juu yeye anaongeza mafuta kwenye moto kwa kuwakejeli na kusema ni wahuni. Sasa yamekuwa wameanzisha chama tena kwa jeuri. Je huyu atanisadia au atazidi kuharibu mambo? Lazima nimtimue kabla walevi hawajanitimua.

Ngoja kwanza niongee anisikie. Maana namuona anakuja yuleee! We mshenzi Mgosi Machungi mjukuu wa Kambale uitwaye Makambale, koma na ukomae. Nenda shule ukasome hata kama umebakiza miezi minne kukata roho. Wewe ni fisadi ambaye nilikupa cheo kwa bahati mbaya. Lazima mwaka huu nikutimue na mabwana zako.

Kabla ya kuendelea Mgosi kashatia timu. Anaanza: “Osie, hata kuti naakuzidi umri, nakuheshimu saana mia sikuogoha. Iituka zeze utaanza kunkank’a na ulimi wako bia hata kuitanga kikao cha sii tishezageana shoni want’hu wagima.”

Tafsiri :

“Bosi hata kama ninakuzidi umri nakuheshimu sana ila sikuogopi. Imekuwaje unaanza kunitukana tena kwa ulimi wako bila hata ya kutaka tuitishe kikao faaagha tusije kuumbuana wazee wazima?”

Anatoa leso yake mfukoni na kujifuta jasho na kuendelea: “Mgosi tiheshimiane eeehe! Kama titageukana sisi kwa sisi maadui zetu watatishinda kiahisi uje hio. Kwanini tisikae tikazungumza na tizungumze tikapata suuuhu badaya ya kutukanana hazaani bosi?”

Nami najitutumua na kusema. Hivi haujasikia wapuuzi hawa waliounda chama cha jeuri tena kwa jeuri ya kutaka kutia mchanga kitumbua changu! Hapa hakuna cha kuheshimiana tena.

Mmenitumia na sasa sikubali kuendelea kutumiwa tena. Badala ya kutekeleza sera umekuwa ukifanya maigizo na vichekesho. Sasa unaona matokeo yake? Hawa walevi tutawafunga kamba gani tena iwapo miaka mitano iliyopita hatukufanya chochote zaidi ya kila mtu kuiba mahali pake?

Kabla ya kuendelea, Mgosi alionekana kuchukia wazi wazi na kusema: “Lakini umesahau kitu kimoja. Wakati wewe na bi Mkubwa mkizuua ughaibuni ni mimi aliyejibu mashambuizi dhidi yako. Sasa kosa langu hapa ni nini bosi? Naona titume mashushu wakisambaatishe.”

Bila kufikiri nilimjibu. Kumbe nawe sasa una jeuri ya kuanza kunitisha siyo? Mashushu wa umma watumiwe kusambaratisha chama cha umma? Sasa tutaona. Kama mnajifanya mna jeuri basi mimi nitawasaidia chama cha jeuri niue chetu cha UNM tuone.

Nitafanya mazungumzo ya faragha nao kama alivyofanya Karumekenge na Madevu halafu nione nyinyi kama mtakula jeuri yenu. Mmefulia msijue. Hata best wangu Ewassa Mbwa Mwitu naye nampiga peni na kila mtu lazima hapa abebe msalaba wake.

Mara nilimuona Mgosi amenyong’onyea asijue la kufanya. Kumbe nilikuwa na safari ya kwenda zangu Uswizini. Ziara hii niliweka wazi majina ya watu nilioandamana nao. Ilibidi nianze kutafuta jinsi ya kuachana na Mgosi.

Akiwa anajiandaa kuendelea kujitetea si waandishi wa habari walituzonga. Niliwaona akina Martin, Mchunguliaji kiboko ya matrafiki na makofia meupe, Jeni Mura na wanoko wengine ikabidi niingie kwenye shangingi langu nikitoe kabla hawajaniandika vibaya.

Khalas kweisine.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 3, 2010.

No comments: