Katibu mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa.
ALIPOKUJA na orodha ya walioitwa "watafuna nchi," ambayo iliwaacha uchi karibu vigogo wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wenye akili walitia akilini.
CCM ambao ni watuhumiwa wakuu, kama kawaida yao, walisema Dk. Willibrod Slaa ni mwongo na mnafiki. Lakini kadri siku zilivyokwenda na mambo kuwekwa hadharani, wanafiki, waongo, wababaishaji, wezi na mafisadi walijulikana.
Huyo si mwingine bali shujaa wa kupambana na kufichua ufisadi, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Slaa.
Sasa baada ya Dk. Slaa kuipua madai mapya ya CCM kukwepa kulipa kodi kwenye ununuzi wa magari, haraka ikajengwa ngome na kukanusha na kutishia kumfikisha mahakamani.
Yako wapi sasa? CCM wameona huu ni mwiba mwingine mkubwa na mkali. Wamefyata na kuanza kupingana hadharani hovyohovyo kama njia ya kukwepa kuwajibishwa.
Mwanzo aliposema kuna ujambazi benki kuu kwenye fuko la madeni ya nje (EPA), unaowahusisha wakubwa wa serikali ya sasa na iliyopita, CCM na serikali yake walimwita mwongo na mbea mkubwa. Ilipothibitika walifyata.
Hivi sasa wananchi wengi wanaamini kuwa serikali ya sasa ama ni tunda la ufisadi wa EPA au kimelea chake. Nani apinge au kujibu wakati ukweli uko hadharani?
Rais Kikwete alikuwa kwenye orodha ya aibu ya “watafuna nchi.” Hakujibu. Angejibu nini wakati kila kilichosemwa na Slaa kilikuwa ukweli ambao hauwezi kukanushwa.
Kuna wapumbavu na mafisadi waliosema eti Kikwete na CCM wakimjibu Slaa itakuwa sawa na mtu kuvuliwa nguo na mwehu halafu akaanza kukimbizana naye.
Pamoja na usemi huu kuwa mfu, unathibitisha jinsi gani nchi ilivyojaa vihiyo na waroho wasio na hata ubongo. Hata ndege wanajua kuwa Tanzania imo msambweni.
Nguvu ya ufisadi imemeza utu, uongozi, busara hata akili. Wananchi sasa wanajua kuwa nchi ina ombwe la uongozi na watawala wetu ni walafi na wachafu; wanaoweza kula kwa mikono na miguu, tena bila kunawa.
Katika suala la hivi karibuni sikiliza viongozi wanavyoumana. Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, John Chiligati alisema Dk. Slaa atafikishwa mahakamani.
Siku mbili baadaye Amos Makala anasema hakuna kitu kama hicho. Alikaririwa akisema, “Mimi ninayezungumza hapa ni Katibu wa Fedha na Uchumi. Ndiye mwenye dhamana ya kuzungumzia suala hili kwa niaba ya CCM.” Aibu.
Chiligati na Makala wana ofisi pale makao makuu madogo ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam; lakini kutokana na kuchanganywa na kashfa tajwa, walishindwa hata kuwa na msimamo wa pamoja. Je, chama kama hiki kinaweza kuivusha Tanzania?
Hakika CCM haina ubavu wa kumshitaki Slaa. Ikifanya hivyo itakuwa inashitaki wananchi na wataivua nguo zaidi na zaidi. Muhimu ni wananchi kutia akilini. Wakati ukifika watoe hukumu mujarabu.
Chanzo: MwanaHALISI Desemba 30, 2009.
No comments:
Post a Comment