ZAMANI kulipotokea mgawanyiko ndani ya chama cha TANU/CCM, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwa kutumia busara na vipaji vyake, harakaharaka aliitisha vikao vya Kamati Kuu ya chama na kuweka mambo sawa.
Baada ya kung’atuka kwa Mwalimu na busara kuwa haba, huku siasa zikigeuzwa kijiko cha kuliibia taifa, kulianza kutokea nyufa kwenye chama chake.
Rejea kuibuka kwa kundi la 55 ambalo kama si Nyerere kuvaa jezi upya na kurejea ugani, CCM ingekuwa historia. Hii ilitokea baada ya Zanzibar kutaka kujiunga na Jumuia ya Kiislamu (IOC). Ujasiri huu sasa ni historia.
Ukiachia mbali historia ya Tanzania, kuna mfano toka nchi jirani ya Kenya ambapo kichwa ngumu Daniel arap Moi alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la chama tawala cha KANU.
Hii ni pale alipotaka kulazimisha kibaraka wake, Uhuru Kenyatta agombee urais na kumrithi. Baada ya Moi kuonywa kuwa angekiua chama bila kusikia, kundi lenye ushawishi mkubwa la Raila Odinga lilijitoa chamani na kujiunga na upinzani kiasi cha kuizamisha KANU.
Sasa KANU ni dhaifu na ya hovyo hata haifai kuitwa chama cha upinzani.
Hapa Tanzania bado tunakumbuka jinsi Nyerere alivyohusia kuwa upinzani wa kweli utakaoifurusha CCM utatoka ndani ya CCM.
Haiwi haiwi, sasa imekuwa. Ndani ya CCM, baada ya kuzika maadili ya uongozi, kuna kila dalili kuwa kama hali itaendelea hivi, Rais Kikwete ataingia kwenye historia kama mtu aliyewawezesha Watanzania kuzika chama nyemelezi.
Tujalie nguvu alizo nazo spika wa Bunge Samwel Sitta anayeandamwa na wale waliojitofautisha kama mashabiki na washirika wa ufisadi; akiamua kujiondoa CCM na kujiunga na upinzani, kweli kutakuwa na CCM kutawala milele kama makada walevi ndani ya chama wanavyotamba na kuamini?
Huu si uzushi. Kama vigogo kama Samuel Malecela, Dk. Harrison Mwakyembe, Fred Mpendazoe, Lucas Selelii, Christopher ole Sendeka, William Shellukindo, Anna Malecela na wengine wakiamua kukipiga teke chama, kutakuwa na chama tena kilichosalia?
Hili likichangiwa na udhaifu na utovu wa umakini katika chama, tuombe Mungu sana hali hii itokee ili CCM iwe kwenye benchi la upinzani kama KANU au UDF Malawi.
Ingawa ilipoandikwa kuwa Kikwete ameshindwa, kama alivyosema Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha wananchi (CUF), wale wanaomuunga mkono rais walikuja juu na majibu mepesi ya kujipa moyo kuwa mambo ni safi.
Migawanyiko na kuvuana nguo tunakoshuhudia ndani ya CCM ni cheche za kuimaliza CCM hata kama wahusika hawajui wala hawataki kujua na kulikubali hili.
Bahati nzuri kwa Watanzania na mbaya kwa CCM, kwamba udhaifu huu umejitokeza kipindi kifupi kuelekea uchaguzi huku CCM ikiwa imeshindwa kutekeleza karibu ahadi zake zote ilizotoa kwenye kampeni za uchaguzi.
Pia ufa huu umejitokeza wakati ambapo vigogo wengi wa CCM wakikabiliwa na tuhuma za wazi za ufisadi na kughushi vyeti vya taaluma.
Rejea CCM kudaiwa kumiliki makampuni ya Deep Green Finance na Meremeta; na wizi mkubwa uliofanywa kwenye akaunti ya benki kuu ya madeni ya nje (EPA) wakati wa utawala wa mwenyekiti wake mstaafu Benjamin Mkapa.
Angalia kubainika kwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa kushiriki ufisadi wa Richmond ambao hivi karibuni ulizidi kukigawa chama.
Rejea taarifa iliyotolewa na mwanasheria, Bhyidinka Sanze aliyeshuhudia mikataba ambayo hivi sasa inatajwa kuwa ya mashaka na mingine ya kifisadi iliyotumiwa kuchota mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu.
Hapa hujaongolea mitandao ya kuchafuana na kumalizana inayoendelea kukitafuna chama. Ingawa Kikwete aliambiwa aiue mitandao baada ya kuingia madarakani, hakufanya hivyo.
Leo ukiuliza mantiki ya Kikwete kushindwa hata kutaja mali zake au kuwabana wenzake wataje, hakuna atakayejitokeza kujibu. Wako wapi mashujaa wa kumjibia utadhani yeye ni bubu?
Chini ya Kikwete CCM imekosa msemaji. Kila mtu anasema lake, kwa wakati wake na namna yake. Rejea hivi karibuni waziri wa utawala bora usio bora Sophia Simba alipowashambulia wenzake kuwa ni mafisadi ingawa wanajifanya kupiga vita ufisadi.
Nao hawakusita kufichua udhaifu mwingine. Waziri mkuu na makamu mwenyekiti CCM wa zamani, John Malecela alinukuliwa akisema Simba ni “kichaa anayepaswa kuchunguzwa.”
Haya si madai mepesi. Je, inakuwaje Kikwete ateue watu vichaa kwenye ofisi za umma, ukiachia mbali wale walioghushi. Ajabu Kikwete huyuhuyu aliyeahidi utawala bora na maisha bora, ameshindwa kuwawajibisha hata kuwakemea. Je, huku siyo kushindwa kweli?
Pigo jingine kwa CCM ni kuendelea kuahirisha kashfa ya Richmond ikidhani ndilo jibu bila kujua kuwa kadri inavyoahirishwa ndivyo uoza na ushiriki wake katika ufisadi unazidi kuwekwa wazi.
Wananchi wameichoka CCM. Wamechoka kutawaliwa na serikali inayowaaminisha kuwa inapambana na ufisadi wakati ikiupamba; serikali inayowalaghai wananchi kuwa itawaletea maisha bora.
Yako wapi maisha bora miaka minne karibu na nusu tangu Kikwete aingie madarakani? Yako wapi iwapo akina mama wanajifungulia nje ya hospitali huku watawala wakishindana kununua mashangingi kwa fedha za maskini haohao.
Juzi ziliripotiwa habari kuwa walimu sita wa shule moja ya msingi wilayani Lushoto, wanaishi kwenye ofisi ya shule tena bila vyoo. Haya ndiyo maisha bora aliyomaanisha Kikwete?
Wakati wake zetu wakiendelea kufa wakijifungua, mke wa Kikwete anatesa na NGO yake akionekana kwenye kurasa za mbele za magazeti akimpigia kampeni mumewe kila mkoa kwa kisingizio cha kuhimiza maendeleo.
Wengi wanajiuliza, hivi kwanini mke wa Kikwete, kama ilivyokuwa kwa mke wa Mkapa, aanzishe NGO mara baada ya mumewe kuingia madarakani?
Ushahidi wa kushindwa kwa Kikwete ni gunia si debe. Bali katika kushindwa kwake, kuna jambo moja la maana anaanza kufanya. Anaua CCM; kitendo ambacho ni ukombozi kwa Watanzania.
Tuna kila sababu ya kumuunga mkono katika hili huku tukiwapa changamoto wanaobanwa wasipambane na ufisadi kuacha kuogopa kujiondoa katika CCM.
Je, mwanzo wa mwisho wa CCM umewadia na tunaanza kuushuhudia?
Chanzo: MwanaHALISI Nov. 25, 2009.
No comments:
Post a Comment