Thursday, 5 May 2011

Sasa ni vita kuvuana magamba

Kuna usemi maarufu kuwa kumbikumbi akikaribia kufa huota mbawa na kupaa ili kunguru wamtafune. Hili ndilo linalokikabili Chama Chama Mapinduzi (CCM) baada ya kuja na usanii uitwao kujivua gamba.

Sasa tujiandae kushuhudia mnyukano na mpambano baina ya CCM hasa yale makundi ya kimaslahi maarufu kama mitandao. Huu ni ushahidi kuwa hata ajivue magamba vipi nyoka atabaki kuwa nyoka. Isitoshe hakuna kuishiwa kama huku ambako ni kiashiria cha mwanzo wa mwisho wa CCM. Tumpongeze Rais Jakaya Kikwete kuwa wa mwisho kupigilia msumari kwenye kaburi la CCM. Ama kweli waliosema yeye ni chaguo la Mungu, hawakukosea!

Turejee mitandao. Kimsingi, mitandao hii ya wasasi wa mali na madaraka ndicho chanzo kizuri cha kuporomoka na kuchukiwa kwa CCM. Maana, iliundwa mahsusi kutafuta madaraka. Ili kupata madaraka lazima uwe na fedha ya kuhongea wapiga kura hasa wakati ule takrima ikiruhusiwa. Ili kupata pesa lazima ushiriki ufisadi. Nani hakutumia kanuni hii kuanzia mwenyekiti na wale waliotimuliwa?

Kimsingi, mitandao ndilo chaka la ufisadi wote tunaopigia kelele bila kusikilizwa. Tulisema hadi sauti zikakauka. Wahusika walitupuuzia na kutuona wazushi na wenye wivu wa kike. Waliendelea na business as usual kulindana, kufadhiliana na kuzidi kushikamana katika jinai. Maskini hawakujua kuwa mambo hubadilika. Baada ya umma kuwastukia, hatimaye nyufa zilianza kujitokeza na kukisambaratisha Chama bila kuiacha serikali yake.

Kinachoshangaza ni ile haya ya sasa ambapo mitandao, yenye ama madaraka au ukaribu na wenye madaraka, kuanza kuitafuna ile inayotishia madaraka kutoka mikononi mwake ama kutokana na kuchusha au kuliana njama.

Hali inazidi kuwa mbaya hasa ikichangiwa na ulevi wa madaraka kiasi cha watu kujihisi na kujiona hawagusiki, ndiyo CCM ilizidi kutota.

Sasa baada ya wenye (wana) nchi kuiadhibu kwenye uchaguzi mkuu uliopita ikanusurika kwa kuchakachua, CCM, hatimaye, imezinduka na kutia akili ikiwa imechelewa sana. Kutaka kuendelea kuwaridhisha na kuwaibia wale iliowadharau na kuwaibia kwa muda mrefu, CCM ilikuja na usanii wa kujivua gamba. Katika kufanya hivyo ilijivua kigamba kidogo cha mkiani huku ikiacha gamba lenyewe liendelee kutuna! Je tatizo la nyoka ni sumu au gamba?

Kwa wanaojua mshikamano na ushirika wa CCM katika kutenda jinai kama vile wizi wa fedha ya umma toka Benki kuu chini ya fuko la EPA, watakumbuka jinsi jinai hii ilivyo kama mduara. Si mkubwa si mdogo wote wamo- (mtego wa panya) wamechafuana. Hakuna msafi CCM kuanzia mwenyekiti hadi mfagia ofisi.

Baada ya kukaa Dodoma na kufanya kile wazungu huita Cosmetic Changes (CC) kwa kutoa shinikizo kwa vigogo wake waliotaja sana waachie ngazi, CCM , kama mtoto mchanga ajipakae maji tumboni akiamini ameoga, ilikuja na majigambo kuwa imejivua gamba wakati gamba bado linaonekana.

Kwa vile CCM wamejifanya vipofu kiasi cha kudhani na watanzania ni vipofu, hatuna shaka sasa wale waliojeruhiwa na sanaa hizi watatwambia mengi. Hii maana yake ni kwamba nguvu ilivyokuwa ikitumika kuwahonga wanahabari wenye roho na tamaa za fisi, itaelekezwa kuwarudi waliowajeruhi. Sitashangaa kuona yale magazeti yaliyonunuliwa kwa pesa ya EPA kuanza kuwashughulikia walioidhinisha wizi huu.

Na hii ni matokeo ya watu kufanya maamuzi bila kuangalia matokeo yake. Tunajua CCM baada ya kuona umma umewastukia na hasa ikichangiwa na kinachotokea kwenye baadhi ya nchi, walikurupuka na kutosana kama walivyozoea wasijue, si jibu. Hili haliwezi kuwa jibu lenye kuingia akilini kutokana na umma kujua yote yanayofanyika chamani na serikalini. Watu wanajua nani ameiba kiasi gani akimtumia au kusaidiana na nani. Wanajua kuwa chanzo cha mchezo huu licha ya ufisadi ni kulipana fadhila, kujuana, kulindana na kutoona mbali.

Haiingii akilini, kwa mfano, watuhuhumiwa wa EPA watolewe kafara wakati waliofaidika na wizi huo wakiachwa wawe ndio waamue nani atoswe na nani abaki. Hapa ndipo wenyeviti wa CCM yaani Benjamin Mkapa (mwenyekiti mstaafu aliyeasisi skandali ya EPA) na Jakaya Kikwete hawana jinsi ya kupona hata kama watatumia maguvu ya madaraka yao.

Wengi watauliza Mkapa naye alinufaika vipi? Bila kuasisi EPA unadhani angenusurika kufikishwa mahakamani? Wakipona ni kwa muda. Ukweli wa matokeo haya utajulikana mwaka 2015 ambapo CCM piga ua itajikuta kwenye benchi la upinzani huku kesi nyingi zikifumka.

Kwa kosa walilotenda CCM wajue fika, kufikia kwenye uchaguzi wa 2015, watakuwa wamechafuka zaidi ya sasa kutokana na wale waliotemwa kumwaga mboga ili wote wakose. Hii ni silka ya binadamu. Na hili litakamilisha utabiri wa mwanzilishi wa CCM marehemu baba wa taifa kuwa atakayeibomoa CCM atatoka CCM.

Na hakika huyu si mwingine bali Kikwete na genge lake la washauri na waramba viatu.vyake, ataibomoa CCM sawa na wenzake wakishirikiana naye walivyoanza kuibomoa walipotelekeza maadili ya uongozi na kushabikia madili. Je mwanzo wa mwisho wa CCM upo nasi? Hata wajivue ngozi achia mbali gamba unyoka na sumu yao vitaendelea kuwaandama.
Chanzo:Tanzania Daima Mei 4, 2011.

No comments: