How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 16 December 2009

Bora uadilifu kabla ya 'Kilimo Kwanza'

SINA kawaida ya kuingilia sera na mipango ya watawala hasa ikiwa inaingia akilini. Nitawezaje kupinga kitu kinachoingia akilini? Ila inapotokea mtu au kikundi cha watu kikaja na sanaa za kitoto, huwa sina subira wala simile.

Katika kuelekea uchaguzi mwakani, baada ya watawala kuishiwa kila uongo wa kuweza kupatia kura, nasikia kelele nyingi zikipigwa.

Zinasema, ili kumkomboa Mtanzania, basi hakuna budi kilimo kuwa kitu cha kwanza kufikiriwa na kupewa kipaumbele.

Nashindwa kuamini. Kilimo kwanza au masikio mabovu? Nani huyu anasema kilimo kwanza wakati haohao wanaojaribu kutuaminisha kuwa wamedhamiria kukiinua, ndiyo haohao waliokiua na kuanza sera za ubinafsishaji, ugenishaji, uchotaji, ufisadi, ulaghai, usanii na kila aina ya ubabaishaji?

Hawajui wanalosema? Je, na umma utaingia mkenge kwa mara nyingine badala ya kuwauliza zile sera tulizoingia nazo mkataba wakati wa uchaguzi kwamba zimeishiwa wapi?

Kwanza nani anataka kulima? Hata punda na maksai hawapendi kulima. Nani alime wakati kuna umachinga, ufisadi na ubabaishaji vinavyolipa kwa haraka na bila kulowa jasho?

Nani wa kulima iwapo vijana wengi wameishatekwa na umachinga; wakati wazee nao wametekwa na umachinga wa kisiasa? Au serikali inataka kujifanya kuwa haijaandaa kizazi cha sasa kwa ajili ya kilimo?

Na wakishalima, watauza mazao yao wapi? Je, si kweli kwamba serikali itaruhusu wafanyabiashara walewale – wafadhiri wa chama tawala – kukopa mazao ya wakulima?

Nani alime wakati mtu anaweza kulala lofa na kuamka tajiri baada ya kutengeneza nyaraka feki kwa msaada wa watawala na kujipatia mabilioni ya shilingi za umma kwa muda mfupi tu?

Nani anataka kulima wakati pale Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kumejaa mabilioni ya shilingi ambayo serikali na washirika wake wanaweza kuchotea wawatakao?

Nani anataka kulima wakati anaweza akavunja benki au kughushi na kupata mamilioni ya shilingi na kuitwa mheshimiwa au mfanyabiashara maarufu wakati ni kibaka na jambazi la kawaida?

Yupi anataka kulima wakati anaweza kuingia mikataba ya kijambazi na kuwa milionea na kuabudiwa kama wezi wetu? Je, watu wa aina hiyo wanaweza kuwekeza kwenye kilimo kisicho na tija?

Nani mpumbavu huyu ambaye yuko tayari kujipinda kulima ili mazao yake yaishie kuwanufaisha wafanyabiashara haramu wa mazao wenye kula na wakubwa? Hivi kweli baada ya miaka zaidi ya 40 ya uhuru bado kuna mtu mpumbavu kiasi hiki wa kufanya hivi au kuamini uongo huu?

Nakumbuka Bw. Benjamin Mkapa alivyokuwa akitueleza kuwa bila uwekezaji huwezi kuwa na uchumi wa kisasa. Kumbe alimaanisha uchumi wake, mkewe Anna Mkapa, watoto wake na marafiki zake.

Hata ahadi za Rais Jakaya Kikwete, “Maisha Bora kwa kila Mtanzania” zimeanza kuishia kuwa “wote wao” na siyo wote kama tulivyohadaika na kuamini.

Hebu tuzingatie ushahidi huu. Hii ni karne ya 21 ya sayansi na teknolojia. Serikali makini haiwezi kuwekeza kwenye ununuzi wa mashangingi badala ya matreketa, kisha ikadai kuwa inataka kujikomboa kupitia kilimo.

Huwezi kuingia mikataba feki ya uwekezaji kwenye madini ukamshawishi mtu kuwa unaweza kuinua kilimo. Kilimo ni sayansi – mikakati, mipango, ufuatiliaji, uwezeshaji na uwajibikaji. Kilimo ni visheni si makeke ya maneno majukwaani.

Ajabu hawa wanaosema “Kilimo kwanza” hawaelezi watakavyomkwamua na kumwezesha mkulima waliyemtelekeza na kuweka taifa lake rehani miaka nenda rudi.

Rejea uwekezaji wa kijambazi unaolizamisha taifa letu kwenye umaskini wa kunuka. Na hali ikiendelea hivi, vita baina ya walionacho na wasionacho haiwezi kuepukika.

Kwa nini iwe “Kilimo kwanza” na si “Madini na uwekezaji Kwanza? Jibu ni rahisi sana. Huko kwenye madini ndiko watawala na marafiki zao walikowekeza. Ndiko walikochuma.

Ndiyo maana pamoja na Tanzania kuwa na madini mengi ya kuwezesha kujitosheleza kiuchumi kama Botswana, watawala hawataki kuangalia mikataba hiyo badala yake wanaimba “Kilimo Kwanza.”

Huwezi kuwashawishi Watanzania kuwa utafufua kilimo wakati umeshindwa hata kukusanya kodi itokanayo na madini. Serikali iliyoshindwa hata kujadiliana na wawekezaji katika sekta ya madini, itawezaje kusimamia kilimo?

Kama si hivyo, yako wapi marekebisho ya mikataba ya kijambazi iliyoingiwa na utawala uliopita? Mbona sasa ni karibu miaka mitano hakuna hata mkataba mmoja uliorekebishwa zaidi ya kuingia mingine ya kinyonyaji?

Mfano hai ni mkataba wa Buzwagi, ambapo waziri alisaini mkataba nje ya nchi na kinyume cha taratibu.

Tukubaliane. Kwamba kama ilivyokuwa kwenye ahadi ya safari ya kwenda Kanani iliyoishia kuwa jehanamu, hata kilimo kwanza ni sanaa za kawaida za kisiasa.

Kama mpango uliopo ni kutegemea hiki kilimo cha ngwamba, basi hakuna kubwa litakalofanyika. Wakulima ambao bado wanalima kwa ajili ya matumbo yao, wanafanya hivyo kwa sababu hawana la kufanya wala pa kwenda.

Wangekuwa na mahusiano na mijini, wangeachana na jembe na kutimkia mijini ambako wezi wao wa kisiasa wanaishi peponi na kurejea mara moja kila baada ya mitano kuchuma wasichopanda na kuvuna wasipolima. Ujinga.

Kelele za za kuletwa matekta tayari zimesikika. Lakini ambacho serikali haijasema ni kule kwamba haya nayo hayataingia katika mashamba ya wakubwa kama ilivyowahi kutokea kwenye mradi wa kupambana na mbu wakati serikali ya Japan ilipotoa msaada wa magari.

Badala ya magari hayo kutumiwa kama ilivyokusudiwa na serikali ya Japan, yalitumiwa na wakubwa kwenye biashara zao. Hiyo ilikuwa ni miaka ya mwishoni ya 80. Leo ni 2009. Tusubiri.

Jambo la muhimu hapa ni kwamba bila kuwa na watawala wenye adili na taamuli, kila kitu ni bure. Watu walioshindwa hata kusimamiana maofisini hawawezi kusimamia sera ya kilimo na kulinda mazao ya mkulima.

Huku ni kukumbuka kiatu baada ya kumaliza safari. Wakulima tieni akilini. Mkishapiga kura “Kilimo kwanza” kinakufa na kuwa “Sisi kula kwanza.”

Hapo ndipo mafisadi walewale watateuliwa kwenye ulaji zaidi ili kuzidi kuwatumieni kujineemesha wao na mawakala wao. Hao ndiyo watakaoteuana kwenye vyeo na ulaji kwa kulipana fadhila.

Bila uadilifu na mipango mizuri hakika hakuna kitakachofanyika katika kilimo. Serikali yoyote makini haiwezi kuongoza, kutawala au kuikwamua jamii kwa siasa na sera za kudandia na kuendeshwa na matukio.
Chanzo: MwanaHALISI, Desemba 9, 2009.

No comments: