The Chant of Savant

Wednesday 27 January 2010

Hili la Msekwa ni aina nyingine ya ufisadi


SAKATA la Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), Pius Msekwa, kudaiwa takriban shilingi 7,000,000 alizokopa ubalozini Uingereza, limetufumbua macho.

Msekwa alikopa pesa tajwa ili aweze kumtibia mwanae aitwaye Julius aliyeugua ghafla akiwa njiani kwenda Paris Ufaransa akiwa ni mfanyakazi wa ubalozi.

Ukichukulia na kugundulika kuwa watoto wengi wa vigogo wa chama na serikali wamejazana Benki Kuu (BoT) tena wengine kwa kuingia na vyeti vya kughushi, hili linazidisha shaka.

Hebu fikiria, Msekwa huyu huyu alikuwa Spika wa Bunge kwa miaka nenda rudi kabla ya kuteuliwa Makamu Mwenyekiti wa CCM. Zidi kufikiri. Msekwa huyu huyu mwanaye anafanya kazi ubalozini.

Bado hajaridhika na neema zote hizi anazokamua kwenye nchi. Msekwa huyu huyu anakopa pesa ubalozini. Mwisho wa yote anaacha kulipa? Je, huu si ufisadi na ubinafsi wa kutisha? Je, ni wangapi kama Msekwa madudu yao hayajajulikana?

Ingawa huu mara nyingine huchukuliwa kama umbea, utakuta kuna ukweli hasa kuhusiana na watawala wetu kujipendelea wao na familia zao.

Nenda pale Ikulu. Alipoingia Benjamin Mkapa tulianza kusikia baadhi ya majina yakitajwa. Kwa sasa hatujui wapo kina nani. Ila uhakika ni kwamba kuna watoto wa vigogo ama wa chama au serikali.

Je, balozi zetu zina watoto wangapi wa watu kama kina Msekwa? Je, wamepelekwa kule kwa vile wana sifa au ni kwa vile wazazi wao ni vigogo?

Hivi karibuni nchini Kenya kuligunduliwa kitu cha kutisha ambapo mabalozi na baadhi ya wafanyakazi ni ndugu wa vigogo. Walitajwa mabalozi Dk. Wenwa Akinyi (USA) dada yake Waziri Mkuu, Raila Odinga; Bi Catherine Muigai Mwangi (Jamhuri ya Ireland) ambaye ni dadake Waziri wa Afya, Bi Beth Mugo, ambaye pia aliwahi kuwa mkurugenzi wa tume ya mawasiliano wa Kenya Airways.

Bi Mishi Masika Mwatsahu ambaye muda wake kuwa balozi nchini Pakstan umerefushwa ni dadake Waziri wa Uchukuzi, Chirau Ali Mwakwere.

Wakati huo huo mwakilishi wa kudumu wa UNESCO, Dk. Mary Khimulu, ni dadake Waziri wa Ushirika, Joseph Nyagah. Huyu aliteuliwa mara ya kwanza wakati kaka yake alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje.

Profesa Sospeter Machage (Urusi) ni pacha wa Waziri Wilfred Machage. Kabla ya kuteuliwa alikuwa akiendesha hospitali binafsi kwenye mji mdogo wa Kilgoris.

Mwingine ni Elkanah Odembo (Ufaransa) ambaye shemeji yake ni Chief Whip wa serikali, Jakoyo Midiwo.

Kwa vile sura za ufisadi barani Afrika zinafanana, kuna haja ya Watanzania kuanza kuchunguza mabalozi wetu nje hata wafanyakazi wa ubalozi nje kujua kuna kina “Msekwa, Sons & daughters” wangapi.

Hapa tunaongelea balozi zetu nje. Bado kuna sehemu nyingine nyeti kama uhamiaji, bandari, wizarani, mbuga za wanyama na sehemu nyingine zenye vipato vikubwa.

Hapa bado hujamulika makampuni binafsi ya vigogo yanayofanya shughuli za kibiashara na serikali hiyo hiyo wanayotumikia. Rejea sakata la miraba ya uwindaji na kumilikiwa na mawaziri na wazito wengine serikalini au washirika, wake na marafiki zao.

Rejea kashfa inayozidi kusukumizwa chini ya busati ya wizi wa mapato pale Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo ambapo wizi umehamishiwa Machinga Complex.

Je, kwa mtaji huu nchi haijawa mali ya vigogo wanaotuaminisha kinadharia kuwa ni yetu wakati kivitendo ni yao?

Je, pesa aliyokaa nayo Msekwa kwa muda aliokaa nayo ingekuwa benki ingezalisha faida kiasi gani? Je ni wangapi wamekopa pesa kubwa kuliko hii kwa miaka mingi kama ilivyobainika kwenye ufisadi wa CIS hadi leo hawajalipa wala kuchukuliwa hatua?

Je ni wangapi wamepeleka watoto, marafiki hata ndugu zao kusoma nje kwa pesa za umma ambao hatuwajui kwa vile wanalindana serikalini?

Kwa nchi za Magharibi zinazotupa misaada, kitendo cha Msekwa kilitosha kumwajibisha na chama chake kuingia tafrani kwenye uchaguzi ujao. Lakini kwa vile Tanzania ni shamba la bibi la mafisadi, hakuna anayeliona hivi.


Achia hili la Msekwa, Mawaziri na wabunge waliotuhumiwa kughushi vyeti vya taaluma wamechukuliwa hatua gani zaidi ya kuendelea kupeta wakati ni matapeli wa kawaida tu? Je, rais hata umma unaowavumilia wahalifu kama hawa si wa wahalifu na mafisadi pia?

Leo watu kama Profesa Mwesiga Baregu wananyimwa ajira wakati kuna matapeli walioghushi wako kwenye nyadhifa za juu wakilipwa vinono kwa ujuzi wasio kuwa nao!

Kama kuna maafa yanayoikumba Tanzania si mengine ni haya. Maana hawa wanalipwa pesa nyingi na kutumiwa na wezi wanaoitwa wawekezaji kwa kujua hawajui lolote kiasi cha taifa letu kuendelea kuwa maskini wakati lina raslimali nyingi.

Mawaziri vihiyo au walioko madarakani kwa udugu ndio chanzo cha mikataba michafu kama ya TRL, IPTL na mingine inayolisumbua taifa. Nani atamwajibisha nani kwa mfano mtu anayeshutumiwa kutenda kosa ni shemeji au kaka hata dada wa anayepaswa kumwajibisha?
Chanzo: Tanzania Daima Januari 27, 2010.

No comments: