The Chant of Savant

Friday 5 August 2011

Chenge na Lowassa wanangoja aibu zaidi?


Ingawa watuhumiwa wakuu wa ufisadi wanaopaswa kujivua gamba wanaamini kuwa hawana hatia, mazingira ya kuwajibishwa kwao yanaweza kuwa ushaidi wa kimazingira tosha kuwaona wana hatia. Baada ya aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa mbunge wa sasa wa Monduli kutakiwa na kamati teule ya bunge kujipima na kuamua na akaamua kuachia ngazi, ilitosha kumfanya aonekane ana hatia. Vinginevyo asingeachia madaraka kama aliamini hakuwa ametenda kosa lolote. Kwanini aliamua kuachia ngazi kama kweli hakuwa amehusika na kashfa ya Richmond iliyoliingizia taifa hasara na kulitumbukiza kizani? Majibu sahahi ya maswali haya ni kumburuza Lowassa na wenzake mahakamani ili haki itendeke. Pia, kama watakutikana na hatia mali walizochuma zitaifishwe.

Baada ya kuachia ngazi baada ya kujipima, Lowassa hivi karibuni alisikika akijaribu kujitakasa bila mafanikio. Alikituhumu chama chake kinachomtuhumu kuwa gamba kuwa na ugonjwa wa kutofanya maamuzi mazito ingawa uamuzi wa kuwataka Lowassa na wenzake waachia ngazi si rahisi. Maskini Lowassa hakujua kuwa kumshughulikia yeye ni sehemu ya maamuzi hayo magumu anayohimiza wenzake wafanye bila kuchelea lawama. Na kwa kuzingatia ushauri wake, Lowassa hana sababu yoyote ya msingi kulalamika kuwa anaonewa au amelengwa kwa sababu ya azma yake ya kugombea urais ambayo hata hivyo hajawahi kuiweka wazi ukiachia mbali mikakati yake kuonyesha hivyo. Lowassa alikwenda mbali zaidi kutaka wananchi wawapime uwezo wa watendaji naye akiwamo wakati baadhi yao walikwishajipima! Wananchi, kwa mfano, wampime Lowassa kwa lipi wakati alikwishajipima na kuamua kuachia madaraka kutokana na kuridhika kuwa alitenda makosa? Hata hivyo Lowassa na wenzake wana bahati. Maana kwa makosa wanayotuhumiwa kutenda na matokeo ya makosa haya, ingekuwa nchi za wenzetu, maandamano ya kushinikiza wakamatwe yasingezuiliwa na risasi wala mabomu. Hata hivyo, taratibu tutafika huko kama wahusika wataendelea kuwaona wananchi waathirika kama woga na mataahira wasiojua lolote.

Tukija kwa Andrew Chenge waziri na mwanasheria mkuu wa zamani almaaruf kama mzee wa Vijisenti, naye kama Lowassa,hana bao tena ikizingatiwa kuwa hajawahi kutoa utetezi wowote kuhusiana na tuhuma zinazomkabili. Hawezi kukwepa kuhusika na ufisadi wa Rada kwa sababu rahisi kuwa hajawahi kukana kuwa na akaunti kwenye visiwa vya Jersey yenye pesa taslimu zaidi ya shilingi 1,500,000,000. Pili hajawahi kutoa maelezo ya jinsi alivyopata hiki kiasi kikubwa cha pesa na kwanini aliamua kuzificha nje. Hajawahi kueleza alivyosafirisha hiyo pesa ambayo kimsingi alitorosha.

Hakuna ubishi kuwa kikao cha Kamati Kuu (CC) Chama Cha Mapinduzi kilichomalizika hivi karibuni mjini Dodoma kimewaacha watu wengi hoi? Kimeionyesha CCM kama chama ‘kinachojipiga mtama’ hata kuchechemea na kuogopa baadhi ya makada wake ambao wanaendelea kukigharimu. Ingawa CCM imekuwa ikilaumiwa kwa mizengwe kujuana na kulindana, kwa kushinikiza watuhumiwa hawa papa waachie ngazi ni mwanzo mzuri kama kuna mpango wa kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki.

Kinachogomba ni hii hali ya kuvuta vuta miguu kuwashughulikia vilivyo. CCM inawabembeleza watuhumiwa. Na pia bado hawa hawatoshi kuna wengine wanaopaswa kuachia ngazi mfano wale waliotuhumiwa kughushi shahada na jinai nyingine. Hawa matapeli nao ni magamba kwa chama. Hivyo kuna haja ya kuishauri CCM izidi kujichunguza vilivyo ili magamba zaidi yaporomoshwe. Kadhalika, chanzo cha magamba matatu ni tuhuma za CHADEMA pale Mwemba Yanga. Hivyo wahusika wajue kuwa orodha bado ni ndefu. Maana ufisadi unaodaiwa kufanywa unawagusa wengi.

Turejee kwa magamba ambayo yameishatajwa kwa majina na kupewa la kufanya-yaani kuachia ngazi kama lilivyofanya gamba la kule Igunga, Rostam Aziz. Kwanza, walipewa siku 90 zikapita na hakuna kilichofanyika zaidi ya mmoja wao kujiondoa siku ya 92.

Sasa wamepewa mwezi mmoja ambao ni siku 30 je watajiondoa? Je wakiendelea kung’ang’ania kama walivyofanya miezi mitatu iliyopita na CCM ikaendelea kuwagwaya, umma ufanyeje? Maana pesa iliyoibiwa na kufichwa nje au iliyolipwa Richmond si ya CCM bali watanzania wote bila kujali vyama vyao.

Siku moja baada ya kikao cha Kamati Kuu (CC), mmojawapo wa watahumiwa wakuu Chenge alikaririwa akikikejeli chama na maazimio yake kwa kusema: "Sijui kama mimi ni gamba," Sambamba na kejeli hii, Chenge aliendelea kuwataka wananchi wa jimbo lake kupuuzia uongo unaosemwa juu yake. Je hii ni dharau kiasi gani kwa mtu ambaye asingefika hapo alipo kama si chama kumuunga mkono? Je ni ile shukrani ya punda au mtoto umleavyo? Je CCM bado ina haja ya kuendelea kuwafunga mafisadi? Je jeuri ya Chenge na Lowassa inatoka wapi? Kuna wanalojua ambalo wakilimwaga hadharani kuna watakaoumbuka au ni jeuri tu na harakati za mfa maji? Je ni ile hali aliyoieleza katibu wa uenezi wa CCM Nape Nnauye kwa nukuu hii?

“Samaki ana nguvu akiwa ndani ya maji tu, ukimtoa hakuna kitu tena wala hana ujanja na hivyo hata hawa wanatusumbua wakiwa ndani ya chama lakini tukiwatimua hawana mahali pa kuegemea,’’

Je kama Nnauye anamaanisha anachomaanisha huku kusuasua na kuchelewa ni vya nini wakati wahusika wakizidi kukipasua na kusambaratisha chama kadri mambo yanavyozidi kucheweshwa? Je CCM itawatoa majini samaki wake baada ya mwezi mmoja kama ilivyoahidi? Wengi wangetaka kuona CCM ikijivua magamba mengine mengi makubwa na kuona itakuwa na sura gani.

“Ni heri kupoteza jimbo au kata halafu tukarudi kwenye uchaguzi maana ndiyo njia pakee ya kukisafisha CCM kuliko kuendelea kung’ang’ania wachafu kwenye chama chetu.” Kama maneno ya Nnauye yatatekelezwa, si haba CCM inaanza kurejea kwenye mwelekeo ilioupoteza baada ya kukumbatia na kutekwa na mafisadi wachache wakiitumia kwa maslahi binafsi.

Tumalizie tulipoanzia. Je Chenge na Lowassa wanangoja aibu zaidi au kutunishiana kwao misuli na CCM mwisho wake utakuwa upi? Yetu macho.

Chanzo: Dira ya Mtanzania Agosti 4, 2011.

2 comments:

Anonymous said...

You got great points there, so I always visit your blog, it seems that you are an expert in this field. keep up the fantastic work, My friend recommends your blog.

My blog:
taux pret consommation www.rachatdecredit.net

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Many thanks for comments and visiting me. Keep doing that. I am no expert in the field. I am trying to share what I know with others as my contribution for the emancipation of my country.