Friday, 11 December 2009

Makamba, kati ya mwehu na mtumwa yupi bora?

MANENO makali kuwa wanaompinga Rais Jakaya Kikwete kugombea muhula wa pili ni wehu kama alivyodai Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, hayawezi kupita bila kudurusiwa.

Baada ya vyombo vya habari kumkariri waziri wa zamani katika utawala wa awamu ya tatu, Mateo Qares, akiwataka CCM wamtose mwenyekiti wao, Kikwete kutokana na kushindwa kuchukua maamuzi mazito dhidi ya ufisadi, Makamba alijitosa kumtetea bosi wake bila mafanikio.

Makamba alijivua nguo kwa kutumia jazba badala ya busara kiasi cha kuharibu mambo akidhani anajibu. Makamba alionyesha dhahiri kujikomba hasa baada ya Rais Kikwete kupuuzia wito wa kutaka ampumzishe kutokana na kupwaya kwenye cheo chake.

Dhambi ya Qares ni kusema maneno haya: “Ninayemzungumzia sasa kwamba achukue maamuzi magumu si mwingine, ni Rais wa Jamhuri ya Muungano.”

Qares aliongeza: “Anaweza kuchukua maamuzi magumu kwa kufumba macho na kuwashughulikia hao wanaosema hakujuana nao barabarani, kwa kupitisha wino mwekundu akawa rais mzuri tu. Lakini kama atashindwa, basi ashauriwe miaka yake mitano inamtosha.”

Laiti maneno haya yangesemwa na wapinzani au wachambuzi, ungesikia kejeli na nyodo kibao. Sasa kuchele! Yanasemwa na wana CCM tena vigogo.

Japo wengi wameshauri mara nyingi rais Kikwete awajibishwe kwa njia moja au nyingine na umma umekaa kimya, hali ilivyo, umma utaanza kuamka na kusikiliza sauti hizi za wenye busara ambao kwa Makamba ni wehu. Je, mwehu hapa ni nani? Jibu unalo.

Hata hivyo, tusimshangae Makamba. Anatetea kitumbua chake ila kwa njia ya hovyo. Inasikitisha Makamba kuwaandama wanaotoa ushauri mzuri huku akiwakumbatia mafisadi wanaojulikana fika kama alivyosema hivi karibuni Qares.

Qares hakukurupuka wala kubabaisha. Alikaririwa akisema maneno haya: “Siku moja niliwahi kumuuliza (katibu mkuu wa CCM, Yusuf) Makamba kwanini matajiri wachafu ndani ya chama wasing'oke, akanijibu sasa wewe unataka matajiri waende chama gani?”

Watu wenye akili nzuri, wangetaka Makamba ambaye si “mwehu” akanushe madai haya yanayomvua nguo na kumwonyesha kama kibaraka wa mafisadi.

Hii si mara ya kwanza Makamba kuonyesha anavyoshabikia ufisadi. Nani amesahau alivyokuwa akihamanika kumpigia debe mwajina wake Yusuf Manji ili agombee kule Kigamboni ambapo hata hivyo alitoka kapa?

Hebu angalia majibu ya Makamba: “ Mtu mwenye akili nzuri hawezi kusema kwamba Rais Kikwete ameshindwa kutekeleza wajibu wake. Anayefikiria hivyo, ni mwehu.”

Hivi hapa mwehu ni nani kati ya aneyeongopa mchana na anayesema ukweli? Ama kweli nyani haoni ‘nonihino’ lake! Ajabu Makamba anasema yuko tayari kufungwa kwa ajili ya kumtetea (kujikomba kwa) Kikwete! Hajui sheria huyu.

Nani akufunge kwa kujidhalilisha mwenyewe? Pia anasema tuheshimu wenye madaraka kwa mujibu wa Biblia na Quran. Si kweli. Mbona Yesu aliwapinga akina Kaisari na Muhammad kuwapinga watemi wa Makureishi. Si kila mamlaka zatoka kwa Mungu. Nyingine hutoka kwa shetani hasa zile fisadi.

Je, kweli, wehu ni nani kati ya Qares, Joseph Butiku, Juma Nkhangaa Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim, Mhashamu Methodius Kilaini, Askofu Mkuu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na wote wanaoona udhaifu wa Kikwete na wale wasioona kwa vile wamepofushwa na fedha chafu za mafisadi kiasi cha kuwa watumwa wa hiari?

Wengi tumemshauri Kikwete mara nyingi amtimue Makamba. Kwani kuwamo kwenye safu za juu za chama kumezidi kukidhoofisha kutokana na kauli zake na kupenda kuchukulia mambo mazito kama mepesi.

Hata hivyo, hili hatumlaumu yeye kutokana na kiwango chake cha uelewa na umri wake. Hapa, kwa mara nyingine, wa kumlaumu ni Kikwete ambaye amekuwa mpole kuliko hata njiwa.

Ila mwisho wa siku ajue, hawa mafisadi anaowabeba na kuwakingia kifua watammaliza. Aachane na mapenzi ya mshumaa.

Wengine wanasema Kikwete hana mapenzi yoyote na yeyote isipokuwa nafsi yake. Hapa ndipo wale aliowataja Qares kuwa wanasema hawakukutana na Kikwete barabarani.

Wapo wanaoona: Kikwete hana jinsi. Lazima awalinde mafisadi kwa vile ndiyo waliomuweka madarakani. Na hapa ndipo siri ya Makamba kuwatetea mafisadi ilipo. Kwani CCM inaendelea kushutumiwa ukiachia mbali kugundulika kuwa ilikuwa nyuma ya wizi wa EPA, Meremeta na mwingine ili kutunisha fuko la uchaguzi na kufanikisha ushindi wao.

Kwa maana nyingine CCM haina tofauti na genge lolote la mafisadi. Tofauti ni kwamba imo madarakani.

Hivyo, aibu zake nyingi zinafichwa humo. Ila siku zinavyozidi kwenda, CCM inaanza kujionyesha ilivyo kiasi cha kuwaudhi wanachama wake ambao hawaoni hasara wala woga kulipuka kwa hasira kama alivyofanya Qares na wengine ambao waliamua kuitolea uvivu CCM.

Bahati mbaya, CCM huwa haina neno kujitathmini zaidi ya kuishi kwa matumaini kuwa kila uchaguzi ujuha na ujinga wa watanzania ambao imewageuza wadanganyika utaiweka madarakani milele. Sasa mambo yanabadilika. CCM inazidi kuumbuka.

Kwa anayejua ufa ulioikumba CCM tangu Makamba ateuliwe na Rais Kikwete awe mwenyekiti, hawezi kushindwa kuanza kutabiri kinachoweza kuikuta CCM. Ina ombwe la wazi la uongozi wenye fikra na visheni ukiachia mbali mipango na uadilifu.

CCM ni dhaifu kuliko inavyoonyesha nje. Ukitaka kujua hili, angalia jinsi viongozi wake wanavyozungumza kwa kukurupuka bila mpangilio.

Angalia watu kama Sophia Simba, Kingunge Ngombale - Mwiru, Yusuf Makamba, Makongoro Mahanga, Rostam Aziz na wengine wanavyopigilia misumari ya mwisho kwenye jeneza.

Kila uchao laana mbili zinazidi kuisumbua CCM. Laana ya kwanza ni ya aliyekuwa katibu wake mkuu marehemu Horace Kolimba ambaye, licha ya kukolimbwa, alisema wazi kuwa CCM imepoteza mwelekeo.

Laana baba ya laana ni wosia wa Baba wa taifa kuwa watakaoiua CCM watatoka mle kutokana na chama kutekwa na matajiri tena vibaka.

Hapa ndipo siri ya ulegevu wa utawala wa sasa ilipo. Rejea maneno ya hivi karibuni ya mzee Butiku: “Tujitambue kwanza sisi ni Watanzania. Haya makundi…mitandao haina maana. Msaidieni rais, (wanamtandao) acheni majungu.

Wezi waliomzunguka rais waondoke. Hatukumchagua rais awe mtumwa wa wafanyabiashara, wafanyabiashara wanatamani kumfanya rais mtumwa.

Hapa ndipo Makamba anapopaswa kumsaidia Kikwete kwa kunyamaza na ikiwezekana kujiondokea. Maana kwa kauli za chama chake na wale wanaounga mkono ufisadi ni wehu tosha.

Wehu ni ugonjwa usababishwao na Mungu na unaweza kutibika. Na isitoshe, wehu mwingine ni wa muda- Lakini utumwa wa hiari ni kilema na hautibiki.

Chanzo: Tanzania Daima Dec.9, 2009.

No comments: