Aliyekuwa waziri mkuu Joseph Warioba
INGAWA hii inaweza kuonekana kama kejeli, kuna ukweli usiopingika kuwa wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi wanamuonea Mwenyekiti wa chama chao, Rais Jakaya Kikwete. Wanachofanya ni sawa na kumbembesha sungura mzigo uliomshinda tembo.
Shutuma za hivi karibuni dhidi ya serikali chafu na dhaifu ya Kikwete zimetolewa kwa wakati kwa namna muafaka. Kwani wakongwe hawakukurupuka ingawa wamesahau kitu kimoja-mwenyekiti wao hakujaliwa masikio.
Amejaliwa kinywa kipana na ujasiri wa ajabu hasa unaowashinda wenye akili. Ndiyo maana tunaona kama wanamuonea. Kumsaidia ni kuwahimiza wananchi wampumzishe. Maana mzigo umemlemea na unaweza kumuumiza.
Hata hivyo, wakongwe hawakukurupuka. Wamemngojea Kikwete afanye vitu vyake ndipo walipomtathimini na kumpa ‘live’ tena kwa uwazi kuwa anazidi kulizamisha taifa hasa kwa kuliweka mikononi mwa mafisadi uchwara.
Kwanza walimtaka asambaratishe mitandao iliyomwingiza madarakani kihalifu baada ya kugundua kuwa iligeuka mizigo na kikwazo kwake kufanya kazi. Kama ada, aliwapuuzia na kula jiwe.
Sasa wanamtaka afanye maamuzi magumu ili kuinusuru nchi na utawala wake.
Ila wamesahau kitu kimoja. Kikwete si kiongozi wala mtawala. Watani wake humuita msanii na asipinge ikimaanisha kukubaliana na sifa hii ambayo kimsingi ndiyo inayofanya kazi kwa sasa baada ya taratibu zote za uongozi na utawala kuwekwa kapuni.
Hivyo hapa wenye kushauriwa kufanya maamuzi magumu ni wananchi hasa wapiga kura kuondokana na mazoea na kuishi kwa matumaini kama waathirika.
Kwa wanaokumbuka Kikwete alivyokuwa akikesha akipiga kampeni hadi kuzimia kwa muda kule Mwanza akihutubia, watakubaliana nasi kuwa Rais wetu, pamoja na udhaifu mwingi, ameonyesha kipaji kimoja cha ajabu-kutosikiliza la muadhini wala mteka maji msikitini! Ni kichwa ngumu!
Wakongwe wamesahau kitu kingine; Mwenyekiti wao ni bingwa wa kutoa ahadi na bingwa wa kutozitekeleza ukiachia mbali kuachia mambo yajiendee ilhali yeye akiwa ughaibuni akitumbua. Vijana wa mjini wanasema-kutesa kwa zamu.
Kitu kingine walichosahau wakongwe ni ukweli kuwa wakati akijinadi, Kikwete alionyesha wazi kutokuwa na sera zaidi ya mitandao ya kuchafuana na kusaka ngawira.
Rejea kutumia waandishi nyemelezi wajiitao waandamizi wakati si waandamizi kitu bali wadandizi na wasaka ngawira ambao wazungu husema: They can say anything for a buck.
Ukimuondoa Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyestuka mwaka 1995, wengine walisema: ngoja yamshinde tumpe vipande vyake.
Nyerere alijua mambo yaliyokuwa yakifanyika nyuma ya pazia kati ya Kikwete na wale wezi aliowastukia na kuwapa ‘live’ kuwa walikuwa wamejilimbikizia mali nyingi itokanavyo na ujambazi wa kisiasa na ufisadi. Kwani hamkuwaona wakiadhirika baada ya laana ya gwiji huyu kuwaandama?
Wakongwe walisahau kuwa Rais Kikwete ni mjanja, mjuaji na mtoto wa mjini ambaye ameweza kuuingiza mjini umma na asichelee lolote. Hawakujua amejaaliwa kinywa kipana na masikio haba ukiachia mbali kutojaliwa kuona mbele hasa alama za nyakati.
Hapa ndipo yanapoibuka madai makali ya akina Mateo Qares, Juma Nkangaa, Salim Ahmed Salim, Joseph Butiku, Joseph Warioba, Philip Mangula na wengine wenye majina na waandamizi katika chama.
Kitu kingine ambacho wakongwe wamesahau ni ukweli kuwa CCM si yao tena. Ilikuwa yao zama zile za miiko na maadili ya uongozi.
Ya sasa ni ya wafanyabiashara nyemelezi, walamba viatu, wapambe na mafisadi uchwara wanaouza watu na nchi yao bila kujibakiza hata wao.
Ni ya vipofu wasiojua kesho bali leo tu ambao hawana aibu kusema kuwa Kikwete ni maarufu kuliko chama. Hivyo ni mtaji wa chama badala ya chama kuwa mtaji wake.
Siku zote wazee ni hazina ya jamii kama watatumika vizuri. Hii ndiyo maana wameamua kumkabili Kikwete wakati huu mzuri kwa jamii na mbaya kwake-kuelekea kwenye uchaguzi
mwakani.
'Timing' hii ni nzuri kama itatumika vizuri hasa kwa umma kusikiliza maonyo ya wakongwe ambao hata mambo yakienda vibaya vipi hawawezi kulala njaa.
Hawa hawasukumwi na tumbo wala utumwa wa kutumiwa na mafisadi kama walivyobainisha kusema kuwa Rais ni mtumwa wa mafisadi.
Hawa wanasukumwa na fikra, busara na uoni wa mbali. Hawa si watu wepesi wanaoweza kununulika kwa shilingi mbili. Si watu wa kuweza kununuliwa na mafisadi uchwara waliotamalaki chamani wakimgeuza Kikwete ‘muungu mtu’ wasijue kila jambo chini ya jua lina mwisho.
Kama alivyosema mzee Qares: Hawa hawana hasara nchi ikisambaratika. Watachomoa pasi za kusafiria na kurejea uraia wao. Hawa ni sawa na ndege kwenye mti. Ni kupe kwenye mgongo wa ng'ombe.
Wakongwe wameamua kuwakabili mafisadi waliomzunguka Kikwete na Kikwete mwenyewe kwa kujua wazi kuwa hawa hawana ubavu wala tishio kwao.
Kwa sababu hawana tofauti na vyangudoa ambao mara nyingi huangalia mfukoni. Unapoishiwa nao wanatoweka. Angalia walivyompiga teke Benjamin Mkapa waliyekuwa wakimuabudia. Hata Kikwete atapigwa teke siku madaraka yakiondoka mikononi mwake.
Kuna jambo hata hivyo wakongwe wamezingatia- mfano hai wa Afrika Kusini ambapo Thabo Mbeki alipigwa chini ili kuikoa nchi na chama. Ukiangalia nchi hizi mbili zenye uhusiano wa kihistoria,
zina mambo yanayofanana. Afrika Kusini baada ya kung'atuka baba wa taifa mzee Nelson Mandela, ilianza kuendeshwa kibabe.
Tanzania kadhalika baada ya kung'atuka Mwalimu Nyerere mambo yakaanza kuwa shaghala baghala.
Kuzikwa kwa Azimio la Arusha na kuzaliwa Azimio la kijambazi la Zanzibar ambalo tofauti na la Arusha halikuwa na sera zaidi ya uroho. Azimio la Arusha liliasisi sera ya ujamaa. Je, la Zanzibar zaidi ya ufisadi liliasisi nini?
Utandawazi nao uliruhusiwa kuingia nchini bila kuwekewa vizuizi na bila kufahamu kuwa utageuka utandawizi au chambelecho Profesa Issa Shivji; 'mtandao wa wezi' umeshika kani na kuangamiza uchumi wa nchi badala ya kuuboresha.
Maandamano ya wafanyakazi karibu katika kila sekta yameshtadi yakiakisi kutoridhishwa na sera zilizopo.
Ahadi zinazotolewa kutotekelezeka kutokana na mazingira yenyewe kutoeleweka, hivyo maisha bora kwa kila Mtanzania yamekuwa ni ndoto.
Je, kwa haya na mengineyo, upo uhalali wa kumlaumu Rais Kikwete? Yeye amerithi mfumo mbovu, kuurekebisha si kazi yake peke yake bali ni kazi ya Watanzania wote.
Chanzo: Mwananchi Desemba 17, 2009.
No comments:
Post a Comment