Tuesday, 19 January 2010

Tafdhali rais, tangaza mali zako

MARA ya mwisho ikiwa ni ya tano kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutangaza mali zake ilikuwa ni kwenye gazeti hili Agosti 12, 2009.

Kwa hiyo, hii ni mara yangu ya sita kumtaka Kikwete atangaze mali zake, ukiachia mbali kumkumbushia pia kurejesha nyumba za umma alizoahidi kurejesha lakini asifanye hivyo.

Nina sababu kuu mbili

Mosi, ingawa ameshindwa kutekeleza ahadi zake zote alizotoa kwenye kampeni za 2005, anaweza kutimiza moja-kutangaza mali zake na za mkewe ambaye ni mwenyekiti wa NGO inayoingiza mabilioni ya shilingi ya WAMA.

Pili, ni baada ya kuona waziri wake mkuu Mizengo Pinda kukiuka mizengwe yote na kuamua kuweka hadharani ‘utajiri’ wake (kama kweli hakuna alichoficha. Nasema hivi kutokana na uzoefu na udhaifu wa sheria husika ukiachia mbali usanii).

Jambo hili licha ya kumuongezea heshima, ni suto kwa wale ambao hadi sasa hawataki kuweka wazi utajiri wao. Pia Pinda ametoa changamoto kwa rais ambaye ndiye bosi wake.

Amefanya kitu kilichomshinda bosi wake. Hili linahitaji ithibati na ujasiri wa hali ya juu. Maana kwa tawala zetu za kujuana, kufanya hivi kunaweza kumponza mhusika huko tuendako.

Ingawa watu wenye ufisadi wa kimawazo wamemuona Pinda kama hajafanya kitu chochote, kuna haja ya kumpongeza na kumpa moyo kuwa kazi aliyofanya si haba. Imewashinda wengi akiwamo bosi wake. Laiti wangemuuliza ni kwanini hakutaja za mkewe, kiasi fulani ingeingia akilini.

Kitu kingine kinachovutia kuhusiana na tukio hili la kupigiwa mfano, ni ile hali ha Pinda kuwa maskini kwa viwango vya wakwasi wetu. Huyu amejionyesha asivyo pale kutafuta mali bali kutumikia umma. Kwa vile tunataka watu waadilifu wasio na ulafi na ufichi, tuweke nukta hapa ili hapo baadaye atufae.

Hili likitokea, hata hivyo, litamjenga kisiasa hasa katika nchi ambamo watu waadilifu ni tone la mkojo baharini.

Wakati Rais wa Urusi, Dimitry Medvedev, alipotangaza azima yake ya kuweka wazi utajiri na mapato ya familia yake, ikiwa ni kuthibitisha dhamira yake safi ya kupambana na ufisadi, nilidhani Kikwete angefuatia. Lakini wapi? Kwanini? Ajuaye ni Kikwete mwenyewe.

Juzi juzi serikali ya Rwanda ilipowatimua watu kazi kutokana na kutotangaza mali zao, nilidhani Kikwete angetangaza mali zake.

Bila kutangaza mali kama sheria itakavyo, Kikwete ataendelea kuvutia mashambulizi mengi kuwa ni muhimili wa ufisadi licha ya yeye kuwa ni fisadi.

Pia atawapa kichwa wasaidizi wake mafisadi. Hawatatangaza mali zao. Maana jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani. Kikwete ni kama baba. Hawezi kuzuia watoto kutokunywa iwapo yeye analewa tena chakari.

Kuna wanaoona kuwa Kikwete anaogopa kutaja mali zake kutokana na kutokuwa na maelezo ya jinsi zilivyopatikana hasa ikichukuliwa kuwa alipotuhumiwa kwenye list of shame hakujitetea wala kutoa maelezo.

Hii maana yake ni kwamba kilichodaiwa na Dk. Wilbroad Slaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA kule Mwembe Yanga ni kweli tupu.

Je, kwanini Kikwete hataki kutaja mali zake? Je, alineemeka kwa namna yoyote na dili za awamu ya pili na tatu? Je, ni miongoni mwa waliopewa mgawo hata wa nyumba za umma zinazosemekana ziligawiwa kwa vigogo wa wakati ule ambapo naye alikuwa waziri na mjumbe wa baraza la mawaziri lililopitisha wizi huu?

Kuepuka kumzushia rais, tungemtaka atangaze mali zake na kutoa majibu ya baadhi ya maswali muhimu kama kipato chake na cha mkewe hasa ikichukuliwa kuwa kwa kuanzisha NGO kama ya Anna Mkapa aliyemchafua mumewe, anafanya biashara ikulu.

Hata hili la NGO nimeishaliandikia sana. Kwanini ianzishwe baada ya kuingia madarakani na kuona madudu ya EOTF? Tulioko nje tunaiona EOTF kama madudu. Kwa walio ndani ni ulaji wa dezo tena mkubwa.

Kikwete, kwa kukaa madarakani miaka mitano bila kutangaza mali zake, ilipaswa lichkuliwe kama kosa kubwa ambalo lingetosha kutorejea tena.

Maana hatujui aliingia na mali kiasi gani na kutoka na kiasi gani. Kwa maana nyingine ni kwamba amejenga mazingira yenye utata kuhusiana na uadilifu na uwezo wa kuongoza kwa mifano.

Iwapo Benjamin Mkapa aliingia na kutangaza mali zake lakini akatoka bila kutangaza anachukuliwa kama fisadi, inakuwaje kwa Kikwete na mkewe ambao hawakutaja wakati wakiingia? Na sasa wamebakiza miezi michache kuondoka.

Ingawa wanaosema Kikwete hapaswi kuongezewa muda wanaonekana kumchukia, mambo mengine Kikwete ajilaumu mwenyewe.

Huwezi kuhimiza watu watii sheria wakati wewe na familia yako mnaivunja wakati mlipaswa kuwa kioo kwa walio chini yenu.

Kama ni uongozi, huu ni mfano mzuri wa utawala mbovu usioheshimu sheria wala kanuni. Kama kutangaza mali imekuwa mbinde, je, itakapokuja kuitolea maelezo si tutakesha?

Ingawa Kikwete amekuwa akipuuzia miito mbali mbali kumtaka atangaze mali zake, ajue kitu kimoja. Watanzania wa sasa si wa jana. Wanaweza kumbwaga kwenye uchaguzi, kama uchaguzi utakuwa wa haki kama ilivyotokea nchi jirani ya Kenya.

Watu wamechoka na uongozi fisadi na fichi. Wanataka watu watakaowavusha toka kwenye bahari hii ya ubabaishaji na ufisadi. Na hakika hawa si wengine bali watakaoonyesha sura zao halisi kama alivyofanya Pinda.

Ingawa wapambe wa Kikwete wanajitahidi kutuhadaa kuwa ametenda mema, hakuna baya kama kuficha mali zako huku ukiwa msimamizi wa mali za umma.

Ingawa wanajipa moyo kuwa atashinda tena kwa kishindo kama ilivyotabiriwa na wapiga ramli na makuadi, mambo yanaweza kubadilika asiamini macho yake.

Maana imekuwa too much. Ameshindwa kutupeleka Kanani alipotuahidi. Anaweza kusingizia mtikisiko wa uchumi duniani ingawa si kweli zaidi ya matumizi mabovu na usimamizi mbovu, je, hata hili la kutangaza mali nalo limemshinda?

Sasa kama ameshindwa suala dogo lakini nyeti kama hili la kuthibitisha uadilifu wake, atatufaa kwa lipi huko tuendako ambapo ufisadi unazidi kupanda chati?

Tafadhali bwana rais, tuondolee kupiga ramli. Tangaza mali zako na za mkeo kabla ya kumaliza muhula huu.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 20,2010.

No comments: