Friday, 4 December 2009

Takukuru ifutwe au kusukwa upya

HAKIKA, ni aibu na hasara kuwa na taasisi zinazojinadi kuwa za wananchi ilhali zikiwa ndiyo kichakacha kulihujumu taifa kwa kutumiwa na watawala fisadi. Hivi karibuni tulishuhudia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikikamia kuwahoji wabunge kwa kupokea posho mbili ingawa spika wa Bunge Samuel Sitta alisema posho hizi ni halali. Huenda, nasema huenda, huu ni mkakati mahsusi wa makusudi wa kutaka hata kuwasafisha watuhumiwa wa kashfa ya EPA na wengine wengi ambao mwisho wa siku, kama ilivyopendekezwa hivi karibuni kwa rais mstaafu-mwenye kashfa na nyumba yake pia-Benjamin Mkapa, kulipwa mabilioni ya shilingi kwa dhambi ya kuliibia na kulihujumu taifa ukiachia mbali ‘kutaifishwa’ kwa Kiwira.

Bahati mbaya, suala hili linaonekana kuondolewa mbele ya hadhira ingawa tatizo bado linazidi kututumka kama jini lililotolewa kwenye chupa.

Ni haki kulipongeza bunge ambalo kwa mara ya pili limesimama imara dhidi ya mbinu hizi mfu na chafu. Maana, kama bunge lingekubaliana na upuuzi huu, lingejigeuza kikaragosi na mhuri wa kutumiwa na wahalifu wenye madaraka kuendelea kulibaka na kulinajisi taifa letu.

Kimsingi,watuhumiwa wa Richmond si watu wa kusafishwa bali kufungwa. Na wale wenye ndoto za kurejea tena kwenyeukuu wasahau-mambo yamebadilika na pepo ya mabwege, taratibu, inatoweka. Badala ya mafisadi wenye madaraka kuotea kutuibia tena kupitia uchaguzi watueleze wametekeleza nini katika ahadi lukuki waliozotoa tena kwa hiari yao.

Hadi sasa sijajua mantiki ya kuendelea kutomshitaki waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa na wenzake walioachia madaraka baada ya kubainika walikuwa nyuma ya Richmond! Sijajua mantiki ya rais Jakaya Kikwete swahiba na mshirika wa Lowassa kuendelea kutotoa maelezo kuhusiana na kufikishwa mahakamani kwa Lowassa ukiachia mbali kwa rais kuelezea alivyoshiriki kulihujumu taifa kwa kuridhia uchafu huu utokanao na ulafu, myopia na nyongea ya maono!

Bado sijajua mantiki ya watanzania kuzidi kuiamini, kuithamini na kuiheshimu Takukuru ambayo mkurugenzi wake, Edward Hoseah sambamba na mwanasheria wa serikali mstaafu Johnson Mwanyika, walitaka kuwasafisha washirika wao kwenye kashfa hii iliyopoteza mabilioni ya shilingi ambayo yangetumika kufanya shughuli za kimaendeleo.

Hivi karibuni, spika wa bunge Sitta-ingawa bila kutaja majina- alieleza jinsi wezi wa Richmond walivyo na mtandao mpana unaohusika karibu na kashfa zote nchini. Kabla ya vumbi kutua, mbunge wa Nzega, Lucas Selelii aliongezea uzito kwa kutaja majina.

Ajabu serikali na Takukuru hii hii badala ya kutaka msaada wao kuhusiana na mali na majina alizotaja spika kuwa licha ya kupatikana kwa uhalifu, zimefichwa nje ya nchi-alizitaja baadhi ya nchi, inaendelea na mikakati yake ya kutaka kumpatiliza kwa kuridhia bunge lifumue na kuibua kashfa ya Richmond.Hatuwezi wote kuwa wapumbavu, woga wala wanufaika wa mchezo huu mchafu ambao ni mauti kwetu na taifa letu.

Tumeishaona jinsi wana kamati teule ya bunge iliyoshughulikia kashfa hii anavyoandamwa na makundi ya ujambazi na ufisadi bila serikali hata kutoa karipio zaidi ya kuamuru Takukuru iongoze chumvi kwenye donda!

Kwa ukimya huu na ushiriki wa nyuma ya pazia, wengi wanadhani rais Kikwete ni mshiriki mkuu na mwasisi wa uchafu huu ambao amekuwa akiufumbia macho kwa muda mrefu huku muda wake wa kuwa madarakani ukiyoyoma naye akituaminisha kuwa anafaa kugombea na kuchaguliwa tena. Atagombea kwa udhu upi iwapo kwa miaka yote aliyokuwa madarakani hajawahi kukanusha uhusika wake na kashfa ya EPA na sasa Richmond ukiachia mbali kushindwa kutaja mali zake na mkewe?

Ili afanye nini zaidi ya kuizamisha nchi zaidi kwa kunyamazia ufisadi? Tumekuwa tukimfananisha Kikwete na Mkapa karibu kwa kila kitu bila ya yeye kujibu ukiachia mbali vibaraka na walamba viatu wake kutoa majibu yasiyo na mashiko. Rejea kutolewa kwa majibu yanayojikanganya ilipodaiwa na mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba kuwa Kikwete ni mhusika mkuu wa Richmond.

Kimsingi, Kikwete ameishiwa na anaonyesha wazi asivyo na ubavu wa kuwabana wala kuwashughulikia mafisadi papa ambao, kimsingi, ndiyo waliomweka madarakani kutokana na kutunisha fuko lake la uchaguzi na kuendesha serikali yake nyuma ya pazia.

CCM imekuwa ikijibu kwa majibu uchwara inapoguswa kuhusiana na kashfa zilizopoteza mabilioni ya taifa huku ikesema: wenye ushahidi waupeleke Takukuru ili utumike kuwapatiliza watoa habari-whistle blowers kama inavyowatokea akina Dr. Willbrod Slaa na Sitta; kutaja kwa uchache.

Nani anaiamini Takukuru ambayo mkurugenzi wake, alionywa na kuambiwa ‘awe makini’ ili hali alichofanya kilitosha kumvua madaraka? Lakini nani atamvua madaraka iwapo wanaopaswa kufanya hivyo wananuka hata saa nyingine kuliko yeye? Je Kikwete anaogopa nini kuwawajibisha na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa Richmond hata EPA? Je anaogopa wasimwanike na akaadhirika? Je ataficha ukweli na kuukimbia hadi
lini? Kama yeye anawaogopa umma haumuogopi mtu.

Wakati wa kumkabili Kikwete na genge lake umefika ili kuiondoa nchi kwenye makucha ya mafisadi. Hatuwezi kuwa na maisha bora wala kupelekwa Kanani chini ya utawala fisadi na wa kifisi unaoibia taifa.

Kuna suala jingine linalomwonyesha Kikwete na Takukuru kuwa hawafai na wanafanana na Mkapa. Rejea kwa Takukuru kutochunguza NGO ya mke wa Kikwete, Salma ambayo haina tofauti na ile ya Anna Mkapa aliyemtia majaribuni mumewekiasi cha kuingia madarakani akiwa bwana Clean na kuondoka akiwa Bw. Mess kutokana na uroho wake.

Tunashindwa kuelewa. Kama Kikwete ameshindwa kupambana na ufisadi na kuleta tija kwa taifa na kuonyesha mwelekeo kwenye ngwe ya kwanza ambapo anakabiliwa na kibarua cha uchaguzi mwakani, atawezaje kuacha kuiacha nchi msambweni atakapopewa ngwe ya lala salama ambayo imeonyesha inavyotumiwa na watawala kuuibia umma wakijua wazi hawatarejea madarakani kama ilivyotokea kwa Mkapa na Bakili Muluzi wa
Malawi?

Je watanzania wapiga kura wataendelea na uzezeta wamchague tena Kikwete ilhali
ameonyesha asivyofaa kama alivyowahi kudokeza na kuonya baba wa taifa Marehemu
Julius Nyerere ambaye kadhalika alituasa tusimchague Lowassa na akabainika kuwa
hafai na ni mroho wa madaraka na mwenye kujilimbikizia mali zitokanazo na jinai
ya kuliibia taifa?

Umefika wakati wa kuikataa Takukuru ambayo licha ya kuendeshwa kwa kodi yetu, imekuwa uti wa mgongo wa mafisadi na serikali zandiki ziendeshwazo kijambazi.
Rejea kuvunjwa na kufilisiwa kwa Benki Kuu chini ya kashfa ya EPA na kuridhia kwa wezi wa Kiwira kulipwa fidia kwa jinai yao.

Hakika, Takukuru haifai ifutwe. Ni chaka la mafisadi. Kuna haja ya kushinikiza ifutwe mara moja huku tukijiandaa kumuumbua rais kama hatakuja na maelezo yanayoingia kichwani na kutumia cheo chetu kuwakingia vifua mafisadi wahujumu wa taifa.

Jambo muhimu ni kuiondoa Takukuru mikononi mwa ikulu ambamo inatumika vibaya kulihujumu taifa kama tulivyobainisha hapo juu.
Chanzo: MwanaHALISI Desemba 2, 2009.

No comments: