Thursday, 25 February 2010

Mapenzi ya ulaji na kuokoa Valentine Idodomya

WAKATI watu wengi walisherehekea Valentine Day na wapendwa wao, mzee mzima nilisherehekea na kina Mbwa Mwitu aka Ewassa, Rost Time aka Kanji na washikaji wengine.

Tulikutana kwenye kijiwe cha kahawa cha mtaa wa Dodoma pale Ilala kuweka mambo sawa. Hii ni baada ya Sammy Sixx na wenzake kugeuka mwiba. Ila washikaji msikonde kwani tuliwasilimisha na kurejea mapenzi yetu ya zamani tukiwa kitu kimoja.

Kabla ya kuchonga vilivyo ngoja nikupe kidogo. Una habari mzozo huu ulinichelewesha kwenda zangu Umangani kujirusha na Shosto wangu?

Jingine, kwenye msafara wangu niliandamana na mafisadi papa wa nguvu ambao hata hivyo sikutaka watajwe zaidi ya kusema, niliandamana na wasasi ngawira kadhaa. Unajua maana ya kadhaa? Basi kama hujui kadhaa ni kadhia kwa walipa kodi wa kijiwe. Maana tulipunyua ndululu zao na kwenda kujinoma na washirika zangu. Bila usanii dunia hii huishi ukiishi utageuzwa punda na wasanii. Hayo tuyaache.

Mambo yalikuwaje? Tulivalia kijani kama alama ya kuzika tofauti zetu na kumalizia na nyekundu, alama ya mapenzi ya ulaji wetu na maafa kwa waliwaji na walevi wetu.

Wakati wengine wakienda kusambaza ukimwi, sisi tulisambaza ufisadi.

Kama siyo mzee Maneno pamoja na mzee Machale aka Mchekwa, kijiwe kingegeuka jehanamu baada ya akina Sammy Sixx kutaka kuwasulubu washirika zangu akina Mbwa Mwitu na Kanji.

Kwa vile sisi ni wanasiasia, tulisia sia mikakati na kuamuru ugomvi baina ya makundi mawili ufe vinginevyo tungewanyima jamaa nafasi za kugombea ulaji kwenye uchafuzi ujao. Upo hapo? Hii ndiyo siri ya akina Sixx kugeuka mbwa na kulamba matapishi yao.

Ile kashfa ya mkaa tuliyoibatiza Richmonduli nusu ikidedishe kigwena chetu cha UNM yaani Ugali Nyama na Maharagwe aka Chama Cha Maulaji kama wakiitavyo watani wetu.

Kuweka mambo sawa, mzee mzima niliteua kamati ya watu watatu kusuluhisha mafisadi na wasimafisadi. Nilimteua mkuu wa zamani wa kijiwe Ali Assaani Mwi..we koma we, Pio Mchekwa na Abdalaman Kiaina kusuluhisha tatange hili.

Wengi hawakustuka ni kwanini nilimchagua Pio wakati ana usongo na nongwa na Sixx. Nilimteua ili kwenda kuvuruga njama zozote za kuwawajibisha akina Mbwa Mwitu. Na ilikuwa hivyo. Kwani alifanya kazi ya kupigiwa mfano ya kuja na mapendekezo ya kuwaminya akina Sixx na hatimaye kuwageuza ndondocha wa hoja.

Kuwapata vizuri, alitumia Baibo huku Ali akitumia Al Koroani.

Najua waumini wa kweli wa dini watakuwa wanashangaa ni vipi shetani anaweza kutumia vitabu vitakatifu kulinda ushetani wake. Msishangae. Hizi ndizo siasa za kijiwe. Bila rongo rongo unafiki na hila hufiki popote.

Kama nilivyowamegea last week, Ewassa na mafisadi wenzake waliangusha pati ya kufa mtu. Mpaka tunaondoka mtaa wa Dodoma, akina Sixx walikuwa wanaonekana kama vyangudoa wa kawaida baada ya kuzimwa kama mshumaa wasifurukute. Unafanya mchezo na ulaji wa dezo? Hata hivyo walinifurahisha kitu kimoja; kusema kuwa wameamua kufyata mikia kwa kuogopa kunitia mzee mzima kwenye matatizo wasijue mie ndiye baba wa matatizo yote!

Jamaa niliwaona wajanja mwanzoni. Sikujua ni weupe kiasi cha kutojua kuwa mradi mzima wa mkaa niliuanzisha na kufaidika mimi! Au kwa vile jamaa wamelemewa na ulaji kiasi cha kutojitafutia habari na maarifa. Ukiwasikiliza wakipayuka utadhani wajanja kumbe kanjanja watupu. Viko wapi viapo vya akina Mwakiwembe kuwa kama tungeendelea kuwapuuzia wangetoboa siri? Utapeli mtupu. Nani hajui kaya hii ya wasanii na vyangu wa kisiasa?

Nakupa siri. Ingawa wameingia mkenge kuwa wakiacha uhasama watarejeshwa kwenye ulaji, nani afanye kosa hili? Hawa mambo yao kwisha. Harudi mtu wala nini. Afadhali wangekuwa wajanja siyo majuha wangeendelea na mkakati wao wa Chama Cha Jeuri ambacho tumekisambaratisha hata kabla ya kuzaliwa. Hakuna cha Chama Cha Jeuri wala Chama Cha Kupambana na ulaji wetu.

Tumewafanyia kitu mbaya baada ya wao kutaka kutufanyia kitu mbaya. Watoto wa mjini husema tumewafunga goli na sasa wana mimba za mafisadi wa kijiwe. Sie vidume ati. Kwanza tunajua kaya yetu ilivyo ya woga na wabangaizaji. wanaoendeshwa na matumbo yao badala ya vichwa hata wawe na elimu kiasi gani.

Mara hii mmewasahau wale madaktari akina Kusumbuka wa Miayo na Hasidi Kaboro! Walipojifanya wanajua huu nasi tukawaonya kuwa tunaujua ule. Tulisema beekhe! Hao wakanywea na kihoro mavi debe kama mbwa waliojaribu kuiba mafuta!

Wako wapi? Ni watoto wa watu sasa na wako kwenye kiama wametulia.

Muulize Meku wa Kilema. Siku hizi anaimba utukufu wangu baada ya kuexpire na kuishiwa. Naye kama wao analamba matapishi yake na kuyakoga kama nyoka baada ya kunyimwa miguu. Laana hiyo jamani. Laana hiyo! Imeandikwa. Kila mti utaujua kwa matunda yake.

Sisi chata kubwa bwana. Hamkusikia akinisifia kila siku utadhani yeye ni mgosi Machungi wa Makambale! Baada ya meku kupigwa na kisukari nasi tumempa sukari sasa analamba, aam! na kusahu aliyosema juzi. Unacheza na sukari nini?

Kwa kutumia sukari tumeua upinzani kiasi cha waliokuwa wapinzani kijiweni kugeuka wapambe na makada wa chama changu.

Kutokana na mapenzi ya Valentine hakuna anayefanya fyoko. Akifanya fyoko tunamwambia nyoko na kumkata mkia.

Hata akina Sammy Sixx wangefanya fyoko tungewapa talaka bila “haq tamat” kwa wanaojua kiarabu. Utampaje “haq tamat” changudoa? Hata ukimpa ni shiliingi mbili si maelfu sawa na mama mwenye kujiheshimu. Maana kwa kukubali yaishe wamejidhalilisha sawa na vyangu. Tumefanya hivyo kwa makusudi kuepuka kuchukuliwa na wapinzani wetu kijiweni.

Ukitaka kumkomesha mbwa mkate pua. Kwa tulichowafanyia hawa hata ukiwategeshea fisi bingwa wa uroho hawezi wagusa. Tumemaliza kazi na tukiingia kwenye uchafuzi tunapeta. Kwa maneno mengine hawa ndiyo wafu aliowatabiri shehe Ubwabwa.

Hakuna watu nawasikitikia kama wale waliokuwa wakiwaamini vyangu hawa. Maskini hawakujua kuwa kwenye fani ya usanii na mazingaombwe haaminiwi mtu bali ulaji! Sasa yamewakuta. Tutaona tambo na majigambo yenu yataishia wapi kama siyo kula jeuri yenu kama Chama Cha Jeuri ambacho tumekinyonga hata kabla ya kuiona mbeleko.

Tumalizie kwa kuowaonya walevi wanaoshabikia neno la God. Juzi tulimuona jamaa yetu Ka-tortoise pale Menge menge akiwashushia kibano Tanisiko. Kumbe kaya hii inaruhusu kila tapeli kujifanyia atakavyo! Haya ndiyo matokeo ya umbwe na kuendeshwa na mafisi na mafisadi. Mie simo. Ila tufikiri.

Ukija mgao wa umeme tunalalamika. Wakija mafundi tunawachapa! Mbona hatuna jema jamani? Mpaka kesho sijaamini kama tapeli wa mchana kama huyu angezuia shughuli za maendeleo kwa kaya. Ka-tortoise, elewa. Kumbi kumbi akikaribia kufa huota mbawa ili aruke na kunguru wamfanye kitoweo. Zako zahesabika ati.

Valentine Day mtaa wa Dodoma ilifana hasa kwa kuwapata wapenzi wapya akina Sammy Six na kundi lake. Walikuwa wanatubania. Sasa hawatubanii tena. Tunafaidi mavituz kama kawa. Naona gari la Sammy Sixx. Ngoja niende kuzomea na kumzodoa!
Chanzo: Tanzania Daima Feb. 24, 2010.

No comments: