How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 27 January 2010

Kilimo First au ulaji wa magabacholi kwanza?

“The zebra needs not pronounce on its zebritude. It simply stripes!” Kwamba pundamilia hapaswi kuonyesha upundamilia wake bali milia (mistari) Kwaku Sakyi-Addo Wole Soyinka, gwiji la fasihi naye anasema: “A tiger does not shout its tigritude, it acts.” Yaani duma hapigi kelele kuhusu uduma wake bali hutenda. Kumbuka huyu jamaa tumesoma chuo kimoja huko Maiduguri.

Nilikutana na mistari hiyo hapo juu nilipokuwa nikitafakari baadhi ya sera mpya za sasa yaani Kilimo First na utabiri wa mauti.

Mzee mzima nilikuwa kizani. Kabla ya magabacholi waliooiweka kaya mfukoni kuanza kuparurana sikuwa najua kilichokuwa kikiendelea kuhusiana na usanii wa kilimo first! Hapa ijulikane. Kilimo first ni tofauti na kilimo kwanza ya jamaa.

Eti wanasema ni msaada toka kwa serikali ya India. Msaada msahadaa? Kwa nini itulazimishe kutumia wahindi wezi kama si wizi? Mbona wajep wakitoa msaada hatuoni wajep kuja kusimamia msaada?

Je wajua: bila hawa magabacholi-nyemelezi kutaka kutoana roho huku wakiwaanika wabungwe uchi tusingejua ukweli? Si wewe si mimi tuliokuwa tukijua! Kumbe kilimo first ni sanaa tupu na ulaji wa magabacholi na mawaziili? Niulize kwanini?

Yako wapi matrekta zaidi ya kusikia vita ya kunguru ambayo ni neema kwa panzi wa Tanzia? Nani hajui kuwa lile dili la matrekta 1,000 lenye thamani ya madafu 50,000,000,000 limeanza kujulikana kuwa ni la makuadi wenye madaraka na magabacholi fisadi papa kama alivyosema mzee wa Nkuu na Nronga?

Sijui kama jamaa zangu wa Kimbushi, Nkwarungo, Kyarie, Kalali, Namikupa, nakapanya na Goweko wanajua hili. Sasa nawajulisha mchana kweupe; mwaliwa kama hamjui jueni mwaliwa ati!

Matrekta 1,000 ni kitu gani? Jembe la kukokotwa na mbuzi linatushinda tunadandia matrekta!

Mmefungwa kamba, kama mbuzi, mmeingia mkenge tena kichwa kichwa! Muambiwe mara ngapi kuwa adui yenu ni nyinyi wenyewe na ujinga na woga wenu ndiyo mtaji wa mafisadi hawa?

Jiulizeni. Nani awezaye kilimo usawa huu wa ubangaizaji, umachinga, ufisi, ufisadi, ubinafsi, ubinafsishaji na ukuushaji? Kwa nini wasiseme wazi umachinga, ufisadi na ubangaizaji kwanza? Hakuna haja ya kuona aibu kusema wakati unatenda hivyo.

Watu wanakwenda kwenye sinema za semina na wakiwashwa washwa na warsha wanarejea na mipesa tena bila kutoa jasho. Nani awekeze kwenye jembe? Mie naenda zangu Ngurdoto kwenye sinema elekezi narejea na minoti.

Kuna bomba mpya nimetoa hapa. Wasiojua maana ya ukuushaji nawasaidia. Ni ile hali ya mkuu wa kijiwe kumtumia Bi Mkubwa wake kutengeneza fweza kwa kuwatumieni wake zenu na mabinti yenu chini ya mradi sawa na wa bi mkubwa wangu wa MAWAWAWA.

Pia ni ile hali ya vitegemezi vyake kusimikwa kwenye ulaji mbali mbali iwe chamani au lisirikalini. Upo hapo mwanawakwa? Shauri yako!

Wenzenu wamewageuza mitaji nyie bado hamstuki! Ajabu kila siku mnaotea Kanani wakati mwendo uonyeshavyo mtaishia Sudan tena Darfur. Kalagabaho uuwiiii! Nilizeje muelewe kuwa mmekwisha wajameni? Anayedhani mie mbea ajiulize: tangu lini paka akamjali panya kama hamna namna? Na kwanini sasa tena wakati wa lala salama.

Huko nyuma walikuwa wapi na wanafanya nini zaidi ya kuhomola wakati nyinyi dhiki zikizidi kuwaponyoa mmoja baada ya mwingine? Mla mla leo kesho kala’ni?

Tuzidi kujidodosa. Hivi kweli katika karne hii ya ishirini na mosi nani anataka kulima iwapo hata maksai wakilazimishwa hugoma na kulia kama binadamu? Nani anataka trekta wakati hata baiskeli hana?

Mpe uone kama hatauza mataili ili kununua lau nyama ukiachia mbali kupeleka mtoto sekondari hata kuongeza kidosho kingine kutokana na bi mkubwa wake kuharibiwa na shida mlizotengeneza. Unadhani hawa ni wapumbavu kama mnavyowachukulia?

Tuseme ukweli hata kama unauma na kutusuta. Inataka roho ya mwendawazimu kuaminisha na kuaminishwa kuwa kitu kama hiki kinawezekana kwenye kaya ya wamachinga na mafisadi. Inataka wendawazimu acha roho yake kuamini ubangaizaji katika kila nyanja unaweza kuwavusha wachovu na walevi wa kaya hii.

Kwa nini kuvushwa na jembe ziliposhindwa almasi, dhahabu, chuma, tanzanite na madude mengine ya thamani? Kwanini msiyatoe kama mikopo kwa wafa na ngwamba lau waweze kutanua kama nyinyi?

Afadhali hizo bilioni mngewapa mawaziri wajengee mahekalu kama ya boss wa Bunch of Thieves (BoT) au yule mwenzie wa zamani wa shirika la migao ya umeme.

Juzi jamaa yangu mmoja alitoa mpya. Kwanza ieleweke. Jamaa mwenyewe fyatu kama Sofiii. Hivyo akisema jambo si vizuri kulipa uzito. Anavuta ndumu si mchezo!

Unajua alizozaje? Eti anasema ukiona hivi ujue mtaji wa kusakia ulaji kwenye uchafuzi wa uchaguzi mkuu wa kaya unatafutwa hivyo? Yeye bila hata woga anasema hii ni EPA nyingine ya mahepe!

Hayo tuyaache. Wanuka njaa na uchovu watajijua kama wataingia huu mkenge mbichi. Mie simo mwanawakwa!

Juzi nilisika watu wakipiga kelele kuwa wazee tung’atuke kwenye kijiwe. Hawa jamaa wapuuzi kweli. Eti wanasema tuwapishe vijana! Hebo huu ni ubaguzi. Kwa nini jamaa yenu mliyemchagua kuwa ni kijana amefanya nini cha mno ukimlinganisha na wazee kama Alhaj Ali?

Hata ukimlinganisha na mzee Moi Kibaki mzee wa Kikikuyu ana nafuu. Hazururi hovyo mzee wa watu wala mkewe ingawa ni mbabe hana MAWAWAWA kama huyu wenu.

Balaa lote hili lilianzishwa na bwana mazingaombwe mwenyewe alipotaka kuwafunga kamba na kuwatumia vijana asijue naye ni mzee. Yeye ana ujana gani? Hivi kweli kijana wa miaka 60 ni mzee au mzee wa miaka 60 ni kijana?

Tukiacha uvivu wa kufikiri, tutajua kuwa tatizo letu si uzee wala ujana bali uroho, roho mbaya, ufisadi na upofu uliojaa ubinafsi wa kupindukia. Tatizo letu ni mfumo mbovu usiorekebishwa siku nenda rudi.

Kwanza nani anataka kuitwa mzee usawa huu ambapo ukistaafu lazima ung’ang’anie mjini maana shamba kunatisha kwa ukapa na ukosefu wa usalama? Hujaona kila anayestaafu anaishia Bongo badala ya kwenda kwao Namikupa na Likawage kwa jamaa yangu Kimdunge Mwehu?

Ukiona vipi unaanzisha kampuni ya bi mkubwa anakwenda pale Ubung’o au Machinga Comp anafanya vitu vyake siku zinayeya. Lakini siyo kufikiri kulima ati!

Hata ndugu zangu wa Zaainzibaa wanafikiria kuwa Hong Kong kama alivyowahadaa jamaa wa Madevu aliyepata kichaa cha Karumekenge. Hong Kong hawalimi ati. Kilimo ni mambo ya kizamani sana. Hii ni karne ya sayansi na teke linalokuijia. Kilimo tuliwaachia akina Adam na Eva ambao nao walikiona noma wakaamua kuvamia mti wa kati kati ya bustani.

Ila jamaa zangu nao wajue. Hong Kong haiji kwa kuvunja katiba na kuhadaiana kama nionavyo sasa ambapo ndoa ya mkeka inazidi kupanda chati huku jamaa zangu wakiingia mkenge kichwa kichwa!

Nani atahangaika na kilimo iwapo biashara kama vile ya bangi, uchuuzi, udokozi na jinai nyingine inalipa haraka? Mie nimeamua kuanzisha dhehebu langu la dini ili kuepuka kilimo. Mke wangu naye ameanzisha kampuni ya kukusanya ushuru na Ngo ya kupigania haki za wanawake.

Tukikusanya pamoja mambo yanakwenda ati ukiachia mbali zile ninazoponyoa kwenye kijiwe.

Hakuna atakayejiingiza kwenye kifo cha jembe wakati kupiga soga maofisini kunalipa. Kama wapo basi ni wale ambao hawana pa kwenda wala kamba za kuifungia jamii na kusavaivu.

Naona jamaa wanakuja kuhutubia kuhusu kilimo first. Acha nijikate nifikiri jinsi ya kuwatoa takrima hawa wanaokuja kunibamiza mkenge. Salamu kwa Pio Msekua. Bwana we lipa njuluku za watu na ueleze kitegemezi chako kilivyopata ulaji kwenye ubalozi.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 27, 2010.

No comments: