Wednesday, 16 December 2009

Ukuukuu wa kamba si upya wa ukambaa

HUU waraka sikuandika mimi. Umeandikwa na Mzee Maneno akituzodoa mie na Mgosi Joe Machungi almaarufu Makambale.

Mzee Mpayukaji salamu, Juzi nilicheka niliposikia mwehu mmoja akituita wehu watu wazima na busara na majina yetu. Hata hivyo si kosa lake. Kila mwehu hudhani watu wote ni wehu kama yeye.

Na kila ajikombaye hudhani wote hujikomba kama yeye. Kwake maisha hayaendi hadi ajikombe ili apewe makombo akombe na kuishi! Hivi ni wehu kiasi gani kutetea utumwa tena wa kifisadi?

Kwanini siku hizi tumegeuka wapayukaji bila vipaji. Muulize Sofii Fyatu wa Yanga ameishia wapi zaidi ya kuonekana changu la kisiasa. Muulize Kimdunge Mwehu na ujambazi wa lifamilia lake pale kwenye mabung’o. Sasa nasikia amehamia kwa chingaz ili awatoe upepo. Huyu bila kukwapua na kujikomba kwa njaa kaya kama Joe Mgosi tumuitaye Ma-kambale, hawezi kuishi.

Kwa taarifa yenu, nilihudhuria kongamano la kumbukumbu ya Mchonga wa Burito. Nilimwaga mipwenti ila waandishi walinifanyia unoko kutochapisha vitu vyangu. Nilimwaga vipande hakuna tena.

Wakati MNF wakiadhimisha kivyao kule chuoni na kijiwe sambamba kilifanya hivyo chini ya dhana tuliyoiita MNF yaana Mkuu Naye Fisadi. Maana Mwalimu alikuwa mpenzi wa kahawa. Ndiyo maana nilitumwa na kijiwe kukiwakilisha na kumwaga mapwenti.

Kwa hiyo, kwa kujikumbusha ilivyo na jinsi kijiwe kilivyomshupalia Mpayukaji, umeandikwa waraka huu. Hivyo, ijulikane mlengwa hapa ni Mpayukaji na wale wenye sifa na tabia kama zake.

Mna habari wazo kuwa Mpayukaji utemwe usigombee ukuu wa kijwe nilitoa mimi lakini kipaza sauti kikawa kimekumbwa na mgao wa umeme kiasi cha kutosikika kwanza?

Hata hivyo silaumu. Maana wazee wenzangu walinisikia kwa vile nilikuwa nimekaa karibu nao wakarusha laivu kipaza sauti kiliporejea.

Ingawa Mgosi anaota ndoto za mchana kusema wewe unakubalika, ukweli ni kwamba unakubalika kwa mafisadi si walala njaa wa kijiwe ulichokigeuza kuwa Danganyika. Hata mwenyewe hujikubali ndiyo maana wewe na bibi yako mnapoteza muda mwingi mkizurura huku na kule.

Kukwepa kuzomewa na kuzodolewa kwa upuuzi unaoendeshwa na akina Mbwa Mwitu na wenzake akina Kanji.

Nikuulize. Tangu uukwae ukuu wa kijiwe umefanya nini zaidi ya kuwanufaisha mafisi ahadi waliononeana kama paka wa dukani kwa wahindi? Nikuulize tena. Umefanya nini zaidi ya kuzidi kutuuza walevi na kahawa yetu.

Hufai. Wewe na Mbwa mwitu wako ni mafisi na mafisadi msiostahili kuonekana kwenye kijiwe zaidi ya kunyea debe kule Ukonga. Hamna maana senzi sana we. Unanitolea mimacho ili iweje? Unadhani sikuoni unavyowaambia vibaraka wako wanipatilize ilhali wa kupatilizwa ni wewe mjalaana mkubwa.

Zamani nikisema wakasema huyu anapayuka tu. Sasa akina Mtoboasiri Kalesi, Wamsimamo Butuka, Jumaa Nkhahanga na wengine wenye majina yao wamelibutua na kukukaanga.

Nawe kwa ujuha badala ya kujitetea kwa kuonyesha ulipofanikiwa unadai wanamuonea wivu! Mambo ya kitunituni haya. Wakuonee wivu kwa uchafu wako kweli? Una nini katika historia baadaye ndugu? Fitina na umbea mtupu.

Tena utoto japo waonekana mkubwa lakini mtu mzima hovyo! Una nini zaidi ya kungojea kifungo au kuishi kwa kujikomba kwa atakayekurithi kama jamaa yangu Tunituni na Anae Tamaa sura mbaya?

Umejizungushia vibaka wanakuhadaa na kukutumia kama alivyosema Butuka unajiona bonge ya janja siyo? Hakuna sifa mbaya kama kutumiwa hata uwe mkubwa na mtukufu kiasi gani. Kutumiwa ni utumwa period.

Kutumiwa ni kutumiwa. Hakuna kutumiwa kuzuri. Kiatu hata kiwe cha dhahabu kina heshima gani? Mbwa hata alale kwenye kasri ni mbwa tu. Heri ya mbwa mwitu kuliko mbwa wa kufungwa. Heri ya mja maskini mwenye jeuri kuliko mfalme juha atumiwaye na kila mafisi na mafisadi kama unavyotumiwa kwenye kijiwe chetu kitukufu. Una bahati tunaishi kwenye nchi iliyokwishabinafisishwa. Ingekuwa zama zile mbona ungekoma jizi wee.

Akina mzee Maneno, Kidevu na Mchunguliaji na busara zao wamekusaidia kukuonya kuwa kuendelea kuwa mkuu wa kijiwe ni kuchuma janga zaidi. Maana watukutumia wa kukutumia na wa kufungwa ni wewe. Muulize shoga yako Tunituni wa Makapu aitwaye Mipawa.

Hata kama hiki ni kijiwe na si nchi, lazima uonyeshe vipaji vya uongozi badala ya kuonyesha umahiri wa udokozi na ujuha. Unasikia mzee Mpayukaji? Unashangaa na kulalama nini? Nakwambia wewe si mwingine. Kubali. Kijiwe kimekushinda. Si ukitoe tu unang’ang’ania nini wakati hata sera wala huna hata kama una sura? Sura yako hailiwi.

Nasikia na majuha wenzio waliotuhadaa kuwa wewe ni chaguo la God wanaanza kusambaratishwa mmoja mmoja. Na bado. Huu ni mwanzo tu. Tulikwambia kuwa akina Ewassa si watu.

Ungejua wana uchu wa fisi na sasa wanakukaanga baada ya kukutumia na kuona hufai. Huyu Mgosi na Shangingi la Kihaya hawawezi kukusaidia kitu. Watakusaidiaje wakati wanaharisha kwa midomo?

Wenyewe wameshindwa kujisaidia zaidi ya kujikomba kwako wasijue ni wafu wawili mnakokotana kuelekea kuzimu. Siku zaja mzee Mpayukaji kitoe na utubie walevi tukusamehe au tukufunge ili mambo yaishe wenye akili na taamuli waongoze kijiwe.

Kipindi kile ukituingiza mkenge tukuchague ulitumia mitandao ya wambea na mafisi. Sasa tumewastukia sijui utatumia nini muishiwa wewe?

Mpayukaji hebu tuongee ukweli. Hivi kweli wewe si msanii? We si muongo na mbabaishaji? Hebu nieleze. Tangu tukupe ukuu wa kijiwe zaidi ya kutuibia kahawa na kashata zetu tena wewe na mkeo na marafiki zako umefanya nini cha maana?

Zaidi ya kuendekeza uzururaji na visingizio nambie ndugu yangu umefanya nini? Una habari uliwaahidi walevi kahawa na kashata kwa wingi hadi wajihisi wako Kanani wakifaidi manna na maziwa? Kumbe hatukujua wewe ni bonge la msanii na uliposema wote tutafaidi ulimaanisha wote vibaka na mafisi wanzako!

Hebu ndugu yangu tuache utani. Unasema watu wanakuonea wivu na wana chuki binafsi. Ya kweli hayo wakati unayejichukia ni wewe mwenyewe?

Hebu angalia ulivyogeuza kijiwe kuwa shamba la bibi. Hebu angalia kijiwe kinavyokwenda utadhani wewe ni kipofu? Hivi unashindwa nini kuwaambia akina Ewaa na wenzie waache kuiba kashata na kahawa zetu?

Ingawa unaona tunaokwambia ukweli tunakuchukia kiasi cha wewe kutuchukia, kuna siku utaona mwanga.

Muulize Tunituni pale kijiweni. Tusingetaka uwe kama mfalme juha aliyesifika kwa kucheka hata kwenye misiba hadi akaitwa chekacheka akicheka wakati taifa lake likiangamia . Tia akilini ndugu yangu.

Naachia hapa. Naona walamba viatu wako wana marungu wakinijia. Sitaki kujichafua kubishana na wehu nisijeonekana mwehu bure.

Ila kaka jua. Ukuukuu wa kamba si upya wa ukambaa. Hata wazee tuna pwenti kuliko hao vijana unaowatapeli kirahisi kama ulivyosema siku ile kuwa ukichaguliwa kuwa mkuu wa kijiwe tena utawapa ulaji wa kahawa na unywaji wa dezo kama ufanyavyo wewe na bi mkubwa wao mpenda sifa pimbi wa Mpimbuke wa Shari lakini Salama.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 16, 2009.

No comments: