Thursday, 14 January 2010

Kawawa, hatukuenzi, tunakusanifu tu

Rais Jakaya Kikwete akiteta jambo na marehemu mzee Rashid Kawawa.Ni wengi wamejitahidi kuelezea walivyomjua marehemu Rashid Kawawa mmojawapo wa viongozi waadamizi na waasisi wa vuguvugu la kupigania uhuru wa Tanzani na rafiki na mshirika wa karibu wa nguli baba wa taifa marehemu Mwalimu Julius Nyerere.

Ukijikumbusha vilio na mayowe na machozi ya mamba kwenye msiba wake hivi karibuni, unaweza kuona ukweli wa kichwa cha habari hapo juu-unafiki unafiki unafiki mtupu!
Ni kitu kimoja kilikosekana katika onyesho hili-nyimbo zilizotungwa tayari kuomboleza kifo chake.

Kama Mwalimu Nyerere, Kawawa alikuwa mkiwa na mwenye sononeko litokanalo na kushuhudia mema yake yote yakiporomoshwa hasa baada ya kuingia awamu ya tatu na ya nne ambazo zinasifika kupanua ufa uliowekwa na utawala wa awamu ya pili chini ya dhana mbovu ya ruksa ambayo kimsingi ndiyo msingi wa ufisadi na kuvunjika kwa maadili tunavyolalamikia. Rejea kuvunjwa kwa Azimio la Arusha chini ya utawala huu na kuundwa ujambazi wa Zanzibar.

Leo huu si mjadala wetu. Tunataka kubainisha kuwa machozi yaliyomwagwa kwa ajili ya Kawawa ni ya mamba na sifa alizopewa ni za unafiki. Wengi wa waliomwelezea Mzee Kawawa, walimwelezea kama mtu msafi aliyechapa kazi na kufuata maadili. Je wao wanachapa kazi na kufuata maadili kama yeye au madili na soga?

Kawawa na mwenzake Nyerere waliweka miundo mbinu kwa taifa kisiasa hata kijiografia. Je hawa wanaowanafiki na kuwasifia wanafanya nini zaidi ya kubomoa vitu hivi? Muulize Benjamin Mkapa. Wakati akina Kawawa walianzisha NBC yeye aliiuza tena kwa bei ya kichaa!

Muulize Jakaya Kikwete rais wa sasa, akina Kawawa walichunguzana na kutimuana kama ilivyotokea kwa Marehemu Oscar Kambona na wengine. Leo tunalindana! Rejea kushindwa kuwawajibisha watuhumiwa wa ufisadi na kughushi waliojazana kwenye ofisi za umma.
Je namna hii twanaweza kumuenzi au kumheshimu Kawawa zaidi ya kumuona kama mzee mshamba ambaye hakujua kutumia madaraka yeye, familia yake na marafiki zake? Huwezi kumuenzi mtume Mohammad (SAW) kwa kula nyama ya nguruwe au Yesu Kristo kwa kupenda utajiri wakati wao kwao hivi vitu vilikuwa haramu na zahama.

Leo kila mtu atajifanya anamuenzi na kumjua Kawawa kwa vile ameishatoweka. Ukweli ni kwamba hawampendi bali kumtumia tu. Hii imenikumbusha mhindi mmoja tapeli ambaye amekuwa akimtumia baba wa taifa bila kustukiwa. Ni juzi juzi amejinasa pale alipodai taasisi yake inaongozwa na watu fisadi wakati fisadi ni yeye.

Kawawa alisifika hadi kuitwa simba wa vita. Bahati mbaya hawa wanaojifanya kumjua na kumuenzi si chochote bali wasaliti ambao ni panya kwenye ligi ya kumtafuna simba wa vita Kawawa ambaye vita yake ilikuwa kumkomboa mtanzania.

Huwezi kuridhia mikataba mibovu inayosababisha kuibiwa raslimali walizolinda na kutunza akina Kawawa ukamheshimu Kawawa. Huwezi kuuza viwanda na mashirika waliyoyaanzisha akina Kawawa ukawaheshimu hadi kuwaenzi zaidi ya kuwatumia kwa sababu binafsi kisiasa. Huwezi kuingia madarakani kwa pesa chafu za EPA tofauti na wao walioingia kwa uchapakazi na uzalendo wa kupigiwa mfano ukawaenzi mashujaa hawa. Huwezi kutawala kwa ushikaji na usanii ukawaenzi mashujaa hawa. Yote katika yote, huwezi kukataliwa nao ukaja kuukwaa baada ya wao kuondoka ukajifisifu unawajua na kuwaenzi. Huenda neno kuenzi lina maana nyingine tofauti na tuijuayo. Kama ni hivyo sadakta.

Kawawa na wenzake waliongoza nchi. Hawakuiacha ijiendee au kutawaliwa na mafisadi nyuma ya pazia. Walijenga, kuheshimu, kutekeleza na kutegemea miiko na misingi ya uongozi siyo watabiri, mafisadi na mitandao. Walevi na wazinzi hawawezi kusafisha makaburi ya watakatifu. Wakifanya hivyo jua basi ni kufuru sawa na watawala wa sasa kuwaenzi waasisi wa taifa hili wanaloliuza kwa hongo ya upuuzi mdogo mdogo.

Hatuna uchungu na taifa hili kwa sababu hatukulivujia jasho wala kulihangaikia zaidi ya kulipoka kwa njia zao za kifisadi na jinai na kulikabidhi kwa mabwana zetu.
Tungemuenzi Kawawa tungepambana na ufisadi badala ya kuupamba kwa mbinu hizi na zile. Tungemuenzi Kawawa tungechukia rushwa, utukufu, kupenda anasa na sifa tusizo hata stahili. Tungemuenzi Kawawa tungeheshimu maadili ya uongozi aliyoanzisha na si madili kama ilivyo.

Kawawa alisifika kwa kukataa posho za vikao visivyokuwa na faida zaidi ya kuwa vigwena vya ulaji.

Kawawa aliwahi kuua simba waliowasumbua wanakijiji wenzake. Sisi tumefuga majini yanayowasumbua watu wetu. Bila majini haya hakifanyiki kitu hata kiwe kidogo namna gani.

Wao waliwekeza kwenye utu na watu. Sisi tumewekeza kwenye vitu na wawekezaji na mafisadi wetu. Wao waliishi kwa ajili ya kesho. Sisi tunaishi kwa ajili ya le oleo bila kujua kuna kesho-vipofu na majuha.waliasisi ujamaa na kujitegemea. Sisi tumeasisi uhujumu (uhujumaa), kujimegea na utegemezi. Waliasisi Tanzania ambayo tumeigeuza Tanzia.

Walijenga taifa tunalouza na kubomoa. Waliongoza kwa mifano safi . Tunaongoza kwa mifano michafu. Rejea EPA, Richmond , CIS, ANBEN, Tanpower na uchafu mwingine. Wala maskini hawakujilimbikizia mali za wizi kama sisi. Rejea ukwapuzi wa Kiwira na pesa zitokanazo na hongo na NGO za wake na washirika zetu. Hawakuwarithisha madaraka watoto wao kama sisi. Hawakuwa na wenyeviti wa chipukizi wala wa umoja wa vijana waliotoka viunoni mwao kama sisi.

Wakati kina Kawawa walikonda na kupandwa presha kuikomboa nchi hii, sisi tunaotesha viriba tumbo na kutononoka tukiifuja na kuangamiza. Wao walikuwa chachu sisi dumuzi wa maendeleo. Hawakufuga mafisadi-rejea kutaifisha mali za mabwenyenye na makabaila. Sisi tunagawana nyumba za umma na kufadhiliwa na maadui hao hao. Je hapa twaweza kujinakidi kuwa tunafanana na kuwaenzi akina Kawawa?

Panya hawawezi kumuenzi simba wagugunaye ngozi yake. Ni nani ana udhu na roho ya kumuenzi Kawawa miongoni mwetu. Nionyeshe mmoja nitakuonyesha panya elfu. Heri ya kutawaliwa na simba mmoja kuliko panya mia. Pumzika mahali pema kwa salama mzee wetu Rashid Mfaume Kawawa aka Simba wa Vita aka Charles Chaplin wa Tanzania na mkono wa kuume na mwanafunzi mtiifu aliyefuzu wa Mwalimu Nyerere.

Nenda kamwambie Mwalimu kuwa nchi yake sasa haipo tena bali jina. Hakika hatukuenzi Kawawa bali kukutumia na kukusanifu tu.
Chanzo: MwanaHALISI Januari 14,2009.

No comments: