Wednesday, 27 January 2010

Tatizo ni Zanzibar si Maalim Seif

MAKALA ya Absalom Kibanda kuhusu mustakabali wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla haiwezi kupita bila kujadiliwa.

Naomba niungane na Kibanda na kutofautiana naye kimtazamo.

Kwanza nakubaliana na Kibanda kuwa tatizo ni Zanzibar si Maalim Seif ingawa naye ni sehemu ya tatizo. Kabla ya Seif kuja na madai ya kuahirishwa uchaguzi na kumuongezea muda Rais wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Amani Abeid Karume, Seif alikuwa akivutia na kuonewa huruma kutokana na kuibiwa ushindi kama ambavyo mara zote amedai.

Katika makala tajwa Kibanda anaonekana kutekwa na hoja za Maalim Seif Sharrif Hamad, hasa woga. Ni kweli Zanzibar imepitia kwenye mikiki na mikwaruzano mingi kabla na baada ya uhuru.

Kwa vile tumeishaainisha kiini cha haya yote kuwa ni wizi wa kura na uchaguzi usio huru na wa haki, tunapaswa kutafuta majibu yanayokubalika kisheria na kuingia akilini kimantiki.

Kwa vile wote tumeishatambua umuhimu wa amani ya Zanzibar kama ngazi ya amani ya taifa, hakuna haja ya kugwaya kutafuta jibu hata kama ni kidonge kichungu.

Ingawa Kibanda ameridhia kuchezewa kwa katiba na kusogezwa mbele uchaguzi, kuna mambo ya msingi yamempiga chenga. Kwa mfano, anaridhia kusogezwa mbele uchaguzi. Hili haliingii akilini hata kama lina nia njema kwa nchi. Kwanini tusifanye yafuatayo:

Iundwe tume huru ya uchaguzi ambayo itaundwa na vyama vyote vya siasa na asasi za kiraia kama inavyopaswa kuwa kwenye uchaguzi wa vyama vingi.

Bado tuna muda wa kutosha wa kufumua na kusuka upya tume ya uchaguzi itakayoundwa na kukubaliwa na pande husika.

Pili, uchaguzi uendelee kama kawaida. Tofauti, usimamiwe na waangalizi huru wa kimataifa.

Kama kweli CUF wamekuwa wakiibiwa ushindi, hawana haja ya kugwaya kuingia kwenye uchaguzi. Maana wapiga kura wao bado wapo na kinachogomba ni mfumo.

Tatu, turekebisha mazingira ya kampeni ambapo vyombo vya habari vya umma kama radio na runinga zitoe airtime sawa kwa vyama vyote vitakavyoshirika uchaguzi.

Hivyo basi, hoja iwe kuweka mazingira ya uchaguzi huru na haki na si kuchezea katiba.

Kama kweli CUF wana imani na rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, kwanini wasitumie fursa hii kuingia kwenye uchaguzi?

Na kama kweli CUF ilikuwa ikishinda na kuibiwa kura na ushindi kama ambavyo CUF wamekuwa wakidai, sasa wanaogopa nini wakati huu wanapoaminiana na Karume kiasi cha kumuona kama ndiye muarobaini wa kuivusha Zanzibar?

Nne, kwa vile makubaliano ya Karume na Seif ni kwa ajili ya wananchi wote wa Tanzania na si Zanzibar pekee kama inavyoanza kuaminishwa, lazima yaliyojadiliwa na Karume na Seif faraghani yawekwe wazi ili umma ujue.

Maana ni juu yake, si wawili hawa. Hawa ni viongozi tu wanaoweza kutoweka lakini umma siku zote utakuwapo. Kuna haja ya kuangalia mbali.

Tano, muafaka utokane na kuangalia sheria na kukubali hoja za upande mwingine badala ya ‘one man show’ inayoendelea.

Sita, suluhu itafutwe kwa kushirikisha vyama viwili vinavyokinzana badala ya watu wawili binafsi.

Leo maalim Seif na CUF watakuja na madai ya kubadilisha katiba ili kukidhi mahitaji yao, tutakubali. Kesho kikiundwa chama kingine cha siasa au hata CCM ikajikuta ilipo CUF, nao watakuja na wazo kama hili. Tutachezea katiba mara ngapi? Hakuna haja ya kujifunza mchezo mchafu hata kama nia ni nzuri.

Hatuna haja ya kuvunja katiba.

Ingawa huu ni mtego na mtihani wa aina yake kwa CCM na taifa kwa ujumla, CCM itapaswa kuwa makini na kusimamia ukweli. Iji-commit kwenye badiliko hili hata kama maana yake ni kuinyima ulaji.

Hii itasaidia kuisafisha CCM kama uchaguzi utakuwa huru na wa haki na mshindi wa kweli atapewa ushindi wake.

Hakuna ubishi. Kuna hisia kuwa kuna hoja fichi ya Uzanzibari dhidi ya Muungano. Hii imesimikwa na matamshi ya Seif hivi karibuni kuwa Bara hawapaswi kuongelea mambo ya Zanzibar.

Hili haliwezekani na haliingii akilini. Kwanini tumekuwa wote kwenye mazonge yote haya kwa muda wote wa zaidi ya miaka 40 halafu leo tunaenguliwa kana kwamba hatuna haki kwenye masuala ya Zanzibar ambayo ni sehemu ya nchi moja ya Tanzania?

Ingawa Kibanda amekubaliana na msimamo wa wanachama wa CUF kuhusiana na suala zima ambalo hawalijui undani wake zaidi ya kupewa matumaini kuwa linalenga kuleta amani ya Zanzibar, kuna haja ya kuambiwa kilichomo kwenye makubaliano husika.

Kitendo cha Kibanda kukubaliana na hoja ya kuchezea katiba ikiwa ndiyo njia ya kutibu majeraha ya Zanzibar hakitoi jibu la tatizo lenyewe. Hatuwezi kuacha kufanya uchaguzi eti kwa kuogopa vurugu. Kinachopaswa kufanyika ni kutatua tatizo na si matokeo ya tatizo.

Kibanda anasema: “Ni jambo la kusikitisha kwamba wanazuoni ambao wameingia kwa kujua au kutojua katika kundi la wachambuzi wanaomshambulia na kumsuta Maalim Seif, kwa sababu tu ya kushindwa kwao kutambua au kwa sababu ya kusahau kwao kwamba Zanzibar haijapata kufanya uchaguzi huru na wa haki katika chaguzi tatu za vyama vingi za mwaka 1995, 2000 na 2005.”

Hii hoja haina mashiko. Maalim Seif ‘anashambuliwa’ na kukosolewa kutokana na alivyoleta na kutetea hoja yake ambayo si ya kidemokrasia, hasa pale anaposhinikiza lake liwe asijue kuwa kama anavyosimamia masilahi ya chama chake, na wapinzani wake wanasimamia masilahi na sera za chama chao ambacho kwa bahati mbaya ni tawala.

Hapa suluhu inaweza kufikiwa si kwa kushinikiza, kutishana, kuenguana au kuitana majina ya ajabu kama kidudumtu au wasioitakia Zanzibar mema bali kufuata sheria na kuona mbali.

Tatizo kama nilivyobainisha hapo juu kuwa ni kutokuwapo uchaguzi huru, basi tutafute namna ya kuwa na uchaguzi huru lakini si kumuongezea muda Karume au kusogeza mbele uchaguzi. Kama walitaka hivyo, kwanini wamengoja hadi saa za majeruhi kama kweli hakuna namna?

Leo Karume ameishatamka wazi wazi kuwa hataki kuongezewa muda. Je, atakapojipiga mtama ilhai kilichokubaliwa baina yake na Maalim Seif bado ni siri ya wawili hakijulikani, Kibanda na wenye mawazo kama yake hawaoni kuwa ataeleweka kama alikuwa akichezea akili zetu kwa kujifanya hataki kuongezewa muda wakati ukweli ni vinginevyo? Je, hii haitamjengea kutoaminika mbele ya umma litakapokuja suala zima la kuandaa mazingira ya uchaguzi huru?

Kuna hili la serikali ya umoja wa kitaifa. Nadhani Tanzania hatujafikia huko, zaidi ya kuwa na tume huru ya uchaguzi na mazingira muafaka kwa uchaguzi huru.

Uzoefu unaonyesha kuwa serikali za umoja wa kitaifa si jibu la matatizo bali mafuta kwenye moto wa matatizo. Kenya na Zimbabwe ziliridhia kuundwa kwa serikali za umoja wa kitaifa.

Jiulize mwananchi wa kawaida amefaidika nini zaidi ya wahusika kutumia muda mwingi na rasilimali kulumbana wakishindania ukuu? Niliwahi kuliandikia hili kwenye jarida la The African Executive Magazine Nairobi Aprili 30, 2009 chini ya kichwa cha ‘Power sharing deals; Africa ’s anathema.’

Kwa sasa Wakenya hata Wazimbabwe wanajuta kwanini walikaribisha jinamizi hili.

Maana wahusika hawana muda wa kuwatumikia zaidi ya kuwatumia kutafuta madaraka. Tanzania haiwezi kwenda huko.

Huwezi kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa upande mmoja wa nchi huku upande mwingine ukiendeshwa na serikali ya chama kilichoshindwa. Lazima kutakuwa na mgongano mkubwa katika utekelezaji. Hili ni rahisi kuliona. Halihitaji uwe na PhD kwenye political science.

Hata hivyo Kibanda ameshindwa kuibua kitu kingine muhimu-muungano wetu unahitaji marekebisho ili kuepuka kuendelea kuwepo mazingira ya wizi wa kura na vitu kama hivyo.

Hakuna ubishi. Muungano wetu ni wa kale na unaendeshwa kikale tofauti na mazingira ya sasa. Ingawa CUF hawaweki wazi madai yao-wangetaka yaendelee kuwa - kuna shaka.

Kuna hisia za kuona kama Zanzibar imedumazwa na Bara.

Hili unaweza kulipata kwenye maneno ya Maalim Seif aliposema anataka Zanzibar iwe Hong Kong ya Afrika Mashariki. Hii si ndoto nzuri. Hapa tatizo si muungano, bali serikali zisizo na visheni na mipango mizuri hasa kupambana na ufisadi na ubunifu.

Nafasi haitoshi. Kibanda na Seif wanaweza kuwa na hoja. Kinachowaangusha ni kuangalia matokeo badala ya mzizi wa tatizo. Yote yanawezekana. Lakini suluhu itokanayo na kuvunja katiba si suluhu kitu na haitufai kama taifa. Ieleweke. Tatizo ni Zanzibar si Maalim Seif, ingawa naye ni sehemu ya tatizo.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 27, 2010.

2 comments:

Anonymous said...

Nice dispatch and this fill someone in on helped me alot in my college assignement. Say thank you you for your information.

Anonymous said...

I would like to exchange links with your site mpayukaji.blogspot.com
Is this possible?