Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma wakibembea nchini Jamaica.
WATANZANIA wengi wanajiuliza: Kwanini siku hizi rais anapokwenda ziarani nje ya nchi ujumbe wake hauwekwi wazi?
Je, kunakuwa na watu – mfano wanafamilia, marafiki, washirika hata mafisadi – ambao asingependa wajulikane au wasiostahili lakini bado wanafaidi kodi ya umma?
Kinafichwa nini kama hakuna namna ya ufisadi au ufujaji pesa ya walipa kodi maskini?
Kisa cha mwisho kutokea ni cha safari ya juzi nchini Jamaica ambapo tulionyeshwa picha ya rais na gazeti la serikali akipanda ndege kwenda Jamaica na baadaye picha akiwa anafika uwanja wa ndege wa Manley, mjini Kingston .
Hapa ndipo tulijua kuwa kumbe aliandamana na mkewe. Zaidi ya hapo hakuna anayejua idadi na majina ya watu alioandamana nao rais. Kwanini tufichwe wakati wanatumia kodi zetu kwenda kutumbua huko?
Hata ukiangalia kinachompeleka huko ni kutuwakilisha ingawa mara nyingi hatuhitaji hili kwa kuzingatia hali yetu mbaya kifedha.
Kipindi fulani yalitokea malalamiko kuwa rais anatumia pesa nyingi kutalii ughaibuni. Wapambe wake walijibu kuwa huenda kule kuomba ingawa hawakutwambia katika ombaomba hii amewahi kupata kiasi gani kikilinganishwa na alichotumia kufanya hivyo.
Inashangaza kwa rais wa nchi inayowategemea wahisani kwenye bajeti – kwa aslimia 40 – kurukaruka na kutumia mabilioni ya shilingi bila kuangalia hili.
Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye utegemezi mkubwa kwa wafadhili na inayoshika namba ya juu kwa rais wake kufanya ziara ugenini.
Katika bejeti ya mwaka wa fedha wa 2009/10 (Julai-Juni), aslimia 11.4 ya bajeti yake au $831,000,000 ilitolewa moja kwa moja na nchi 14 wafadhili.
Kwanini hili halimsumbui rais kama kweli anadhamiria kutuletea maisha bora kama alivyoahidi, ingawa hali ilivyo hakuna kitu kama hicho.
Gazeti la The Economist la 7 Mei , lilihoji mantiki ya Kikwete kutumia muda mwingi nje akihangaikia matatizo ya nje huku akiyapuuzia yale ya ndani hasa uchumi na ufisadi.
Kwanini rais au washauri wake hawataki kuliona hili? Je, nchi inaweza kuendelea kwa kutegemea sera za nje tu bila kuwa na sera madhubuti za ndani?
Je, uchumi wetu unaweza kukuzwa na misaada na biashara tu bila kuwa na uwajibikaji na nidhamu ya matumizi?
Kama ziara za rais zinalipa zaidi ya kuwa utalii binafs, mbona hatuwaoni akina Mwai Kibaki (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) hata Komredi Almando Guebuza (Msumbiji) wakikesha kwenye ndege lakini uchumi wa nchi zao ni imara kuliko wetu?
Turejee kwenye usiri wa wanaoandamana na rais. Licha ya majina ya wanaondamana na rais kuwa nadra kutangazwa, mke wa rais naye anaonekana kushabikia aina hii ya utalii.
Kwani kwenye ziara nyingi hupenda kuandamana na mumewe bila wote wawili kujali kuwa kufanya hivyo ni kumuongezea mzigo mlipa kodi huku wakizidisha mateso kwa watu wa kawaida.
Kama anapenda sana kutanua si ampe uwaziri kama alivyofanya imla wa Uganda ili awe na uhalali wa kuandamana na rais kila aendeapo ughaibuni? Mbona hatumuoni mikoani na rais ingawa rais hufanya ziara za mikoani kwa nadra?
Hebu fikiri, kwa mfano, kwenye ziara zisizo na umuhimu za kujitambulisha alizofanya Kikwete mwaka 2006; hata huko aliandamana na walaji.
Endelea kujiuliza: Ziara hizo ziliteketeza mabilioni mangapi ya shilingi za mlipa kodi? Kwanini kujitambulisha nje ya nchi kana kwamba ndizo zilikupigia kura? Mbona hatuwaoni marais wa nchi nyingine wakija kwetu kujitambulisha?
Hebu jionee baadhi ya ziara: Rwanda, Uganda, Kenya, Swaziland, Msumbiji, Zimbabwe, Botswana, Namibia, Afrika Kusini.
Nijuavyo, rais yeyote akichaguliwa hutambulishwa na vyombo vya habari duniani. Na kama ana wasiwasi sana na kujulikana kwake, basi anaweza kuwaagiza mabalozi wake walioko nchi husika kufanya kazi hiyo.
Sikumbuki kuona marais wapya kama Ian Khama (Botswana), Rupiah Banda (Zambia), Bingu wa Mutharika (Malawi) au Jacob Zuma (Afrika Kusini) wakija kujitambulisha Tanzania. Kwanini iwe big deal kwa rais wetu kujitambulisha kwao?
Haya ni masuala ambayo wapinzani wanapaswa kukumbusha wapiga kura kuonyesha Kikwete asivyofaa kuchaguliwa tena. Hana uchungu na nchi hata kidogo.
Tuchukue kuwa kila ziara rais alitumia Sh. 500,000,000. Ina maana kujitambulisha kumelihujumu taifa si chini ya Sh. 5 bilioni.
Nimefanya makadirio kwa kurejea maneno ya waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye alipofanya ziara Marekani na kutumia Sh. 500 milioni alizosema zilikuwa kidogo.
Je, fedha hii ingesomesha vijana wangapi vyuoni, kutibia wagonjwa au kujenga shule ngapi ukiachia mbali kujenga kilometa kadhaa za barabara?
Je, kwa uzembe na israfu hii, kwa kipindi kizima cha urais, rais atakuwa amepoteza fedha kiasi gani ambazo zingeweza kutukwamua kimaendeleo?
Hapa hujaongelea mawaziri wake wanaoweza kufuatwa na mashangingi kila waendapo ili kujishaua.
Hebu angalia hili. Rais anatumia fedha za walipa kodi maskini kwenda kushangilia timu ya Real Madrid nchini Hispania. Ilikuwa 15 Septemba 2006.
Je, hii ndiyo njia ya kujali mateso wanayopata Watanzania? Kuna haja ya mabadiliko.
Chanzo; MwanaHALISI Januari 6, 2010.
No comments:
Post a Comment