The Chant of Savant

Thursday 31 December 2009

Salma Kikwete na kampeni za urais



JE, Salma Kikwete ameanza kampeni kwa ajili ya mumewe hata kabla ya kipenga kupulizwa? Uchaguzi mkuu ni Oktoba 2010 na vita vya maneno vimeanza.

Kama si hivyo, kwa nini sasa anaonekana zaidi katika vyombo vya habari na kutembelea mikoani, tofauti na ilivyokuwa mumewe alipoingia ikulu?

Watetezi wa anachofanya wanasema anafanya kazi ya shirika lake lisilo la kiserikali la Wanawake Maendeleo (WAMA). Hili nalo linahitaji mjadala kwani linaweza kumuingiza rais, na hata yeye binafsi, katika mgogoro.

Haiwezekani mumewe akawa mkuu wa serikali naye akawa na shirika lisilo la kiserikali, halafu kukawa salama. Ni lazima kutakuwa na mgongano wa kimaslahi na hata kisheria.

Uzoefu tulioupata kutoka kwa Anne Mkapa, mke wa rais mstaafu, Benjamin Mkapa unatosha kumsaidia Kikwete kuondokana na aina hii ya mashirika binafsi.

Salma hawezi kutoa majibu kwa nini aanzishe NGO baada ya mumewe kuwa rais. Hawezi kujibu kwa nini hatuoni wake za viongozi wengine wa vyama vya siasa wakimiliki NGO. Hawezi.

Kwani hata hawa wakiwa nazo hakuna wa kuzichangia. NGO zinazochangiwa ni za wake wa marais; huko ndiko wachangiaji wanatafuta kuwa karibu na ikulu ili waweze kufanikisha malengo yao.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa NGO ya mama Mkapa EOTF. Wengi waliokuwa wakiichangia walikuwa na malengo binafsi.

Imeandikwa na kuhubiriwa: Mke wa Kaizari hapaswi kutenda tendo lenye kuweza kutilia shaka utawala wa mumewe. Tuliishi na kumuona Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Tuliona jinsi mkewe, Maria Nyerere alivyokaa mbali na utawala wa mumewe.

Mama Maria hakuwahi kujihusisha na “uchuuzi” wakati mumewe akiwa ikulu.

Lakini taasisi ya mke wa rais – WAMA imefanya jambo moja la maana. Imeondoa maneno yasemayo WAMA Foundation, The Office of The First Lady of the United Republic of Tanzania kwenye tovuti yao.

Hata neno Jamhuri ya Muungano, kisheria halipaswi kutumiwa na mtu au taasisi yoyote isipokuwa mihimili mitatu ya dola – Bunge, Mahakama na Utawala. Cheo cha mke wa rais (First lady) hakimo katika katiba yetu.

Kama mzalendo, nimejaribu kukusanya baadhi ya maoni kuhusiana jinsi ufisadi unavyoingia ikulu kiasi cha kututatiza.

Ukiangalia kinachofanywa na WAMA hakina tofauti na kile kinachofanywa na EOTF. Ni vema mama Salma akajifunza kutoka kwa wengine. Ajifunze kwa kilichompata Regina Chiluba, mke wa zamani wa rais wa Zambia, Fredrick Chiluba.

Bahati mbaya sana, hata wavuti wa Kurungenzi ya Habari Ikulu inaonekana kutangaza biashara ya WAMA badala ya wizara za serikali. Ajabu hakuna anayestuka wala kupiga kelele.

Kama umma ukishupaa NGO hii inaweza kufutwa hata na mahakama kutokana na mgongano wa maslahi. Na kutokana na kutokuwapo kwa sheria kuchuja na kutangaza wafadhili wake, WAMA inaweza kujikuta katika mgogoro wa kuchangiwa fedha chafu.

Hata neno Jamhuri ya Muungano, kisheria, halipaswi kutumiwa na mtu au taasisi yoyote isipokuwa mihimili mitatu ya dola – Bunge, Mahakama na Utawala. Cheo cha mke wa rais (First lady) hakimo katika katiba yetu.

Bali kwa mtindo huu, Tanzania inaweza kuwa nchi pekee ambapo rais na mkewe wote ni marais. Kikwete ni rais wa Jamhuri huku mkewe akiwa rais wa WAMA.

Ukitaka kujua hili angalia mapokezi ambayo Mama Salma anapewa na taarifa zake zinavyochapishwa na kutangazwa na vyombo vya habari. Ukitafuta uhalali wake kikatiba, hakika haupo.

Hata kama anajulikana kwa ubabe na upayukaji wake, bado mke wa rais wa Kenya, Lucy Kibaki hana mamlaka kama aliyo nayo Salma ambaye anaweza kuingia mkoa wowote kwa kisingizio cha NGO yake na kufanya shughuli za kisiasa kama kulakiwa na viongozi wa mikoa na kukagua miradi ya maendeleo ukiachia mbali kutoa kauli mbiu zinazoonyesha wazi kumpigia debe mumewe.

Kile ambacho Salma anamzidi Lucy, ni ile hali ya kufanya kitu waitacho Waingereza, “one woman show.” Kwani kila lilipo jina WAMA yupo. Maana yake ni kwamba, yeye anapenda madaraka na anataka kufanya kila kitu peke yake.

Kwa nini hatuoni makamu wake au hata wasaidizi wengine wakifanya shughuli za WAMA kama kweli ni ya umma kama anavyodai? Kuthitibitisha hili, tembelea tovuti ya WAMA uone ukweli huu. Hii haiwezi ikawa taasisi ya wanawake na watoto wa Tanzania.

Kuonyesha kuna namna ya kampeni na kutumia mamlaka ya mume wake, hivi karibuni, Mama Kikwete amewahi kutoa namba yake ya simu ya mkononi ambayo ni 0754-294450.

Aliitoa kwa wanawake mkoani Singida ili waweze kumpigia au kumtumia ujumbe mfupi wa maneno pindi waume zao watakapowanyanyasa kutokana na kitendo cha wao kwenda kupima kwa ajili ya kujua afya zao.

Japo kwa juu hili linaweza kuonekana ni jambo bora, kwa mtu anayejua mipaka ya mamlaka yake na utaratibu wa utawala kisheria, angeshauri wahusika waelekeze madai yao kunakohusika: polisi, vituo vya kutetea haki za binadamu na hata wizarani.

Licha ya kuwa ubabe, hii ni kampeni ya wazi kuonyesha wahusika wanawajali wananchi jambo ambalo si kweli. Kwanini hasira zake zisielekezwe kwenye kumshauri mumewe kupambana na ufisadi kama ana uchungu na nchi hii?

Ina maana hajui kuwa ujinga na umaskini ndivyo vyanzo vya yote haya? Sijui kama, hata kwenye kupokea misaada, anauliza usafi wa mtoaji.

Kwa kadri nijuavyo upenzi wa sifa wa watawala wetu na watu wao, kama utafanyika uchunguzi huru juu ya matumizi ya WAMA, usishangae pesa inayotumiwa kwenye ziara ikawa kubwa kuliko hiyo inayowafikia walengwa. Bahati mbaya sijawahi kusoma popote taarifa ya hesabu za mwaka za WAMA au EOTF.

Wengi wanaweza kuona kama tunamuandama mke wa rais au kutotambua umuhimu wa kupigania haki za akina mama. Lakini swali ni, kwa nini mke wa rais, wakati tuna wizara yenye watendaji wanaolipwa pesa ya kodi yetu?

Kwa nini misaada anayopokea isipelekwe moja kwa moja wizarani au kwenye mashirika huru kama kweli ana uchungu na walengwa na si kujipatia umaarufu? Kubwa zaidi ni kutumia ikulu kwa manufaa binafsi, yawe yake au mumewe na marafiki zake.

Je, akina mama wa Tanzania wataingia mkenge wake huku waume na kaka zao wakizidi kuteswa na sera za Kikwete za kuvumilia mafisadi?

Je, atawalainisha wasahau kuwa Kikwete hajatimiza ahadi zake? Je, watahoji uhalali wa NGO yake na kumwambia ukweli kuwa ni ya mashaka na utata?
Chanzo: MwanaHALISI Desemba 23, 2009.

1 comment:

Anonymous said...

Well done Mhango. Hiki kimwanamke kifupi kama pia kimezidi tamaa. Hakina tofauti na Anna Mkapa wala Kikwete Mkapa. Kimakonde hiki kishamba na fisadi sina mfano. Ila iko siku watanyea debe Ukonga niamaini. Kikwete ni balaa kwa taifa na sina la kuongeza yote umeyamaliza. Laiti hawa nguruwe wangelikuwa wanasoma alama za nyakati!