The Chant of Savant

Tuesday 30 August 2011

Hongera Luhanjo na Jairo



Kwa mara nyingine mhimili mmoja wa dola yaani utawala umeuumbua mhimili mwingine yaani bunge kwa kuuonyesha ukuu na ujabari wake.

Wabunge walipotoa shutuma za kuwepo rushwa na ubadhilifu kwenye wizara ya Nishati na Madini hawakujua kuwa walikuwa wakitaka kuwagusa wasiogusika. Zilipotolewa shutuma kuwa katibu mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, David Kitundu Jairo alikuwa akitaka kujipatia pesa kwa njia zisizo halali kwa lengo haramu wengi walidhani Jairo angeshughulikiwa vilivyo. Walikosea hasa wakati huu ambapo mauzauza na mazingaombwe ni sehemu ya maisha ya kawaida. Wabunge walikosea kutaka kukata tawi kutokana na sumu ya mti mzima. Walikosea sana kudhani kuwa nyoka akivuliwa gamba anaacha kuwa nyoka. Wengi walitegemea matokeo haya. Unategemea nini kesi ya tumbiri inapohukumiwa na nyani?

Maneno ya Luhanjo yanaeleza hali halisi. Alikaririwa akisema, “Nawaonya watumishi wa umma wanaotoa siri za Serikali…, tutafuatilia tujue nani alitoa barua kwa mbunge, akipatikana atapewa adhabu,” Kumbe mchezo wote ulikuwa siri! Siri ya nini kama hapakuwa na namna?

Kwa busara zake na mapenzi wa taifa na uadilifu, katibu kiongozi Philemon Luhanjo aliamua kuwaacha uchi wabunge kama onyo kutowagusa wasioguswa. Wengi tulishangaa mantiki ya kumuandama Jairo huku tukiwafumbia macho mabosi wake yaani waziri wa nishati William Ngeleja na naibu wake Adam Malima.

Isitoshe, haikuwa mara ya kwanza kwa wizara ya Nishati na Madini kufanya madudu tena makubwa kuliko hili la kuhomola na kutaka kuwahonga wabunge. Nani haoni walivyofanikiwa kuliweka taifa kizani kwa miaka bila kuguswa? Nani haoni madudu haya ambayo kimsingi yanadhoofisha hali za maisha ya watu na uchumi wa nchi? Kuna kosa kubwa kama hili la kuhujumu taifa?

Hivyo basi, shutuma za mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo hata kama zina kiwango kikubwa cha ukweli kuliko uongo zimefanywa kuonekana fitina badala ya msaada kwa taifa hasa linalojidai kupambana na ufisadi na uvunjaji wa maadili. Nani hajui kuwa maadili yamepinduliwa na madili?

Kwa hukumu safi ya Luhanjo, kwanza, inaonyesha wabunge ni wambea na wafitini. Pili wabunge wanaonyeshwa kama wala rushwa hasa katika kupitisha bajeti za hovyo kama walivyofanya kwenye bajeti za wizara za nishati, utalii na mali ya asili.

Je wabunge watatahayari na kunywea au kujikusuru na kutaka wahusika washughulikiwe? Nani atawashughulikia wateule hawa? Je wabunge watanywea na kuonekana kama wala rushwa wa kawaida wanaoweza kuhonga pesa kidogo na kupitisha bajeti zinazowaumiza waliowachagua kuwawakilisha? Nini kitafanyika au ndiyo imetoka? Je namna hii tunajenga taifa la namna gani ambapo kila mhalifu anaposhitakiwa huachiwa na aliyemshitaki kuonekana mfitini na mtu asiye na lolote bali fitina?

Kwa uamuzi wa kumrejesha kazini Jairo, Luhanjo ameonyesha busara ya hali ya juu. Kwanini ahangaike na mjumbe wakati waliomtuma wanaendelea kupeta? Je alichofanya Luhanjo ni haki au kuwasuta wakubwa wasiowawajibisha wateule wao? Je rais atakubaliana na uamuzi huu wa kustua na kulindana huku ukimtia doa kuwa hana ubavu wa kupambana na mafisadi papa? Je ni wangapi wamepewa nguvu na kutiwa moyo na uamuzi huu wa aina yake unaowapa mwanya wa kuendelea kutenda watendavyo bila kujali kelele za wale watakaostukia madudu yao?

Baada ya kutolewa tuhuma waziri mkuu Mizengo Pinda alimwamuru mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), Ludovick Utoh na si TAKUKURU, “kumchunguza” Jairo. Baada ya “uchunguzi” wake Utoh alikaririwa akisema, “Pia taasisi hii ililipia gharama za tafrija iliyofanyika Julai 18 jioni katika Ukumbi wa St Gasper Dodoma kwa gharama ya Sh 6, 141,600, pamoja na kuwa bajeti haikupita, tafrija ilifanyika kwa kuwa maandalizi yalishafanyika na hata gharama ingelipiwa tu,”

Matokeo ya “uchunguzi” wa Utoh yanaacha maswali mengi kuliko majibu. Je Ewura waligharimia tafrija hii ya kuwalisha wabunge kama nani na ili iweje? Je wabunge kwa kufanyiwa tafrija siyo hongo? Je hapa kosa ni mkosefu kumshitaki mkosefu mwenzake? Kwanini serikali ilimtumia mkaguzi wa hesabu za serikali ambaye kimsingi alipaswa kuwa shahidi kama mtaalamu? Je kazi ya mkaguzi wa hesabu za serikali ni kuchunguza watuhumiwa au kukagua hesabu za serikali? Je huu si mgongano wa maslahi kati ya serikali na bunge? Hivi nani alitegemea mkaguzi wa hesabu za serikali ambaye naye ni mteuliwa kama Jairo aiaibishe serikali yake? Je kwanini Bunge halikuunda kamati huru kuchunguza kashfa hii?

Maswali yanazidi kuongezeka kutokana na majibu ya CAG. CAG alisema katika uchambuzi huo, imebainika kwa uhakika kuwa malipo yaliyofanyika yalihusu posho ya kujikimu, takrima na posho za vikao kwa maofisa walioshiriki katika shughuli nzima ya kuwasilisha bajeti ya wizara na kwamba hakuna ushahidi wa malipo kwa wabunge.

Je CAG hajui kuwa takrima ilipigwa marufuku kutokana na kuwa rushwa ya wazi? Je kwa wizara kutoa takrima na wabunge kuipokea wakati ni wao walioibatilisha si kutoa na kupokea rushwa?

Ukiachia mbali uamuzi wa Luhanjo kuacha maswali mengi kuliko majibu, umemvua nguo waziri mkuu ambaye alikerwa wazi na tuhuma hizi ila kwa vile Jairo hakuwa mteule wake aliichia jukumu la kumshugulikia Jairo mamlaka iliyomteua.

Kabla ya mazingaombwe na sarakasi kuingizwa, Pinda alikaririwa akitoa msimamo wake akisema,

"Kwa jinsi jambo hili lilivyokaa, hakuna jinsi mtu unavyoweza kulitetea hata kidogo, nilitamani sana kwamba nije hapa niseme kwamba uamuzi wangu mimi ni huu, lakini haikuwezekana," alisema Pinda na kuongeza: "Kwa dhati kabisa naomba wabunge tuwe na subira, mara tu mheshimiwa Rais atakapotua South Africa (Afrika Kusini) jioni ya leo (jana), nitamuarifu na ninaamini tutaelewana kuhusu hatua za kuchukua." Hii ni nukuu ya tarehe 18 Julai yalipotolewa madai haya.

Ukiachia mbali kuvuliwa nguo waziri mkuu, hata wabunge wa CCM waliotaka Jairo afukuzwe kazi kuwa ni pamoja na Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Esther Bulaya (Viti Maalumu), George Simbachawene (Kibakwe), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki), Henry Shekifu (Lushoto), Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini), Alphaxard Lugora (Mwibara), Shellukindo (Kilindi) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli nao watakuwa wamevuliwa nguo pia.

Tuhitimishe kwa kuwapongeza Jairo na Luhanjo kwa kuokoana ingawa uamuzi huu hauna faida wala maana zaidi ya kuzidi kuionyesha serikali kama legelege kama walivyowahi kusema wapinzani. Je tutaendelea na madudu haya na kulindana hadi lini? Hata hivyo, bila kushughulikiwa Ngeleja na Malima, Jairo angeonekana bangusilo maana hawezi kufanya kitu bila wao kuridhia.
Chanzo: Dira Agosti 29, 2011.

No comments: