Friday, 22 January 2010

Mkuchika asituchonganishe na jeshi


HATUA ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika kufungia gazeti la KuliKoni kwa siku 90 inalenga kuchonganisha jeshi na wananchi.

Mkuchika anasema gazeti limetenda “kosa” la kuandika taarifa za kuvuja kwa mitihani ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kwanza, huu ni uonevu na hatua inayolenga kupoka haki ya binadamu ya kujieleza, kutoa na kupokea habari bila kizuizi. Waziri anazima sauti ya wasio na sauti.

Pili, kumekuwa na tuhuma za kughushi vyeti vya taaluma nchini. Wanajeshi hawajawahi kuhusishwa kwenye tuhuma hizi. Tatizo la ufisadi wa kitaaluma linazidi kukua sawa na ufisadi mwingine.

Mawaziri wapatao watano na wabunge kadhaa wana vyeti vya kughushi. Hili kwa sasa si kosa kwa kuwa limetendwa na wateule. Si rais wala bunge wamewawajibisha watuhumiwa; hata kuwakaripia.

Hii ndiyo maana kitendo cha gazeti la KuliKoni kufichua uoza kama huu kimejibiwa kwa kulifungia badala ya kulipa nishani. Limegusa ambako wakubwa wasingependa paguswe. Bali naamini hata jeshi haliungi mkono uamuzi wa waziri.

Askari wengi wangependa ufanyike uchunguzi ili waliotenda kosa wakipatikana waadhibiwe. Kwani, siyo jeshi lote linalohusika na mitihani; utungaji wala usimamiaji.

Hivyo hatua ya Mkuchika inatuelekeza kuona kuwa watawala wanataka kulibinafsisha jeshi kwa kulijengea sifa chafu. Hata haya madudu yanayoitwa kampuni ya dhahabu ya Meremeta na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi serikalini, ambamo jeshi letu limehusishwa, tayari yanajulikana kuwa ulikuwa mradi wa watawala na jeshi lilitumiwa kama pazia.

Hivyo, kama kuna mashaka katika kilichochapishwa na gazeti, basi ulihitajika uchunguzi kama alivyopendekeza mhariri wa gazeti husika ili ukweli ujulikane.

Tusisitize. Kwa jeshi lenye kufanana na watu linaolinda na kutumikia, inapotokea taarifa kuhusu kashfa au uvunjaji wa sheria au kanuni, haliwezi kuogopa kuandikwa au kutendewa sawa na Watanzania wengine.

Kitu gani Mkuchika anaweza kusema hakiwezekani kutendwa na jeshi? Mara ngapi wanajeshi wamewapiga polisi? Mara ngapi wamewapiga wananchi, tena mkoani Dar es Salaam?

Kila uchafu wa aina hiyo unapotokea, utawala wa jeshi unachukua hatua ya kuchunguza na hata hatimaye kuadhibu wahusika. Kwa nini kunakuwa na uchunguzi? Ni kwa kuwa makosa au uchafu haukutendwa na jeshi zima.

Kwa hiyo, kama kuna wizi wa mitihani haliwezi kuwa kosa la askari wote. Haliwezi pia kuwa kosa la kwanza ndani ya JWTZ. Lazima wawe wachache wanaoweza kugundulika kwa njia ya uchunguzi.

Waziri anakinga nini?

Kinachoweza kujadiliwa hapa ni, kama hakuna tatizo kwanini “wahusika” wanakataa kuunda tume na kukubali taarifa ya tume iwe wazi tena neno kwa neno?


Je, waliokataa uchunguzi ni jeshi au serikali ambayo inaonekana ililichukulia hili kwa hasira na ukosefu wa busara kwa faida zake kisiasa? Hatua hii nayo inalenga kuwatisha wananchi na kujenga hofu kwa jeshi lao.

Kimsingi, kufanya kama serikali ilivyofanya, licha ya kuficha ukweli, imelifedhehesha jeshi letu na kuua ukweli.

Kwingine Afrika ambako kila kitu juu ya jeshi ni siri, “usalama wa taifa” umezaa “uhasama wa taifa.” Tanzania tusifikishwe huko. Bado tunaliheshimu na kulithamini jeshi letu.

Waziri atumie busara badala ya hasira. Asijenge imani ya kila kitu jeshini kinakwenda vizuri na hakuna kinachoweza kukosewa. Tafadhali Kapteni George Mkuchika usituchonganishe na jeshi. Lifungulie gazeti la KuliKoni haraka na utafute sababu nyingine.

Chanzo: MwanaHALISI Januari 20,2010.

No comments: