The Chant of Savant

Thursday 31 December 2009

Umma ufanye maamuzi sahihi

Useme: "Tumechoka kukumbatia wezi"
Nyumba ya Gavana wa Benki kuu ya Tanzania(BoT) inayodaiwa kulamba Shs. 1,400,000,000!

PROFESA wa Sheria, Issa Shivji, amesema "ufisadi umeshika kasi." Hivi ndivyo imedhihirika leo, kwamba ni jambo la kawaida kwa serikali na taasisi zake kutumia mabilioni ya shilingi za umma kwa mambo ambayo hayana maslahi kwa taifa na watu wake.

Mara ya kwanza kusikia nyumba ya serikali inakarabatiwa kwa Sh. 1 bilioni – si kujengwa – ilikuwa kwenye sakata la Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Sasa kuna hili la nyumba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu.Taarifa za kwanza zimesema imekarabatiwa kwa Sh.1 bilioni.

Rais mstaafu Benjamin Mkapa alipokarabati ikulu yake, wakati ule, kwa Sh. 3 bilioni (kama tulivyoambiwa), “tulipagawa” na kupiga kelele. Sasa hayawi hayawi yamekuwa.

“Ujasiri” huu unatoka wapi katikati ya bahari ya ufukara? Tunaambiwa nyumba ilinunuliwa kwa Sh 500,000,000 na sasa inakarabatiwa kwa Sh. 1 bilioni; katika nchi ambayo ardhi si haba na wala haijapanda bei kiasi hicho.

Tokyo na Dubai ni miongoni mwa miji ghali duniani kwa mtu kununua kiwanja. Lakini kwa bei hii, ikilinganishwa na hali halisi ya soko la viwanja na majumba nchini mwetu, basi Dar es Salaam ni ghali kuliko hata miji mikubwa na ghali sana duniani.

Kitendo hiki kinatukumbusha kisa cha hivi karibuni nchini Zambia ambako bila aibu, serikali ilitumia dola 13 bilioni kushughulikia kesi ya wizi wa dola 500,000 iliyokuwa ikimkabili rais mstaafu Frederick Chiluba.

Kuna swali jingine: Kwanini gharama ya kukarabati nyumba iwe kubwa kuliko ya kununulia? Lakini leo Gavana wa BoT anasema siyo kukarabati. Anasema nyumba imejengwa kutoka kwenye msingi. Anaongeza kuwa gharama inaweza kuwa kubwa kuliko hii ambayo imetustua. Tafadhali sana Bwana Gavana!

Vyovyote itakavyokuwa, wanaoishi kwenye mahekalu haya ni watoto wa maskini wa kunuka ambao kama si Mwalimu Nyerere kuwasomesha bure, huenda wengi wangekuwa vibaka.

Je, fedha hii takribani Sh. 1 .5 bilioni zingewezesha kujengwa kwa shule au zahanati ngapi kama tungekuwa na watendaji wasiopenda makuu?

Kwanza, ilinunuliwa toka kwa nani? Isije ikawa ni kati ya zile zilioibwa wakati wa utawala wa Mkapa au ya kigogo wa benki au hata serikali.

Inakuwaje BoT iliyoanzishwa zaidi ya miaka 40 iliyopita haimiliki nyumba yake kwa ajili ya kuishi gavana wake? Au ni kweli kwamba nyumba ya awali ambayo alikuwa anaishi Dk. Idrissa Rashid au Dk. Daudi Ballali imeshanunuliwa?

Je, ni mashirika mangapi ya umma yana tabia chafu kama hii? Je, kwanini tusiangalie upya maslahi na marupurupu ya wakuu wa BoT ili kuepuka kurudiwa kwa upuuzi kama huu?

Kama fedha hizi zingetumika vizuri, zingeweza kufanya mambo ya maana. Tunaambiwa kukarabati barabara yenye urefu wa kilometa 65 ya Tanga hadi Horohoro ni Sh. 70 bilioni. Hii maana yake ni kwamba tunakarabati nyumba moja kwa sehemu moja ya sabini ya gharama ya barabara.

Je, huyu kiumbe anayeshi kwenye hekalu ghali kama hili anatumia fedha za umma kiasi gani kwa mwezi? Anaendeshwa kwenye gari la aina gani? Thamani yake ni kiasi gani? Je, anachotumia na anachozalisha kinawiana?

Hivi karibuni nchini Kenya kuligundulika wizi wa ajabu ambapo watu 65 walikunywa maji ya zaidi ya Sh. 25 milioni za Tanzania kwa wiki moja tu. Ulafi wa viwango vilivyowahi kuitwa “ufisadi mchafu.”

Gazeti la Mwananchi liliandika kuwa gavana wa sasa anadaiwa kukataa kuishi kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mtangulizi wake kutokana na kutokuwa na bwawa la kuogelea (!) Akili ya aina hii inasaidiaje vijana wetu wanaotafuta elimu?

Siku zote tumesema serikali yetu na taasisi zake ndio chanzo cha maafa yetu. Tunaongelea nyumba moja ya gavana. Bado magari anayotumia, wakubwa wenzake na wasaidizi wao.

Hapa hujamgusa bosi wake yaani rais, ukiachia chama chake ambacho sasa kimekiri kutumia fedha chafu wakati wa uchaguzi mkuu na sasa kimeapa kuwa hakitatumia tena fedha chafu.

Hili la ukarabati wa nyumba ya gavana si dogo. Kwani gharama zake ni kubwa kuliko hata zile za uchaguzi mdogo wa Tunduru ambako iliripotiwa kuwa zimetumika Sh. 243,126,860; angalau kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kwa kiasi hiki, bado gharama ya kukarabati nyumba ya gavana au hata kujenga, ni kubwa kuliko gharama za chaguzi ndogo za Mbeya, Tunduru na Busanda kwa pamoja. Huu ni ufisadi hata yangetolewa majibu na sababu za namna gani.

Wakati upuuzi huu ukiendelea, ile serikali iliyoahidi maisha bora kwa Watanzania inazidi kufumba macho kana kwamba hili si janga.

Ukijumlisha mabilioni ya shilingi za umma ambazo zimekwapuliwa katika kipindi tangu 2004, utaona kuwa sisi (nchi) ni matajiri, tatizo ni ukosefu wa akili timamu kwa umma na utawala wao.

Hata wale wanaotufadhili hawawezi kuishi maisha ya kifujaji kama haya. Mwaka 2007, waziri mmoja kwenye jimbo la Newfoundland and Labrador nchini Canada alifukuzwa uwaziri, ubunge na kufungwa miaka miwili gerezani kwa kosa la kutumia vibaya dola za Canada 117,000.

Ukilinganisha kiasi hiki cha fedha (dola 117,000) na utajiri wa Canada, ni sawa na shilingi mbili tu. Lakini waziri alikabiliwa kikweli na kufukuzwa na kufungwa.

Tanzania hali ikoje? Andrew Chenge na Dk. Idriss Rashid wanashutumiwa kuficha mabilioni ya shilingi, lakini hakuna anayewashughulikia zaidi ya serikali kuzidi kuwateua kwenye nafasi za uongozi wa umma.

Wananchi wanaambiwa wafunge mikanda wakati watawala wanavua mikanda kutokana na kuwa na matumbo makubwa kuliko mikanda ya kawaida.

Hii ndiyo maana serikali imeridhia wajanja wachache pale BoT, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Bandari la Taifa (PTA), Ikulu na kwingineko wanufaike na taifa liangamie.

Tanzania ni taifa lisilo na roho wala aibu. Maana tungekuwa na roho tungeona aibu kuzidiwa na nchi kama Rwanda na Uganda au Kenya ambazo raslimali zake kwa pamoja hazifikii hata nusu ya zile zilizopo kwetu.

Tungekuwa na viongozi wenye ubinadamu, japo kwa tone moja, basi wangeona aibu na kubadilika. Lakini wapi! Kibaya zaidi, ni hawa wanaotuibia usiku na kutuhubiri mchana kuwa tuwachague tena ili wakamilishe kile wanachoita, “kuleta maendeleo.”

Hatuwezi kupata matumaini wala ahueni, bila kufanya maamuzi sahihi: Kuiambia serikali kwa sauti kubwa kwamba, “Tumechoka kukumbatia wezi.”
Chanzo: MwanaHALISI Desemba 30, 2009.

No comments: