How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Wednesday, 6 April 2011
Hii ndiyo dawa niliyopewa na ‘Sir God’
WIKI mbili zilizopita nilitangaza nilivyoonana na ‘Sir God’ na akanipa maagizo kuwa niwatibu watanzania na walimwengu wengine ambao wameshindwa kupata huduma hii kutokana na serikali zao kulamba njuluku zote.
Mwitikio wa watu haukuwa kidogo. Naendelea kutoa vikombe hata kwa majini. Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko kuwa kuna matapeli wanaiba taaluma hii na kujitangaza kuwa nao wameota. Inabidi ieleweke. Mimi sikuoteshwa bali kuonana na mwenyewe mtoaji ambaye kila mtu anamjua hata kama hakumuona.
Nasisitiza ili muelewe. Mimi sikuota na wala sifanyi mambo ya ndoto wala kutafuta kujaza tumbo na vijipesa vichafu vya mafisadi na maskini wa ulimwengu huu.
Hao wote wanaodai kuoteshwa msiwaamini watawaua bure na miugonjwa yenu hasa miwaya. Tangu lini ndoto za Alinacha zikawa ukweli? Mwaambiwa mara ngapi. Yaani mnaamini mindoto tu! Kweli mna akili nyinyi? Nani aliwaroga nyie Watanzania wapumbavu ambao kila kitu kimewekwa wazi mbele zenu?
Hivi mtastuka lini au mshikwe wapi ndipo msistuke? Hamkusikia yule babu yao akisema eti mkinywa vikombe vyake muendelee kutumia dawa za hospitalini? Mie nasema. Ukitumia dawa yangu hauna haja ya kula, kunywa wala kufanya nini bali kudunda tu.
Kutokana na kuona matapeli wakizuka wengi, nimeamua kuwatajia dawa ninayotumia ambayo ni sumu ya panya, mti uitwao mpayushi na kahawa. Kwa hiyo mimi situmii mimaji bali kahawa.
Siku ‘Sir God’ aliponiambia nitumie sumu ya panya kama tiba nilishangaa sana. Bahati nzuri aliona wasi wasi wangu na kusema: ‘Unanitilia shaka hata mimi?” Nilijibu kwa unyenyekevu: utakalo na liwe.
Nilimuuliza kwanini ameniteua mimi na dawa ya panya? Akasema kuwa dawa ya panya ni sumu tena huu viumbe wenye akili ndogo na waroho.
Hivyo, nikiichanganya na kahawa na mpayushi nitatenda maajabu. Maana itafanya kazi kinyume. Badala ya kuondoa uhai kwenye mwili wa binadamu itaondoa uroho na ujinga.
Unajua panya ni wajinga kuliko viumbe wote? Maana hata wakijificha kwenye shimo lao huwa hawaachi kupiga kelele.
Kwa hiyo adui yao atajua walipo. Pia wakiingia kwenye nyumba ya mwenyewe huigeuza kuwa yao. Wataitana wajomba, shangazi, kila aina ya panya kuja la vya mwenyewe.
Bwana ‘God’ alisema kuwa ametumia dawa ya panya kutokana na wagonjwa wangu kuwa na tabia na akili kama za panya. Alisema: “Panya huguguna kila kitu tena bila kunawa na hunya pale pale alapo sawa na mafisadi ambao ndiyo walengwa wangu wakuu ingawa kwa wasio mafisadi natibu magonjwa yote sugu.
Kuhusu dawa ya mpayushi ni kwamba itatibu kwa kuwafanya wagonjwa yaani mafisadi kupayukiana wakubwa kwa wadogo tena bila kuheshimiana. Hii ni dalili tosha kuwa mgonjwa anaanza kurejea kwenye hali yake ya kawaida kiakili na kiroho. Hili limeishanza kujitokeza kule kwenye chama cha nonihino ambapo mipasho baina ya wagonjwa inasikika na kuandikwa kila siku magazetini.
Hamkumsikia Jose Makambale akipeana vipande na Rozishy Bwanji bila kusahau Mgando akiwapa vipande vyao akina Ewassa na Roast Tamu kuwa ndiyo wanaoidedisha Tanzia?
Nani alitegemea baba zima kama Makambale kudandia mambo ya nguoni kwa kitoto kinacholingana na binti yake Mwaviza? Je, huko si kuishiwa kunakopaswa kushughulikiwa nami? Nawahimiza wahusika waendelee kunywa dawa hadi watakapopona gonjwa la ufisidi na uroho na roho mbaya.
Mtaona na kusikia mengi. Watavuana nguo kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Watatiana midole kwenye mimacho hata kutiana ngeu. Laana itawafuata na kuwatafuna hadi dawa itakapomaliza kufanya kazi ya kuiondoa.
Hao wote mnaowasikia nimeishawapa kikombe changu cha kahawa ya tiba. Hayo ndiyo matokeo ya mti wa mpayushi. Watapayukiana hadi wastukie ulaji ukiwatoka na washangae pale watakapoanza kutupwa lupango mmoja mmoja.
Hata hivyo najivunia mafanikio yaliyopatikana haraka. Wale waliozoea kuona sinema za wakuu kuanguka hovyo hovyo wasahau kuziona tena.
Juzi alipita kijiweni kwangu usiku akapata kikombe chake na sasa hali si haba anazidi kunawiri na kurejesha kumbukumbu, aibu na kupunguza kuchekacheka na masihara.
Pia jikumbushe. Kama si kikombe cha kahawa, Freddie Sumuye asingepata ithibati ya kuyaambia mapanya kuwa tatizo si paka bali mipanya yenyewe kuguguna kila kitu ingawa mapanya yanajitahidi kumkatisha tamaa. Sumuye alikuja kwangu usiku na kupata kikombe chake.
Ingawa wote wamekuja na kupata kikombe cha kahawa bado namngoja shehena mkuu ambaye naye siku hizi amekumbwa na ugonjwa wa kuharisha kwa mdomo. Anajipayukia hata bila kufikiria kiasi cha kutia aibu taasisi aliyopewa na genge la mafisadi kuiongoza.
Pia ifahamike. Ukweli wa tiba yangu hautegemei na upuuzi kama ninaosikia. Ukimuuliza mtu kwanini anawaamini waota ndoto na matepeli anakwambia eti hata mawaziri wamekwenda na kunyweshwa kikombe. Kwani uwaziri au ukuu unaondoa upumbavu na upofu na upogo wa mtu?
Ingekuwa hivyo mafisadi wasingehangaikia kula mabaki ya mabwana zao wakati mabaki hayo yanatokana na mali ambayo ni halali yao kama taifa.
Leo natumia maneno yenye kuudhi ili watu wanielewe. Ukuu au elimu ya mtu si kitu.
Nimalizie kwa kuwahimiza wale wanaopwakia kila upuuzi unaowaaminisha kuwa watapona wajikumbushe wachungaji na wahubiri wa uongo kama Paulo Kibwetere na David Kolesh au Vernon Wayne Howell walioteketeza waumini wao wapumbavu walipowahadaa kuwa wana majibu ya matatizo yao.
Nifunge kwa kuwapa mipango yangu ya baadaye. Nitatoa vikombe kwa rahis na mawiziri wote ili waondokewe na pepo la ufisadi, uvivu na usanii wawatumikie vema muondokane na mgao wa umeme, uongo na kuishi kwa matumaini.
Du! Kumbe mbona umeme unakatika wakati wa masika au ni kwa vile wahusika hawajaja kunywa kikombe kuondoa tatizo hili! Khalas kweisine.
Chanzo: Tanzania Daima April 6, 2011.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
2 comments:
Niko na wewe Mhango. Kama Babu angekuwa anatoa kikombe cha kuimarisha akili na uwezo wa kifikiri, ningekuwa nasupport watu kumiminika huko.
Ingawa utawala wa Nyerere ulikuwa na kasoro zake, lakini ulikuwa hau-entertain upuuzi huu. Watu walikuwa wanaenda kwa waganga kwa siri. Siku hizi madokta na maprofesa wametapakaa kila kona na wachawi wanadondoka kila siku kama geese waliopigwa risasi. Of course hamna mtu aliyewashuhudia in-flight, kwa sababu serikali ingebidi iagize radar nyingi za kitapeli kuweza kudhibiti hii air traffic.
Asante Jaribu kuliona hili hivyo.
Tuna msiba mkubwa. Hii ni baada ya watu kuweka rehani roho na akili zao kiasi cha kuwa desperate na kupwakia kila upuuzi. Kila uchao babu anabadili stori ya "unabii" wake na miiko ya "dawa" yake.
Alianza na madai kuwa dawa yake inatibu ndani ya siku moja. Mara amekuja na wiki mbili. Baadaye anadai watu wainywe na kuendelea na dawa za hospitali. Mara inaongeza nguvu za kiume na upuuzi mwingine mwingi. Tumetelekeza mijadala muhimu kuhusiana na ufisadi wa hasara yetu. Jamii na taifa kama letu ni hasara na kichekesho katika karne hii ya sayansi na teknolojia. Wakati wenzetu wakipaa sisi tunapiga mbizi kwenye ujinga na upumbavu! Ni msiba sina mfano.
Post a Comment