How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Monday, 18 April 2011
CCM imejivua gamba lipi?
Hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuja na mpya- kinajivua gamba. Ajabu, badala ya kujivua gamba, kiliwafurusha katibu wake mkuu wa zamani Yusuf Makamba!
Makamba na wenzake si chanzo cha uchafu wa CCM wala gamba. Chanzo cha uchafu wa CCM kinaanzia mbali. Kinaanzia siku kilipotekwa na mafisadi hadi mwanzilishi wake marehemu Baba wa Taifa akaonya.
Uchafu wa CCM ulizidi kutoka kwenye doa hadi kusambaa mwili mzima mwaka 2005 ilipoamua kuiba pesa ya umma kugharimia uchaguzi ulioingiza serikali ya sasa madarakani. Wahusika hawajawahi kukanusha jinai hii wala kulitolea maelezo. Hii maana yake nini?
CCM ilitapakaa uchafu pale ilipoanza kampeni za mitandao ya kuchafuana na kumalizana ambapo baadhi ya watu, tena wenye uzalendo uliotukuka kama Salim Ahmed Salim waliambiwa si watanzania.
CCM ilizidi kuzama kwenye uchafu pale sumu ya uzee na ujana ilipoingizwa kwenye vinywa vya wasaka madaraka. Ajabu tulioambiwa vijana tuwachague walikuwa wazee!
CCM ilizidi kuchafuka na kufa pale mwenyekiti wake alipoogopa kufanya maamuzi magumu huku akiwakumbatia watuhumiwa wakuu wa ufisadi ambao hata kipindi hiki alipokwenda” kujivua gamba” aliogopa kuwafikisha mbele ya sheria akaamua kuwavunga wananchi kwa kuwatosa toka kamati kuu. Je angeweza kuwashitaki naye asishitakiwe kutokana nao kujua siri zake? Rejea tuhuma za CHADEMA za List of Shame ambazo hadi sasa inaendelea kushika hatamu serikalini na chamani.
CCM ilichafuka pale ilipobariki kila aina ya jinai kuanzia kutwaa nyumba za umma, mikataba ya uwekezaji ya kijambazi, kuchota pesa tena Benki kuu na kukosa sera na mwelekeo.
Je hadi hapa Makamba na genge lake ndio chanzo cha masahibu ya CCM? Kama hiki ndicho chanzo, wale waliotajwa na mjumbe wa ngazi ya juu ya Umoja wa Vijana wa CCM watawekwa kundi gani?
Hebu tujikumbushe yaliyonenwa kama chanzo cha kuharibika na kuparaganyika kwa CCM. Mrisho Gambo, Mjumbe wa Baraza Kuu wa Mkoa wa Arusha, alikaririwa akisema, “Nani hafahamu ukweli kuwa Lowassa na Rostam ndio wanaokipotezea mvuto CCM? Wananchi watakuwa na makosa gani wakihusisha Dowans na CCM wakati viongozi wake wakubwa ndani ya chama wanahusika na chama hakijawafanya chochote?”
Alisahau kuongezea Chenge. Je kuwavua ujumbe watuhumiwa inatosha badala ya kuwafikisha mahakamani?
Je pamoja na uzito na ukweli wa madai haya CCM imefanya nini kukabili na kutatua tatizo hili zaidi ya ngonjera za “nawapa siku 90,” lililotolewa na mwenyekiti?
Ina maana, CCM, licha ya ukweli huo juu, haijui kuwa kulindana na uenzetu ndivyo vyanzo halisi vya kuharibikiwa kwake? Je kuwatoa kafara akina Makamba kama ilivyotokea kwa Edward Lowassa kuinusuru serikali yake ni jibu mujarabu au chanzo kingine cha matatizo yake?
Huwezi ukawa na chama au serikali inayopewa ushahidi wa wazi kuhusiana na ufisadi kama ule wa rada na ndege ya rais vikauzima vikaendelea kuwa salama. Vyombo vya kijambazi namna hii haviwezi kuheshimika na kuaminika. Hata wakitumia msasa na “jik” kujisafisha –kujivua magamba, hawatatakata kamwe.
Je nyoka anavyojivua gamba anaacha kuwa nyoka? Nyoka ni nyoka na dawa ya kummaliza unyoka wake ni kumpondaponda na kumsigina kichwa. Kata mkia au vua gamba. Nyoka anaendelea kuwa nyoka kiumbe aliyelaaniwa kuliko wote.
Bila mwenyekiti ambaye ni rais wa nchi kufanya maamuzi magumu-kuwachukulia hatua za kisheria maswahiba wake mafisadi, CCM itaendelea kujifia taratibu. Inaweza kuendelea kujidanganya kuwa itaimarika kwa kugusagusa na kupangusa pangusa makovu. Dawa ya jipu ni kutumbua na si kuliosha tu.
CCM inaweza kujipa na kuishi kwa matumaini kuwa itatakata. Lakini haitatakata wala kukubalika tena kwa wananchi wanaokumbuka madhambi yanayowahenyesha kama EPA, IPTL, Richmond, Dowans, Kagoda na mengine mengi.
CCM haiwezi kutakata kwa ngonjera na mikakati haba na mfu. Wakamateni mafisadi papa muone kama umma hautawaelewa. Umma wa watu wetu si mataahira. Laiti CCM ingeamua kujiuzulu na kuitisha uchaguzi halali na si uchakachuaji ndipo ingejipima vilivyo.
CCM imejivua gamba lipi iwapo magamba kama ufisadi, mgao wa umeme, kuzorota kwa uchumi, wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma vinazidi kuongezeka?
CCM imejivua gamba lipi iwapo kila mhalifu aliyeko serikalini au chamani anaendelea kuhomola atakavyo? Rejea ripoti ya hivi karibuni ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ambapo upotevu awa mabilioni ya shilingi kwenye wizara na serikali za mitaa umeanikwa na serikali ya CCM haichukui hatua yoyote.
CCM imejivua gamba lipi iwapo uongo unaendelea kuwa sera yake? Iko wapi safari ya Kanani ya maisha bora kwa wote? Yako wapi mapambano dhidi ya ufisadi ambayo yamegeuka mapambo? Yako wapi mabadiliko? Inafikia mahali watu wanaikumbuka Misri ya Mkapa baada ya kuikosa Kanani ya Kikwete.
Gamba gani CCM imejivua iwapo mfumko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha vinaendelea kuwatesa wananchi wetu? Ni gamba gani CCM imejivua kwa kutuletea sura zile zile za watoto wa vigogo kurithi nafasi za wazazi wao? Rejea kuteuliwa kwa Nape Nnauye, Dk Hussein Mwinyi, Emanuel Nchimbi na Januari Makamba.
CCM haiwezi kujivua gamba kwa kuendekeza utawala wa kurithishana na kujuana. Haiwezi kujivua gamba. Sana sana imeongeza sumu kwenye mwili wake ili kutenda uharibifu zaidi baada ya kugundua sumu ya zamani (akina Makamba) inaanza kuishiwa nguvu.
Japo CCM inaweza kujiridhisha kwa kujidanganya kuwa imejivua gamba, ukweli ni kwamba anayeamini hivyo, hata kama anaonekana mtu mzima, anafanya utoto na ni wa hovyo. CCM imejivua gamba lipi?
Chanzo: Dira ya Mtanzania Aprili 18, 2011.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
4 comments:
Naafikiana na wewe, Mhango. Huwezi ukavua gamba wakati kichwa cha nyoka bado ni cha zamani. Na huyo mwenyekiti hawezi akawachukulia hatua mafisadi wakati mwenyewe ni mmoja wapo na yeye mwenyewe hakuingia hapo kihalali, kama ulivyoelezea. Kama naweza kuazima msemo wa kizungu, "case of the pot calling the kettle black."; hamna ubaya kuwa mweusi, isipokuwa ni kuonyesha hii interdependence ya ufisadi ilivyotanda CCM kama utando wa buibui.
Jaribu uko sahihi. Sema watu wetu ni wanafiki. Utawasikia wakisema mwenyekit ana nia ya kupambana na ufisadi eti wasaidizi wake wanamwangusha. Kwani wao ndio wanaofanya maamuzi zaidi ya yeye aliyeapa kufanya hivyo na asifanye hivyo?
Bila nyoka (CCM) kukatwa kichwa (Kikwete) ataendelea kung'ata watu tu.
Kitu cha kushangaza ni kwamba nilisoma kuwa alikuwa anawakasirikia wenzake kwenye huo mkutano wa Halmashauri ya CCM kuwa wanajua hao mafisadi ni nani na waache unafiki wawataje. Mtu mmoja jasiri, (by CCM standards at least), akawataja hao usual suspects, Chenge, Rostam na Lowassa; lakini hamna aliyethubutu kusema kuwa yeye mwenyewe anashukiwa kuwa fisadi wa kutupa. Nafikiri na yeye aliuliza makusudi aone kama kuna mtu yoyote atakayejitoa mhanga na kumtaja yeye. Si unajua, good defense is offense.
Jaribu, ni kweli wenzake waliogopa kumwambia kuwa mchawi anayemtafuta ni yeye mwenyewe. Wao wamemwogopa. Sisi tumemtaja. Ni kazi kwa watanzania kutusikiliza na kumshughulikia kama anavyotaka kuwashughulikia wenzake. Ama kweli nyani haoni nonihino lake!
Post a Comment