Sunday, 8 May 2011

Wanadamu tuogopeni sisi siyo Mungu


Hivi karibuni kumetokea wimbi la baadhi ya matapeli wanaojitangaza kuwa watetezi wa manfisadi. Wamedangaya na kuumiza wengi hasa wajinga na maskini wenye matatizo ya kimaisha.

Hivyo usishangae kusikia "askofu au mchungaji" fulani akitetea fisadi wake mwenye madaraka. Mara nyingi, matapeli hawa hawatumwi na wanayemtetea bali kutaka kujipendkeza kwake ili awatupie mabaki ya fedha zitokanazo na ufisadi.

Yesu aliacha busara moja kuhusiana na matapeli hawa wanaotumikia matumbo yake kwa kisingizio cha neno la Mungu. Hawa hawamtumikii Mungu bali kumtumia kuneemesha tamaa na matumbo yao. Tuwaogope kama ukoma. Tukimbie makanisa yao na kupuuzia mahubiri yao.Yesu aliwalinganisha hawa na chui wenye kujivika ngozi ya kondoo ili wawararue kondoo.

Yesu aliwajua vizuri. Alisema kuwa utawajua kwa matunda yao. Ni muhimu kuwatahadhari. Wanatamka maneno mazuri na kutenda shubiri.

Hawa matapeli wa kiroho hawako peke yao. Wapo waandishi wa habari mitondoo ambao wako tayari kujidhaliiisha wao familia zao, taifa na taaluma zao ili washibe kwa mabaki yatokanayo na ufisadi. Tuliwaona wakati wa uchaguzi mwaka 2002 hata 2010. Wamejiweka rehani na kuhatarisha usalama wa jamii ili wajazwe makombo na uchafu vitokanavyo na ufisadi jinai inayosaliti utaifa na jamii.

Bahati mbaya sana, baadhi ya mafisadi wanamilki hata vyombo vya habari na waandishi uchwara wenye roho zilizokaa mifukoni mwao badala ya vifua vyao. Je hawapo? Hebu soma magazeti ya kila siku uone ukweli wa haya yanayoandikwa. Kuna wahariri na waandishi ambao ni vigumu kuwatofautisha na dodoki au nepi. Wanatumiwa na hawastuki wala kuangalia mbele wala nyuma bali mifukoni.

Kinachokera ni ile hali ya wananchi kutoa pesa yao ya maana kusoma uchafu wa maajenti wa mafisadi. Vyombo vyao vya habari vinajulikana kwa majina na mahali vilipo bila kusahau hata hawa mafisadi wanaovinunua na kuvitumia.
Kuna kipindi unashindwa kutofauti kichwa na kiuno cha mtu viko wapi kutokana na anavyojirahisi na kutumiwa.

Turejee kwa wanaojipachika uongozi wa kiroho wakati ni waroho wa kawaida. Ni wangapi sasa wanatumia kila mbinu kutangaza uongo na utapeli wao kwa mfano wanaouita ufanya miujiza wakati ni upuuzi wa kawaida? Juzi kulitokea ugomvi baina ya mbweha hawa waliovaa majoho na babu wa Loliondo. Babu anatafuta kula kwa kutumia mawazo na shuhuda za ndoto akitetea uganga wa kienyeji kwa kuupa umungu. Wao walipoona anatikisa wakaanza kulia lia.

Ni wangapi tulikuwa tumezoea kuwaona wakijisifu kutenda miujiza ya kupata utajiri wakati ni wauzaji wa kawaida wa madawa ya kulevya?
Baadhi yao walipopata vyeo vya kisiasa hatuwasikii wala kuwaona! Tunaowaona na kuwasikia ni wale vidhabu wachungaji wa kujipachika na wanasiasa wa msimu ambao huibuka na kutokomea wanapopewa chao. Je hawa wanaweza kweli kuwa watu wa Mungu au muungu pesa na mafisadi?

Tutawalaumu matapeli hawa kwa kujipendekeza kwa watu wachafu huku wakimtumia Mungu. Vile vile waumini wanaoshindwa kuwapiga teke au kutowapa hizo sadaka wanazotumia kupata umaarufu na kutaka kuwaridhisha mafisadi ili wawakati kitu kidogi hata kibwa. Maana bila ya waumini hawa matapeli ni bure.

Kimsingi waumini ndiyo mtaji mkubwa umaarufu na ndoto za kuwa karibu na mafisadi wakubwa ili wawatumie kupata mabaki.

Hivyo, siri ya kuwamaliza ni kuwakimbia na kutosikiliza ulaghai wao. Waumini wanaweza kujikuta wakichangia kuenea na kutamalaki kwa ufisadi bila wao kujua. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Matapeli hawa wa kiroho waliojaa roho mtakakitu bwanayemuita mtakatifu wanalijua hili. Ndiyo maana huendelea kuwalewesha mateka wao ili wawatumie.
Tumalizie na kisa cha hivi karibuni ambapo gaidi wa kimataifa Osama bin Laden licha ya kuuawa kama mbwa alifichuliwa unafiki na woga wake. Alikuwa akihimiza watu wampiganie Mungu na wasiogope lakini yeye aliisi kwa kujifungia nyuma ya kuta na walinzi. Je kwanini hakumuacha Mungu wake amlinde kama kweli alikuwa akiamini katika Mungu? Bin Laden aliwahimiza watu kuwa mashahidi tena wasioogopa! Ajabu ya maajabu yeye akikuwa mwoga kuliko hata panya! Ajabu nyingine watu wenye mtindio wa akili walimwamini, kumuabudia na kumtumikia bila kutumia hata chembe ya akili.

Ajabu nyingine ni ile hali ya mahasidi wa Bin Laden-Marekani kuonewa huruma wakati wao ndiyo walimtumia na kudhulumiana naye. Nani anajali kupoteza muda kidogo kutafuta ukweli hata kama mchungu umuweke huru.

Tumalizie kwa kusema wazi kuwa hatuna kundi wala upande linapokuja suala la utapeli na kugeuza na mabwege. Viongozi wa kidini wanaojipendekeza kwa mafisadi wanaweza kuwa ima mafisadi wenyewe na wabaya kuliko hata hao mabwana na miungu yao waitwao mafisadi. Je hamkuwsikia wengi wakiwatetea kwa kisingizio cha amani na kuwambea?
Tunawahimiza waumini na wananchi kwa ujumla kuwaogopa mbweha hawa waliojivisha majoho kuliko hata ukoma na ukimwi.
Chanzo:Dira ya Mtanzania Mei 9, 2011.

No comments: