Friday, 25 December 2009

Ni homa ya ufisadi si Lowassa

MAKALA ya rafiki, ndugu na mhariri na mpambanaji mwenzangu, Absalom Kibanda iliyobeba kichwa cha ‘Taifa linaugua homa ya Lowassa” toleo la Desemba 9, mwaka huu, haiwezi kupita bila kudurusiwa.

Baada ya kusoma makala tajwa kama mara mbili nikiwa nimechanganyikiwa na kusema ukweli nimeimaliza bila kuielewa vilivyo, niliwasiliana na Kibanda ambaye alinipa ufafanuzi wa kina ila si utetezi. Maana nilishaanza kumwekea alama ya kuuliza kuwa anatumiwa na mafisadi kama wale waliotumiwa kuisafisha Richmond. Kina Salva Rweyemamu na Gideon Shoo walianza hivi.

Baada ya kujiridhisha kuwa nimeielewa, nimeamua kuidurusu-kuiongezea nyama. Je lengo la Kibanda lilikuwa nini haswa?

Ingawa amemtumia Lowassa kutokana na kuvutia vyombo vya habari na mijadala, kimsingi alichomaanisha ni homa ya ufisadi na umma kutoa haki-mnyonge mnyongeni, haki yake mpe. Lowassa ana mema. Alisahau. Baya moja hufuta mema mia. Lowassa hata hakuwa akifikisha mema saba!

Japo ni haki Kibanda kuamini atakavyo, kimsingi, anayepaswa kumlenga si Lowassa bali Jakaya Kikwete na mitandao yake. Kwani lao moja.

Kwa kujadili mitandao, tutaepuka mtego wa kujadili watu japo wakati mwingine hili halikwepeki. Lowassa hana dola mikononi ingawa kuna maneno kuwa ana mpango wa kulisaka.

Kusaka urais ni haki yake kama Mtanzania yeyote ili mradi awe na udhu, ubavu, sera na baraka za wapiga kura ingawa ukweli ni kwamba ‘it is too late or next to never.’ Je, yawezekana kwa mwanadamu kumfufua maiti?

Je, kweli Watanzania wanamgwaya na kumhukumu vibaya Lowassa? Hakika, Lowassa kama binadamu na mwanasiasa yeyote, hachukiwi bali historia, hulka na matendo yake.

Lowassa si mwanasiasa mbaya kama angekuwa ametulia na ana chembe ya uadilifu. Hata hivyo, ameishaachwa na fursa.

Lowassa asingegeuka kitendawili kiasi cha kuzua mjadala kwa muda mrefu kama angeamua kujitetea na si kukaa kimya tena mara mbili. Mara ya kwanza ni pale alipozuiliwa na marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995 alipotaka kugombea urais. Nyerere hakufumba.

Alibainisha wazi kuwa Lowassa alikuwa na mali nyingi ambazo asigeweza kuzitolea maelezo. Na huu ni ukweli.

Kwanza rejea kimya cha Lowassa na maneno ya hivi karibuni ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Sophia Simba, kuwa Lowassa anaonewa wivu kutokana na kuchuma zamani. Kama ada, sawa na rafiki yake Jakaya Kikwete, hakukanusha wala kujitetea.

Mara ya pili ni pale alipohusishwa na kashfa iliyomgharimu ya Richmond ambayo kimsingi si yake bali ya Rostam Aziz na Ibrahim Msabaha ambao hata hivyo hatuwajadili na kushinikiza wafikishwe mbele ya sheria vilivyo.

Kadhalika, hakukanusha wala kujitetea. Je mtu wa namna hii utamwelewaje? Hata mahakamani ukifikishwa ukashindwa kujitetea, hakimu huwa anakata hukumu chini ya dhana ya ‘admission’.

Ingawa Lowassa si mhusika mkuu kwa sasa hata kama yuko nyuma ya pazia, ana kila sababu ya kuhofiwa (lakini si kwa kiasi hicho) kutokana na kushiriki kumtengeneza mhusika mkuu kwa kumpa mbinu chafu zilizotuingiza kwenye kadhia na mateso tuliyomo-mitandao ya kifisadi na kijambazi ya kusaka madaraka.

Tukiachia mbali na kumjadili mtu, Kibanda alinichokoza aliposema Watanzania tumelogwa. Naweza kukubaliana na kutokubaliana naye. Tutathibitisha kulogwa kama tutarudia makosa kwa kuendelea kumfadhili nyoka kwenye debe la unga ili ale anenepe na kuzidi kutudonoa.

Naungana na Kibanda kuwa tatizo si Lowassa ingawa hakusema wazi hivi. Tatizo ni sisi. Tatizo ni CCM. Tatizo ni katiba; tume ya uchaguzi na mkururo mzima wa utoaji haki na utawala.

Kwa vile tunafanyiwa upuuzi tena kwa miaka mitano halafu tunarudia upuuzi ule ule-kuwachagua walioshindwa dhahiri. Ila ieleweke. Tatizo si kulogwa. Tatizo ni ujinga, ubinafsi, nyongea na ‘myopia’. Ni utapiamlo wa kimawazo bila kusahau ufisadi wa kiroho ambao umejenga tabaka ya watu panya wanaotanguliza matumbo badala ya vichwa.

Tunawaabudu wenye nazo hata kama wameziiba kwetu. Tubadilike na si kuamini tumelogwa. Hatujalogwa bali tunazidiwa ujanja.

Kwa sasa tumepotoshwa na kunaswa kwenye mtego wa mafisadi. Badala ya kumjadili na kumkabili mhusika mkuu-Kikwete na genge lake, tunamuandama Lowassa ambaye kutaka kwake urais ni fununu tu zisizo na msingi kwa sasa.

Tunatumia bunduki kummalizia inzi. Kwa nini tusimngoje wakati muafaka baada ya kumalizana na huyu pacha wake?

Ingekuwa kujadili watu ni tija, ningemjadili hata mke wa Kikwete kuhusiana utumiaji wa NGO yake kuliko Lowassa ambaye ‘kazi kwisha’ kwa sasa.

Ninukuu mzizi mkuu wa hoja ya Kibanda kama nilimwelewa vizuri, “Ni wazi kwamba wakati alipotangaza kujiuzulu uwaziri mkuu Februari, mwaka jana, wanasiasa wengi wa ndani ya CCM na wale wa nje ambao kwa namna moja walikuwa na hasira nyingi dhidi ya Lowassa kutokana na staili yake ya utendaji kazi wa serikali, uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia uwaziri, ukuu wa mikoa, wilaya, ubalozi na hata ushindi wa zabuni mbalimbali serikalini waliliona tukio hilo kuwa lilikuwa likibeba neema kubwa na ufumbuzi wa vikwazo mbalimbali vilivyokuwa vikiwasibu.”

Hapa Lowassa hakuchukiwa kama Lowassa bali waziri mkuu na mtendaji mkuu dhaifu na asiye mwaminifu kwa rais dhaifu na asiye mwadilifu.

Kama uteuzi na utendaji wake vilikuwa kero na hasara kwa umma wa kumlaumu si Lowassa bali yule aliyemwakilisha.

Maana wananchi hawakumchagua na kumwapisha Lowassa. Hivyo, kuendelea kumwacha madarakani aliyechaguliwa ni ushahidi kuwa alikuwa akiridhika na vitendo na namna yake ya kufanya mambo hata kama ni kwa kuvunja sheria, kukurupuka na kujihudumia kama ilivyobainika kwenye kashfa tajwa. Matendo ya Lowassa yalikuwa na mhuri na baraka za rais. Kosa lake ni kutumiwa hapa.

Kadhalika hapa aliyepaswa kuhamanika si wanasiasa kama anavyosema Kibanda, bali Watanzania ambao mpaka ninapoandika, wanaendelea kuteswa na upuuzi huu utokanao na utawala mbovu wa kishikaji na kifisadi.

Na ikumbukwe hapa ndipo taifa linaugua homa ya ufisadi itokanayo na watawala wabovu kama Lowassa na bosi wake. Hapa tatizo si Lowassa wala Kikwete bali mfumo mbovu kuanzia uchaguzi uliowezeshwa na takrima na pesa ya EPA, katiba mbovu na yote katika yote, wapiga kura waroho na vipofu ambao kama hawatasikia watarudia upuuzi uleule kwa mateso yao baadaye.

Kama tutaendelea na upogo wa kumhofia Lowassa na si Kikwete na genge lake, basi tutaangamia. Na hakika kati ya makala ambazo wawili hawa wamezipenda ya Kibanda ni mojawapo.

Kwani, kwa kufumba, kulenga kusiko na kuficha lengo halisi kuwa ilikuwa ni kuuamsha umma umkabili mhusika wa kweli badala ya huyu ambaye mambo yake kwisha, amewasaidia kukwepa patilizi na umma-athirika.

Hapa ndipo ninapomtwisha lawama Kibanda kiasi cha kuonekana kama anatumika au ana mpango wa kufanya hivyo. Najua Kibanda kwa kuwepo nchini na jikoni (mhariri), anajua mambo mengi ama kwa kuona, kuambiwa na hata kushawishiwa kutokana na nafasi yake.

Nisingetaka kumfundisha kazi Kibanda; ila ni vizuri akajua kuwa kufumba sana kunaweza kuuchanganya umma ikizingatiwa kuwa si wasomaji wote ni wachambuzi au wana fani.

Badala ya kumuandama Lowassa, tumuandame pacha wake ambaye ndiye aliyeshikilia madaraka yetu.

Ni taasisi ya urais. Tumtumie Lowassa kama rejea pale inapobidi. Vinginevyo homa tunayougua si Lowassa bali ufisadi na ujambazi wa kisiasa ambavyo muhimili wake ni ukimya wa rais kutokana na ushiriki wake nyuma ya pazia.

Hapa ndipo nilipowahi kuibua dhana nzima ya ‘Ukwete’ ingawa watawala hawakuipenda. Tumtathmini rais na kutafakari kauli na matendo yake bila kusahau wale aliojizungushia. Tutake atupe hoja na sababu za kufika hapa tulipo tofauti na tulivyoahidiwa.

Tumkabe na kumsonga kumuonyesha kuwa hii nchi ni yetu na madaraka yake ni jambo la mpito. Tusimpe nafasi ya kutuingiza mkenge tena.

Tumnyang’anye mamlaka yetu tuwape wanaofaa kama walivyopendekeza hivi karibuni wakongwe wa chama chake.

Nafasi haitoshi. Taifa linaugua homa ya ufisadi. Ila kuna dawa. Dawa ni kutochagua mafisadi hata wajiletelete na ahadi lukuki vipi.

Tuwaulize. Miaka mitano mlifanya nini zaidi ya kulindana? Kama mmeshindwa kipindi cha kwanza lala salama si mtatumaliza kwa vile hamtakuwa na haja ya kugombea tena?

Chanzo:Tanzania Daima Desemba 23, 2009.

No comments: