Wednesday, 30 December 2009

Shehe ubwabwa, shehena Mpayukaji awa mtabiri

BAADA ya mafsisadi wa kisiasa kugawana na kujibinafsishia kijiwe kiasi cha njaa na umaskini kutishia maisha yetu tusio katika siasa wala kuwa na taaluma ya kuweza kuajiriwa, mzee mzima nimebuni njia mpya ya kuishi bila kutoa jasho.

Nimeanza utabiri. Naitwa mtabiri maarufu wa dunia na sayari zote shehe Shehena Mpayukaji Alhaji Maulana, ulamaa Msemahovyo Abu Hikma.

Kuhakikisha nakula kiulaini, nimlenga wenye nazo hasa wanasiasa walioishiwa sera na mbinu za kuendelea kuula. We njoo kwangu usiku au tuma wapambe wakiwa na mshiko. Nitaitisha mkutano na waandishi wa habari na makanjanja halafu namwaga utabiri wenye kukufagilia hata kama mwisho wa yote utafulia. Baada ya hapo simo! Wangu ni mwenye kitu aso kitu asipoteze muda wake.

Sipigi ramli ati. Natabiri kisiasa. Msiniulize chama gani hata kama kinajulikana. Ukitaka kujua mie ni chama gani, jiulize bila kuwa na mshikamano na chama dume waweza kufanya usanii huu bila kunyea debe? Shauri yenu! Utabiri na dini vinalipa si kawaida! Unatabiri: maadui wa mkubwa wako watapukutika kama kuku wa kideri halafu unaondoka na uchache ukiachia mbali ujiko. Kufa kufaana bwana!

Hamjawaona mbweha na mbwa mwitu waliojivika uchungaji walivyotaka kufanya mavituz kumpa tafu jamaa yangu mchovu? Hamkumuona yule daktari kihiyo aliyejipachika uchunga wakati ni changu akiwakamata “walozi’ wakati ni usanii tu? Watu wanauza bwibwi chini ya majoho na kuukata mwabakia kutoa mimacho! Matapeli wanamtumia Yesu hadi wanapata uheshimiwa mnatoa mimacho!

Nawambia mtakwisha msipokengeuka. Shauri yenu! Watu wanatengeneza maisha, mnakalia imani na ushirikina uchwara. Siasa na dini ni mshiko hakuna cha God wala Kanaani.

Kwanza , nawapa ukweli mtupu. Watabiri wote duniani ni matapeli isipokuwa mimi nilisomea fani hii kule Hijaz. Japo maadui wananiita mshirikina mkuu na shehena, hata kama ni kweli yawahusu nini? Nani si mshirikina dunia hii? Msingekuwa washirikina, tena waheshimiwa, msingepwakia ushirikina wetu wala kuutegemea kuendelea kuula. Kwani siri?

Halafu kuna hii mipuuzi inayosema eti ninafuga majini. Afugaye majini na mnaofuga mafisadi kwa ujuha wenu yupi bora? Hivi matapeli na majuha nani wanafaa kuishi nao? Na wasanii na wasanifiwa?

Sasa tegeni masikio na mtie akilini. Natabiri kuwa watakaonipinga kwenye uchaguzi wa kijiwe ujao kama ni wanaume watabeba mimba huku wanawake wakiota ‘mustache’ na mizuzu na kutuna misuli. Natabiri kuwa kule kwenye rasi ya Zaainzibaa kutakuwa na kutapeliana ambapo watu wenye madevu watalizwa kiasi cha kutamani wangezaliwa nyuni.

Natabiri kuwa huko yule mwana wa mteule atataka kuendelea kufanya vitu vyake. Na atafanya hivyo baada ya kuvunja ndoa hii ya mashaka na kuwaacha jamaa wakionekana hawana maana kiasi cha kukimbiwa na mashabiki wao.

Natabiri mwakani, wafu, vibwengo, maruhani na majini watapiga kura ili kuleta ushindi mnono.

Pia natabiri kuwa mwaka ujao utashuhudia watu wengi kuwa mataahira na wenye kukosa kumbukumbu kiasi cha kurudia makosa. Natabiri kuwa chama cha Ulaji, Ufisadi na Usanii kitaendelea kutawala kijiwe chetu walevi wa kahawa huku mkuu wa kijiwe nikizidi kula kashata na kunywa tangawizi kwa sana na watu wangu nikijua sitakuwa na haja tena ya kuwa mkuu wa kijiwe. Natabiri kuwa mgosi Makambale Machungi Joe ataaga dunia kutokana na ugonjwa wa kupayuka kuzidi kuharibu nerves za ubongo wake.

Pia atakabiliwa na ugonjwa mwingine hatari wa cutaneous Kaposi’s sarcoma kisiasa hivi karibuni. Pia natabiri kuwa vihiyo wa kijiweni wengi wao watapigwa chini kwenye uchaguzi. Kule Buchosha, Ruvuma, Mwanza, Hanang, Bukoba, Dar es Salaam , Isimani na Mbeya vitasikika vilio huku vihiyo wakipukutika kama inzi.

Natabiri kuwa wachungaji uchwara wataongezeka mwakani na wengi wao watafanya utapeli wa kisiasa kuwasaidi wakubwa watakao kuwa wameishiwa sera na mbinu za kuendelea kukaa kwenye ulaji. Natabiri kuwa ndoa hii haitadumu. Kwani itavunjika baada ya uchaguzi mwakani.

Pia natabiri kuwa jina la mzee Mchonga litatumiwa na matapeli hasa wa Kihindi kutengeneza pesa. Hawa wakishirikiana na watakaokuwa na mamlaka, watajifanya wanampenda sana Mwalimu kiasi cha kutaka kumpoka toka kwa walio wake. Watatunga kila uongo kuonyesha watu wa Mwalimu ni mafisadi.

Natabiri kutakuwa na mshikamano zaidi wa wakubwa wa kijiwe na mafisadi hasa wenye uraia wa nchi nyingi na ndoa yao italeta maafa makubwa kwa kijiwe.

Alama ya mwaka ujao ni kenge, fisi na mbweha na mbwa mwitu walioshika upanga. Utakuwa ni mwaka wa nyakua nyakua kutokana na mbweha na fisi kuwa na tabia hii.

Pia utakuwa mwaka wa kuvurunda kutokana kenge kufanya ukenge. Utakuwa ni mwaka wa kuzidi wizi, uuzaji mihadarati na ufisadi kutokana na mwaka uliopita kujenga mazingira mazuri ya jinai hizi vikichangiwa na ugonjwa wa utaahira na ukosefu wa kumbukumbu kama utabainika.

Natabiri mwaka ujao utakuwa na ukeketaji mkubwa kiakili. Kutokana na alama ya upanga ulioshikwa na kenge, fisi, mbweha na mbwa mwitu tafsiri yake ni kwamba viumbe hawa kwa kuutumia huu upanga ambao ni alama ya madaraka watakeketa watu wengi kiakili. Hata hivyo kitu kizuri kitatokea. Hata hao watakao wakeketa wenzao mwisho watakeketwa kwa upanga wao huohuo.

Natabiri mwakani wanasiasa wengi nyemelezi watalamba matapishi yao kama wafanyavyo mbweha fisi na mbwa mwitu. Watavihama vyama vyao na kurejea walikokuwa wakikandia. Kutavunjika ndoa nyingi za kisiasa ingawa chache zitafungwa. Natabiri kiongozi mmoja maarufu wa chama cha upinzani atarejea CCM. Kiongozi huyu aliyewahi kujipatia umaarufu anatokea karibu na milima miwili mikubwa.

Pia natabiri kuwa kampeni za uchaguzi zitaanza kabla ya wakati wake huku wake wa wakubwa wakianzisha kampeni hizi kwa kuwapigia kampeni waume zao wazi wazi. NGO nyingi zitatumika kisiasa sawa na misikiti na makanisa.

Udini, ukabila, uanamitandao, urafiki na kujuana vitatawala kwenye uchaguzi ujao bila kusahau pesa nyingi kuibiwa toka kwa umma na kutumika kuuhonga umma uleule. Maana alama ya mwaka ujao ni ya ulafi, uroho, uharibifu, ufisadi na uziwi na upofu kwa watakao kuwa watawala.

Pia natabiri atakayeshinda uchaguzi ujao lazima awe na nyumba ndogo nyingi. Maana hii humaanisha kuwa na mafungamano mengi mabaya hata mazuri. Pia hii ni alama ya ujogoo.

Natabiri kuwa mwaka ujao kutakuwa na uhaba wa chakula kutokana upungufu wa mvua mashambani na mifukoni na wale ambao wangelima kukimbilia mijini kufanya umachinga ukiachia mbali kutengenezwa wezi na wezi wengi wapya.

Pia maisha yatakuwa magumu kuliko yalivyo na watu wengi watajinyonga badala ya kuwanyonga wanaowasababishia ugumu wa maisha. Wakati mvua zikiwa haba kwa walio wengi, walio wachache watakumbwa na mafuriko ya neema kiasi cha kukufuru na kuwaita mitume wahuni na wehu.

Kwa vile watakuwa wameshiba neema kama paka wa dukani, watachafua hewa kwa kutumia midomo yao. Mwanamke mmoja mkubwa atapata wehu na kupaswa kwenda kupimwa Milembe.

Kuhusu bara la Afrika, mtawala mmoja wa kijeshi aliyepigwa risasi na wenzake atafia ugenini akitibiwa. Na kwa mara nyingine Waafrika watagundua njia ya kuwamaliza muda wa madikteta wao au wale wanaong’ang’ania madaraka. Wasaidizi na marafiki zao watawageuka na kuwamiminia risasi.

Mwisho natabiri, atakayejifanya mnajimu mkuu zaidi ya mimi atakufa ghafla mwakani.

Kumbe niko jukwaani nikitembeza sanaa siyo? Bwinotu bwino!
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 30, 2009.

No comments: