OKTOBA mwaka jana ni mwezi wa kukumbukwa kwa wanaharakati wa kupambana na utapeli na ufisadi.
Mwanaharakati mmoja nchini, alikuja na matokeo ya utafiti wake uliodhaminiwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TUC). Utafiti ulianika mawaziri na wabunge kadhaa waliogushi sifa za usomi.
Utafiti huo uliofanyika kati ya 25 Juni na 9 Oktoba mwaka jana katika nchi za Marekani, India na Uingereza ambako vigogo walioshutumiwa walidai kuwa walisoma na kupata shahada shukiwa.
Ilitarajiwa baada ya kugundulika, vigogo hao wangechukua hatua zifuatazo: Kuachia nyadhifa zao kama njia ya kuwajibika na kupisha uchunguzi wa kina kufanyika ili ukweli halisi ujulikane.
Au kutoa utetezi unaoingia akilini badala ya kujirusha kimanga. Aidha, wangekwenda mahakamani kudai haki.
Hawakwenda.
Vinginevyo, bunge lingewatimua kazi kama wasingechukua hatua ya kujiwajibisha. Hata rais angewatimua wateule wake ili kutoa somo kwa wengine watakaokuwa wamefanya hivyo au kufikiria kufanya hivyo.
Bahati mbaya, sasa ni mwaka mwingine, hakuna aliyejiwajibisha, kuwajibishwa wala kutoa utetezi. Ajabu ni kwamba waliodaiwa kughushi na uadilifu wao kutoweka, bado wako kazini kana kwamba hakuna kilichotokea. Nchi ya ajabu.
Je, sheria zetu zinaanza kutumika kibaguzi na upendeleo kuwapatiliza wasio na mamlaka zikiwalinda wenye madaraka? Je, ndiko kujuana ambako kumekuwa kukilalamikiwa kuwa ndiyo sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)?
Je, kwa Bunge na rais kuacha kuchukua hatua kwa makusudi mazima si aibu na onyo tosha kuwa wako pale kwa ajili ya marafiki na washirika zao na si umma? Je, umma unaosalitiwa hivi una sababu ya kuziamini taasisi hizi mbili?
Kisheria, kuwasilisha hati za kughushi kwa mamlaka yeyote ni kosa la jinai ukiachia mbali kujipatia marupurupu na mshahara kwa kazi ambayo huna ujuzi wala sifa nazo.
Hapa tutaambiwa ubunge si kazi ya kusomewa. Lakini tukumbuke, ni utumishi wa umma unaotaka usafi wa hali ya juu.
Je, kuwadanganya wananchi, tume ya uchaguzi na taifa kwa ujumla huku ukijipatia mshahara kutokana na sifa usizokuwa nazo si kosa? Kosa hili lingetendwa na wapinzani mambo yangekuwaje?
Tunaanza kuwa taifa lisilo na kumbukumbu kutokana na unyeti wa suala hili na hatari kwa taifa. Tunalirejesha hili kwa hadhira ili umma uchukue hatua baada ya wahusika kugoma kuwajibika. Tulitegemea maandamano ya kushinikiza haki itendeke lakini wapi.
Kama siyo kuandamana kushinikiza wahusika waachie ofisi zetu basi, angalau kwenye uchaguzi kuwanyima kura kama hawatachukua hatua mujarabu. Tuurejeshe mpira kwa rais, Bunge na tume ya uchaguzi ili watende haki.
Maana tunaohujumiwa ni sisi na si wao. Tumkumbushe na ikiwezekana mawaziri sita wanaoshutumiwa kughushi vyeti na sifa hasa za udaktari wawajibishwe.
Tulishinikize bunge ambalo wabunge wake wanatuhumiwa kughushi pamoja na tume ya uchaguzi ambayo waliokuwa wagombea wake walipita ilhali kisheria hawakufaa hata kusimama kutokana na kutenda kosa la jinai linalohusiana na sifa za kuutumikia umma.
Kwa kuendelea kuwa na watu hawa kwenye nyadhifa zao ni taarifa tosha kuwa serikali, chama chao na hata tume ya uchaguzi wameridhika nao. Hivyo hata kwenye uchaguzi ujao watashiriki na kutumia mbinu za porini kuendelea kuula.
Kwanini rais anayetuaminisha kuwa atabadilika na kutimiza matarajio yetu hataki kuliona hili? Kwanini washauri wake hawalioni hili? Kwanini chama chake hakilioni hili? Na kwanini Watanzania hawalioni hili?
Chanzo: MwanaHALISI January 27, 2010.
No comments:
Post a Comment