MIJITU mingine mipuuzi. Juzi nilitoa utani wa mwaka kwa kuwafunga kamba walevi wanipe ulaji; wajinga wakaubeba kichwa kichwa! Hamjui; msimu wa kamba umewadia?
Unajua ilikuwaje? Niliwatangazia walevi kuwa mwakani wakinipitisha kuwa mkuu wa kijiwe nitawatimua vikongwe wote na kuwapa vijana ulaji wao.
Thubutu! Kulaleki! Nani afanye kosa hili? Kama ni vijana nimeishawaandalia sera ya jembe kwanza mengine baadaye. Wamezidi kwa umachinga.
Kwanza, mie ni kijana wa miaka 60 japo wabaya wangu wanaongopa kuwa ni mzee. Hawaoni ninavyochana nikipiga pamba kama sina akili nzuri? Hawaoni Travotta na michuchumio yangu mingine mbali na kuulamba kama kina Pedejee.
Hawamuoni bi mkubwa wangu aliyekuwa amechoshwa na chaki? Tangu niukwae na ajue kujitona midhahabu na mikorogo kwa sana, hamuoni anazidi kuwa zungu kama mimi? Hamjamuona akizunguka kaya kila uchao kunipigia kampeni kwa kutumia mgongo wa asize yake ya Maulaji ya Wake za Wakubwa (MAWAWA)? Acha nijisifu kidogo. Kitu changu siku hizi chuma kweli kweli kiasi cha kunifanya nipunguze idadi ya dogo dogo wa nje.
Kuhusu hili la vijana, nikiamua kubatilisha kauli yangu, nani ataniuliza iwapo katiba ya kijiwe inaniweka juu ya sheria; ni muungu mtu? Waulize waliotaka niwatimue akina mbwa mwitu wameishia wapi zaidi ya kupiga piga kelele kama Chiwawa. Waulize walionibana niwatimue vihiyo na vighushi vya kijiwe. Nimekula pini nao wameula wa chuya. Hafukuzwi mtu.
Kwanza waelewe, wazee wengi ni marafiki zangu na wana pesa na siri nyingi kuliko vijana. Hata hivyo, msikonde. Kama mnataka tambara la zamani lenye viraka vipya mtapewa tu, lakini si nguo mpya.
Vijana wana tamaa wanaweza kumendea kiti changu cha mwenyekiti wa chama cha Ulaji, Ufisadi na Uongo (UUU) baada ya kuachia ukurugenzi wa kijiwe.
Hivyo, kufanya hivyo kunaweza kuamsha kesi zangu na mke wangu kuiba kashata na kahawa ukiachia mbali mazabe mengine ambayo walevi hawayajui na sitaki wayajue.
Washauri wangu wamenionya: msimu huu nisitoe ahadi nyingi. Hivyo, sitatoa ahadi zaidi ya hii hata kama ahadi nyingi zinalipa hasa ukishachaguliwa waweza kuziruka au kutotekeleza hata moja na walevi wasifanye kitu.
Hata hivyo ni rahisi kuwadanganya vijana. Wakishakuchagua, unawaambia: uliposema vijana hukumaanisha wenye chini ya miaka 60 maana Wazungu husema life begins at 40. Upo hapo? Hivyo usishangae ahadi ya vijana itakapoishia na lugha kama hizi.
Hata hivyo, hili halihitaji ramli. Litatokea muda si mrefu. Kaeni chonjo saa mbaya yaja walevi wataingizwa mkenge. Anayebishia hili ajiulize.
Kama juzi juzi walipoambiwa kuwa zee lenye miaka 50 na ushei ni kijana au jitu lililofadhiliwa na vibaka ni chaguo la Mungu.
Mtegemee nini? Jikumbushe sanaa za jamaa mmoja aliyesema akiula atateua vijana na ndani ya wiki hiyo akamteua kijana wa zamani mwenye umri wa miaka zaidi ya 700 kuongoza mamlaka ya Ngoongoo. Upo hapo?
Vijana si lazima wawe vijana ati. Hata vijana wa zamani ni vijana: wana sifa ya ujana japo wa miaka ileee. Hamkusikia kijana wa zamani mwenye miaka 112 nchini Somalia alivyooa bibi kizee mwenye miaka 20 na ushei hivi karibuni? Au hamkumsikia msichana mmoja mwenye miaka zaidi ya 100 nchini Malaya aliyeolewa na kijana mwenye miaka zaidi ya 50?
Pia naweza kucheza na maneno kuwa niliposema vijana, hawakinielewa, nilichomaanisha ni vijana wa zamani ambao wanajua mambo mengi ya kisasa kuliko vijana wa kisasa.
Hamuoni wanavyojidai na visichana vigori mitaani kwenye mashangingi yao? Hamkusikia yule aliyeka-preg kabinti ka skuli? Tulimhifadhi hadi alipoanza kutupekenyeua ndipo Bi Sofiii Fyatu akampa laivu.
Pia naweza kuwaambia ukweli kuwa kwenye nchi zilizoendelea au zile zilizokuwa zikitutawala zama zile za ujima, kumuita mtu mzee ni tusi na kosa linalokinzana na haki za binadamu ambapo kila mtu anapswa kufaidi kuitwa kijana hata kama ni ajuza.
Ukitaka kujua hili nenda Ulaya umwambie mzee ni mzee uone atakavyokutoa nishai. Najua hapa wasionijua watasema mzee Mpayukaji leo kachapia. Kwani aliishi lini Ulaya? Wasijue nilikulia na kuolea kule!
Kwani hamuoni vijana kama yule tumtaniaye kuwa ni babu wa chama fulani mwenye miaka zaidi ya 800 anayeendelea kupeta na ubunge wa kuteuliwa ukiachia wale wanaopaka piko na kanta kuficha mvi zao ili kuficha ujana wao?
Jamaa yule bado wamo. Anayepinga ajikumbushe kijana huyu wa zamani saaana anavyopayuka pale nonihino ikiguswa pabaya. Hata Joe Mgosi Machungi ni kijana ingawa aliwatania vijana kuwa amebakia miaka minne kurejesha namba.
Hata akirejesha namba kutokana na magonjwa yake nani atajua iwapo sisi vigogo huwa hatuugui wala kuzeeka? Isitoshe, ameishachuma kweli kwa ajili ya vitegemezi ukiachia kuvitafutia ulaji kwenye ngazi za juu za kijiwe. Hamjakaona kabinti kake kanavyotesa pale kwenye shirika la mifweza na mwanae anav’otesa kwenye ofisi ya Njaa Kaya?
Mara hii mmesahau wimbo wa bi kizee marehemu Aaliyah Age ain’t nothing but numbers. Upo hapo mshirika?
Usishangae kuambiwa mtu wa miaka mia ni mtoto na mwenye miaka 40 mzee. Maana siasa na sanaa ujanja wake ni kubadilisha uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo ilmradi wanaowekwa sawa wakubaliane na sanaa husika kama itakavyotokea hivi karibuni sehemu sehemu.
Hamkuona bi kizee mmoja mke wa rais fulani wa nchi jirani alipotinga kimini huku akionyesha ngoko zake chovu? Alipobanwa na wana habari akawaambia waache umbea.
Yeye anajijua bado wamo na mzee bado anammaindi kichizi. Hapa ndipo ilipo siri ya vipodozi, mikorogo na wake wa wakubwa kupenda kuupara ili waonekane vidosho hata kama ni vifutu au sura dume kama rafiki yangu Anae Tamaa Tunituni.
Kabla ya kusahau, nimemwamuru bi mkubwa atumie MAWAWA kuwaingiza mkenge wanawake na watoto wa kike. Ajionyeshe kuwa anawapenda- ingawa anawatumia kutengeneza njuluku- na ukuu wangu wa kijiwe ni ukombozi wao.
Nikichanganya vijana, wanawake na watoto wa kike bila kusahau waroho wa takrima, lazima nipete kama sina akili nzuri hata kama ngwe iliyopita sikukifanyia kijiwe chochote zaidi ya kuponyoa mipesa na kuwalipa fadhila washikaji wangu.
Ngoja kwanza niwape stori kabla sijasahau. Juzi nilipata zari la mentali. Nilipewa mwaliko na washikaji zangu wa Jamaicani ambapo nilipata ndung’u kwa sana ukiachia mbali kubembea kindayaya kama vitoto vya cha chekechea na bi mkubwa wangu kwenye bustani ya Richmond na kushangaa shangaa Eden Gardens.
Si mnajua alivyo limbukeni? Habanduki ubavuni kwangu nirukapo ughaibuni. Alivyojaza nilijua kibembea cha watu kingeporomosha mali zangu. Tulijinoma kwa pesa ya kijiwe kiroho mbaya.
Kukwepa kujua ufujaji wangu, nilificha majina na idadi ya watu nilioandamana nao kwenye matunuzi. Ila niliwafunga kamba kuwa nakwenda kuomba.
Nilikwenda kuomba nini na nilipata nini? Msiulize. Muhimu nimepata mwekezaji kwenye bembea. Hivyo, walevi wote mtaanza kubembea muonje maraha niliyokula Jamaicani.
Kwa ufupi ni kwamba kama vijana mtanipiga tafu basi jua nitaandamana nanyi kila safari zangu ughaibuni ili mle maraha bure kama mimi. Kuepuka yote haya chagueni vibabu kama Mwoi Kibaka. Havizururi nje kama mayanki. Mpo? Ngoja niwahi airport tayari kuelekea ughaibuni kutanua.
Khalas tamam.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 2, 2009
No comments:
Post a Comment